1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yalaani uhalifu wa Wikileaks

Thelma Mwadzaya30 Julai 2010

Ujumbe wa Jumuiya ya kujihami ya mataifa ya magharibi,NATO,ulioko nchini Afghanistan umelikosoa vikali tukio la hivi karibuni la kuvuja kwa hati za siri za kijeshi.

https://p.dw.com/p/OXp3
Kamanda wa jeshi la Marekani na kikosi cha NATO nchini Afghanistan Jenerali David Petraeus na Katibu Mkuu wa NATO Anders Fogh RasmussenPicha: AP

Nyaraka hizo ziliyafafanua mazingira ya vita vya Afghanistan.Kwa mujibu wa msemaji wa ujumbe wa NATO, Brigedia Jenerali Josef Blotz waUjerumani,tukio hilo huenda likayahatarisha maisha ya raia wa  kawaida.Msemaji huyo wa NATO aliusisitizia umuhimu wa kuyakomesha matukio  ya aina  hiyo na kwamba ni kutowajibika,vilevile ni uhalifu. 

Uhalifu mtupu

Akiwahutubia waandishi habari, msemaji wa ujumbe huo wa ISAF, Brigadia jenerali Josef Blotz kutoka nchini Ujerumani,amesema hatari hiyo inatokana na kutajwa kwa majina ya baadhi ya Waafghani ambao wanafanya kazi katika idara za ulinzi nchini humo au hata pia kikosi hicho cha ISAF.Blotz ameongeza kuwa yaliyomo kwenye nyaraka hizo ni mambo ambayo sio mapya, na huenda yanajulikana tayari katika miaka ya 2008 na 2009. Ameongeza kuwa huenda ufichuzi huu unapaswa kutajwa kuwa uhalifu.

Rais wa Afghanistan, Hamid Karzai, ameeleza kuwa ameamuru wizara yake ya masuala ya nchi za nje, na washauri wa idara za ulinzi Afghanistan, kuzikagua nyaraka hizo zilizofichuliwa na mtandao huo, hususan zile zinazougusia mchango wa nchi ya Pakistan, pamoja na kujeruhiwa kwa raia.

Afghanistan / Bundeswehr / ISAF
Vikosi vya ISAF katika kambi ya Feysabad,Kunduz-AfghanistanPicha: AP

Uchunguzi kamili

Wakati  huohuo,Waziri  wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates ameamuru uchunguzi wa kina kufanyika ili kubaini aliyeifanikisha hatua ya hati hizo za  siri kuvuja kwenye mtandao wa Wikileaks,ulioyafichua maelezo  ya vita  vya Afghanistan.  

Kwa mujibu wa jenerali aliyestaafu wa jeshi la angani Marekani, ambaye pia alikuwa mkuu wa shirika la upelelezi nchini humo-CIA, Micheal Hayden,ufichuzi wa aina hii unazipa nguvu pande hasimu, na ni lazima viongozi katika mashirika mbalimbali ya upelelezi wakabiliane na tatizo hili na kujitahidi kutafuta suluhu.

Wachambuzi wanaeleza kuwa ufichuzi mkubwa wa nyaraka za wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon uliofanywa na mtandao huo wa wikileaks,  umedhihirisha changamoto za karne ya mtandao, ambapo mkusanyiko wa taarifa nyeti unaweza kufichuliwa kiurahisi.

Mpaka hivi sasa mtandao huo wa Wikileaks haujabaini chanzo cha nyaraka hizo, lakini shaka ipo kwa mchambuzi mpelelezi wa jeshi la Marekani Bradley Manning, ambaye anazuiliwa  katika gereza la jeshi nchini Kuwait.

Wikileaks veröffentlicht Afghanistandokumente Flash-Galerie
Hati za siri:Mtandao wa Wiki-LeaksPicha: picture alliance/dpa

Raia  hatarini

Manning, alikamatwa mnamo mwezi Mei mwaka huu kufuatia ufichuzi wa kanda ya video iliyoonyesha helikopta moja ya Marekani ikifanya shambulio nchini Iraq ambapo raia kadhaa waliuwawa, na ameshtakiwa kwa kutoa taarifa hizo za ulinzi kwa mtu asiyepaswa kupatiwa.Mwezi uliopita Wizara ya Ulinzi ya Marekani,Pentagon ilieleza  kuwa inachunguza kisa hicho, ambapo Manning alitoa kanda hiyo ya video pamoja na nyaraka nyingine, zaidi ya laki mbili unusu, kwa mtandao wa Wikileaks.

Shutuma dhidi ya ufichuzi wa nyaraka hizo za siri, zinazidi kutolewa zikiwemo zile kutoka kwa kikosi cha kuimarisha amani nchini Afghanistan-ISAF, ambapo imesema kuwa huenda ufichuzi huo ukahatarisha maisha ya wananchi.