1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Harakati za kijeshi za Urusi zaongezeka nchini Syria

Admin.WagnerD8 Oktoba 2015

Katibu Mkuu wa mfungamano wa kijeshi wa NATO, Jens Stoltenberg amesema mawaziri wa ulinzi wa mfungamano huo leo watazijadili athari zinazotokana na hatua za kijeshi zinazochukuliwa sasa na Urusi nchini Syria

https://p.dw.com/p/1GkPT
Katibu Mkuu wa jumuiya ya kijeshi ya NATO, Jens Stoltenberg
Katibu Mkuu wa jumuiya ya kijeshi ya NATO, Jens StoltenbergPicha: picture-alliance/AP Photo/V. Mayo

Katibu Mkuu Stoltenberg amesema kuongezeka kwa hatua hizo kunasababisha wasi wasi.

Akihutubia kwenye mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa nchi za jumuiya ya kijeshi ya NATO unaofanyika mjini Brussels, Katibu Mkuu Stoltenberg amesema, ikiwa itabidi, NATO itakuwa tayari kupeleka majeshi ili kuilinda Uturuki ambayo ni mwanachama wa jumuiya ya NATO .

Hapo jana Urusi iliyarusha makombora ya masafa mafupi kutokea manowarini katika hatua ya kwanza ya mapambano ya ardhini kwa kushirikiana na majeshi ya Syria. Urusi ilianza kuchukua hatua za kijeshi nchini Syria wiki iliyopita kwa kufanya mashambulio ya ndege .

Mwishoni mwa wiki iliyopita Uturuki iliripoti kwamba ndege ya Urusi iliingia katika anga yake. Lakini Urusi imejitetea kwa kueleza kwamba ndege yake ya kijeshi iliingia katika anga ya Uturuki kwa makosa.

Juu ya hali ya nchini Syria, Katibu Mkuu wa jumuiya ya kijeshi ya NATO Jens Stoltenberg amesema sasa dunia inashuhudia ongozeko la harakati za kijeshi za Urusi zinazosababisha wasiwasi. Amesema mawaziri wa NATO watayatathmini matukio ya kijeshi ya hivi karibuni na athari zake kwa usalama wa nchi za NATO.

Hapo Jumatatu nchi za NATO zilitoa tamko kuitaka Urusi iache hujuma zake.Katibu Mkuu wa NATO amewaambia waandishi wa habari kwamba makamanda wa NATO leo watatoa taarifa juu ya hali ya nchini Syria na Afghanistan.

Al-Asaad aambiwa aache kuwashambulia wananchi wake

Wakati huo huo Waziri wa ulinzi wa Uingereza Michael Fallon ameitaka Urusi itumie ushawishi wake na kumshinikiza Rais al- Assad ili aache kuwashambulia wananchi wake kwa mabomu. Waziri Fallon amesema mjini Brussels ambako anahudhuria mkutano wa mawaziri wa Nato kwamba Urusi imeufanya mgogoro wa nchini Syria uwe wa hatari kubwa zaidi kutokana na kujiingiza kwake.

Mawaziri wa ulinzi wa nchi za NATO wakutana mjini Brussels
Mawaziri wa ulinzi wa nchi za NATO wakutana mjini BrusselsPicha: picture-alliance/AP Photo/V. Mayo

Waziri huyo wa Uingereza pia amefahamisha kwamba nchi yake itapeleka idadi ndogo ya wanajeshi kwa ajili ya ulinzi wa mipaka ya NATO ili kuukabili uvamizi unaoweza kufanywa na Urusi.

Na Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen amesema Urusi inapaswa itambuea kwamba ikiwa inawashambulia wapinzani wa Assad, itakuwa inawaimarisha magaidi wanaoitwa dola la kiislamu.

Mwandishi:Mtullya Abdu.ape/ rtre

Mhariri:Iddi Ssessanga