1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yaionya Urusi

30 Agosti 2014

Jumuiya ya kujihami ya NATO imeionya Urusi Ijumaa(29.08.2014)kuhusiana na kile ilichokieleza kuwa ni ukiukaji wa mipaka ya Ukraine baada ya mataifa ya magharibi kuishutumu kwa kujihusisha katika kuchochea mzozo huo.

https://p.dw.com/p/1D3x0
NATO Generalsekretär Rasmussen 29.08.2014
Katibu mkuu wa NATO Anders Forgh RasmussenPicha: Reuters

Hofu ya mvutano mkubwa zaidi umeongezeka baada ya NATO kusema Urusi imetuma vikosi vya wanajeshi kupigana nchini Ukraine na kuingiza idadi kubwa ya silaha kuwapatia waasi wanaounga mkono Urusi katika kile Ukraine ilichosema ni uvamizi.

"Hili sio tukio pekee, lakini ni sehemu ya utaratibu wa hatari katika muda wa miezi kadhaa kuiyumbisha Ukraine kama taifa huru, " katibu mkuu wa NATO Anders Forgh Rasmussen amesema, akielezea hatua ya Urusi ya kupeleka majeshi katika mpaka kuwa ni "ukiukaji dhahiri" wa mipaka ya Ukraine.

Ukraine Konflikt Separatisten bei Kriegerdenkmal in Savur Mohyla bei Donesk
mapambano katika eneo la mashariki mwa UkrainePicha: Reuters

Urusi yashutumiwa

"Tunaitaka Urusi kusitisha hatua hiyo kinyume na sheria ya kijeshi , kuacha kuwasaidia wapiganaji wanaotaka kujitenga, na kuchukua hatua mara moja kuelekea kupunguza mzozo huu.

Ukraine na mataifa ya magharibi zinasema majeshi ya Urusi yanaongoza mashambulizi ambayo yameshuhudia waasi kukamata tena maeneo ya ardhi katika eneo la kusini mashariki kutoka kwa majeshi ya serikali, na kubadilisha ghafla hali ya mambo katika mzozo huo wa karibu miezi mitano sasa.

Ukraine Konflikt Separatisten bei Kriegerdenkmal in Savur Mohyla bei Donesk
Wapiganaji wa mashariki mwa Ukraine wanaotaka kujitengaPicha: Reuters

Rais wa Urusi Vladimir Putin amekuwa akikana mara kwa mara kuwa Urusi inachochea uasi ama ina wanajeshi wake ndani ya ardhi ya taifa hilo lililokuwa zamani moja ya majimbo ya iliyokuwa umoja wa Kisovieti.

Jana Ijumaa (29.08.2014) ameitaka serikali ya Ukraine ifanye mazungumzo muhimu na wanaotaka kujitenga ambao wamechukua silaha na kupambana na serikali ya mjini Kiev tangu Aprili mwaka huu, akielezea mzozo huo kuwa ni maafa makubwa.

Umoja wa Ulaya kuchukua dhidi ya Urusi

Wakati huo huo viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana mjini Brussels leo Jumamosi(30.08.2014)kupanga jibu kuhusiana na hatua ya Urusi kuhusika zaidi katika Ukraine na kuingiza sura mpya katika nyadhifa za Umoja huo.

Wladimir Putin Rede Belarus Treffen mit Poroschenko
Rais Vladimir Putin wa UrusiPicha: Reuters

Viongozi 28 wa taifa na serikali wataketi kwa mazungumzo wakati shutuma zinamiminika dhidi ya Urusi kwamba vikosi vya jeshi la nchi hiyo vinahusika katika mapigano ndani ya ukraine, huku kukiwa na hofu inayoongezeka kwamba Ulaya huenda hivi karibuni ikakabiliwa na vita kamili katika mpaka wake wa mashariki.

Ni wiki tano sasa tangu mataifa ya Umoja wa Ulaya kuimarisha vikwazo vyake dhidi ya Urusi , lakini kwa imani ya jumla ya mataifa ya magharibi kuwa Urusi hivi sasa ina majeshi yake moja kwa moja ndani ya Ukraine, Umoja wa Ulaya uko katika mbinyo kuchukua hatua.

Ukraine Russland Petro Poroschenko und Wladimir Putin
Rais Petro Poroshenko (kulia) wa UkrainePicha: CHRISTOPHE ENA/AFP/Getty Images

"Tabia kama hii haiwezi kupita bila kuchukuliwa hatua, " kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema siku ya Alhamis huku NATO ikisema kuwa kiasi ya wanajeshi 1,000 wanapigana vita ndani ya Ukraine.

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko ni mgeni aliyealikwa katika mazungumzo hayo ya Jumamosi , akialikwa kutoa maelezo ya hali ilivyo kwa sasa baada ya kukutana ana kwa ana na rais wa halmashauri ya Umoja huo Jose Manuel Barroso na rais wa baraza la Umoja huo Herman Van Rompuy.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Amina Abubakar