1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yaionya Afghanistan kuhusu mustakabali wake

4 Desemba 2013

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa jumuia ya kujihami ya NATO wametuma onyo kali kwa viongozi wa Afghanistan katika juhudi mpya za kuusaidia mustakabali wa nchi hiyo iliyoharibiwa na vita

https://p.dw.com/p/1ASeq
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekano John Kerry (kushoto) na Katibu Mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen (kulia)Picha: Reuters

Lakini maafisa wamewachana na vitisho vya awali vya Marekani kuyaondoa majeshi yote kama rais wa Afghanistan Hamid Karzai hatakubali kusaini makubaliano hayo ifikapo mwishoni mwaka huu.

Maafisa hao wa NATO wamesema kuwa wanahitaji uamuzi haraka ili waweze kuandelea na mafunzo yao ya kijeshi nchini Afghanistan baada ya mwaka ujao. Kama hapatakuwa na ufafanuzi, takribani mataifa 50 yaliyosema yatasaidia kipindi cha mpito cha Afghanistan kutokana na miaka 13 ya vita yatalazimika kuanza kupanga namna, na lini, yatawaondoa wanajeshi wao nchini humo.

Muda unazidi kuyoyoma

Lakini Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani John Kerry na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya NATO Anders Fogh Rasmussen wote wamesisitiza kuwa Karzai ni lazima afanye uamuzi wa haraka. Viongozi hao wawili wameionya Afghanistan kuwa inahujumu mustakabali wake pamoja na msaada wa kifedha kutoka kwa jamii ya kimataifa kwa kuchelewesha kusaini makubaliano ya mpango wa usalama. Rasmussen amesema hawezi kufuta uwezekano wa kuondolewa majeshi yote ya kigeni nchini Afghanistan mwishoni mwa mwaka wa 2014. "Kama mpango huo hautasainiwa, hatutapeleka majeshi yetu na msaada unaopangwa utakabiliwa na kitisho".

Mawaziri wa Mambo ya Kigeni wa Jumuiya ya NATO wakikutana mjini Brussels, Ubelgiji
Mawaziri wa Mambo ya Kigeni wa Jumuiya ya NATO wakikutana mjini Brussels, UbelgijiPicha: Reuters

Karzai aliuidhinisha mpango huo kwa muda, lakini akawashangaza washirika mwezi uliopita wakati alipokataa kuisaini baada ya kupitishwa na baraza la wazee linalofahamika kama Loya Jirga. Baraza hilo lilisema muafaka huo usainiwe mwishoni mwa Desemba jinsi Marekani inavyotaka. Badala yake, Karzai anasema uamuzi unapaswa kufanywa na mrithi wake baada ya uchaguzi wa Aprili mwaka ujao.

Ujerumani iko tayari kuchangia

Waziri wa mambo ya nchi za Kigeni wa Ujerumani Guido Westerwelle amesema nchi yake imejiandaa kuchangia katika kutoa mafunzo ya wanajeshi wa Afghanistan baada ya kumalizika kwa operesheni za kivita. Westerwelle amesema "Ni lazima kila mtu ajue msimamo ni upi. Na kwetu sisi ni wazi kwamba tuko tayari kusaidia Afghanuistan baada ya mwaka wa 2014. lakini mazingira lazima yawepo. Ndio maana mipango ya usalama, na makubaliano ya kiserikali ni muhimu na pia pande zote zisimame pamoja".

Foleni ya maroli yanayosafirisha vifaa vya Jumuiya ya Kujihami ya NATO kutoka Afghanistan kupita Pakistan
Foleni ya maroli yanayosafirisha vifaa vya Jumuiya ya Kujihami ya NATO kutoka Afghanistan kupita PakistanPicha: Reuters

Ujerumani ina kiasi ya majeshi 3,500 ambayo yana wajibu mkubwa kaskazini mwa Afghanistan. Hata hivyo Westerwelle ameonya kuwa muda unaendelea kuyoyoma. Haijawa wazi kama Marekani na NATO watafuta mipango yao ya kutoa mafunzo kama muafaka huo hautasainiwa. Kufikia sasa wamewapa mafunzo zaidi ya wanajeshi 345,000 katika mwongo mmoja uliopita.

Na wakati hayo yakijiri, jeshi la Marekani limesitisha usafirishaji wa vifaa kutoka Afghanistan kupitia Pakistan, likiyataja maandamano ambayo yanatoa kitisho kwa madereva wa malori. Hatua hiyo ilijiri baada ya wanaharakati waliobeba virungu kaskazini mwa Pakistan walipoyakagua kwa nguvu malori ambayo yamebeba vifaa vya NATO, ili kulalamikia mashambulizi yanayofanywa na ndege za Marekani zisizoruka na rubani.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Hamidou Oummilkhheir