1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yachukua uongozi wa operesheni ya Libya

25 Machi 2011

Uamuzi wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO kuchukua uongozi wa operesheni za kijeshi dhidi ya Libya umepokelewa vyema kwenye jumuiya ya kimataifa, huku jitihada za Umoja wa Afrika kuutatua mgogoro huu kisiasa zikiendelea.

https://p.dw.com/p/10hHy
Katibu Mkuu wa NATO, Jenerali Anders Fogh Rasmussen.
Katibu Mkuu wa NATO, Jenerali Anders Fogh Rasmussen.Picha: dapd

Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen, ametangaza uamuzi wa jumuiya yake kuchukua rasmi jukumu la kuongoza operesheni ya kijeshi dhidi ya utawala wa Libya, ikiwa ni utekelezaji wa Azimio Namba 1973 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lililoiwekea nchi hiyo marufuku ya kuruka ndege kwenye anga lake.

"Jumuiya ya NATO sasa imeamua kusimamia amri ya marufuku ya anga kwa Libya. Tunachukua hatua ikiwa ni sehemu ya juhudi za kimataifa kuwalinda raia dhidi ya mashamulizi ya utawala wa Gaddafi." Amesema Rasmussen.

Kwa vyovyote vile, huu ni uamuzi uliokuwa ukingojewa sana na jumuiya ya kimataifa, zikiwemo Uingereza, Marekani na Ufaransa, mataifa ambayo, hadi sasa, ndiyo yanayoongoza kampeni hiyo.

Serikali ya Uingereza imeuita uamuzi huo kuwa ni "hatua muhimu ya kusonga mbele", huku msemaji wa Waziri Mkuu, David Cameron, akisifia pia mchango wa ndege 12 za kijeshi kutoka kwa Umoja wa Falme za Kiarabu.

Nchini Ufaransa, uamuzi huu wa NATO umemfanya mkuu wa majeshi ya ulinzi, Admirali Édouard Guillaud, kuhitimisha kuwa sasa operesheni ya majeshi ya washirika nchini Libya itaendelea kwa wiki chache tu na sio miezi.

Huko Brussels, ambako viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana kwa siku ya pili leo kujadiliana masaibu ya uchumi wa eneo lao, wamekuwa pia wakijadiliana suala la Libya.

Umoja wa Afrika watafuta suluhu ya kisiasa

Viongozi wa Umoja wa Afrika
Viongozi wa Umoja wa AfrikaPicha: AP

Huku hayo yakiendelea, mjini Addis Ababa, Ethiopia, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Jean Ping, anatarajiwa kukutana na wawakilishi wa serikali ya Libya pamoja na wale wa waasi, katika jitihada za Umoja huo kuutatua mgogoro wa Libya kwa mazungumzo.

Umoja wa Afrika umekuwa ukipinga vikali uingiliaji kati wowote wa kijeshi dhidi ya Libya, na unasisitiza kuheshimiwa kwa mamlaka ya taifa hilo la Afrika ya Kaskazini.

Hata hivyo, kwa kuwa nchi za umoja huo ni wanachama pia wa Umoja wa Mataifa, na kwa kuwa Umoja wa Mataifa ndio uliopitisha azimio la kuiwekea Libya vikwazo vya anga vilivyopelekea uingiliaji kati kijeshi, mataifa kadhaa ya Afrika yanajikuta yakifungwa mikono nyuma.

Katibu Mkuu wa Umoja Mataifa, Ban Ki-moon, anasema kuwa hadi sasa, utawala wa Muammar Gaddafi haujaheshimu azimio hilo la Baraza la Usalama, na kwa hivyo kuna uwezekano wa hatua zaidi kuchukuliwa.

"Hakuna dalili ikiwa utawala wa Libya umechukua hatua za kutekeleza maazimio namba 1970 na 1973. Na ikiwa Libya itaendelea kukaidi utekelezaji wa azimio namba 1973, ujumbe wangu umesema kuwa Baraza la Usalama linaweza kupaswa kujitayarisha kwa hatua nyengine zaidi." Amesema Ki-moon.

Uganda kuzuia mali za Gaddafi

Rais Yoweri Museveni wa Uganda
Rais Yoweri Museveni wa UgandaPicha: DW/Schlindwein

Na katika hali isiyotarajiwa, Uganda, ambayo imekuwa rafiki mkubwa wa Gaddafi, imesema iko tayari kuzizuia mali za serikali ya Libya zilizomo nchini humo.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor la Uganda, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Okello Oryem, ameliambia Bunge la nchi hiyo kwamba mali zote zinazomilikiwa na utawala wa Gaddafi nchini mwake zitazuiwa kwa kufuatana na azimio la Umoja wa Mataifa.

Uganda inakuwa nchi ya mwanzo ya Kiafrika kutangaza uzuwiaji wa mali za Gaddafi, ambapo inakisiwa kuwa miradi ya Mamlaka ya Uwekezaji iliyo chini ya mtoto wa Gaddafi, Saif al-Islam, inafikia thamani ya Euro bilioni sita kwenye nchi mbalimbali barani humo.

Nchini Uganda peke yake, mali za Libya zinafikia thamani ya Euro milioni 300, zikiwa zimeekezwa katika miradi na makampuni mbalimbali ikiwemo kampuni ya simu ya Uganda Telecom, Shirika la Ujenzi na Nyumba, hoteli ya Viktoria na mradi wa kujenga bomba la mafuta kati ya Kenya na Uganda, Tamoil.

Uganda ni miongoni mwa wajumbe wa kamati maalum ya Umoja wa Afrika inayotafuta suluhu ya mgogoro wa Libya.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/DPAE/Reuters
Mhariri: Othman Miraji

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi