1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yataka uwepo zaidi Ulaya Mashariki

Josephat Nyiro Charo28 Agosti 2014

Katibu mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen amesema huku Urusi ikionekana kama tishio la usalama, mkakati wa usalama Ulaya lazima utathiminiwe upya. Anataka kujengwe kambi zaidi za kijeshi mashariki mwa Ulaya.

https://p.dw.com/p/1D3HQ
Anders Fogh Rasmussen 11.08.2014
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya NATO, Anders Fogh RasmussenPicha: Reuters

Katibu mkuu wa jumuiya hiyo, Anders Fogh Rasmussen amesema huku Urusi ikionekana kama tishio la usalama, mkakati wa usalama barani Ulaya lazima utathiminiwe upya. Anataka kujengwe kambi zaidi za kijeshi mashariki mwa Ulaya huku Poland na mataifa ya Balkan yakiwa katika mazungumzo na NATO kuhusu suala hilo.

Kila kitu kinaanza upya: Jumuiya ya Kujihami ya NATO inataka kuupa kipaumbele mkakati wa pamoja wa ulinzi. Wakuu wa serikali wa nchi wanachama za jumuiya hiyo wanakutana wiki ijayo mjini Newport nchini Wales kuujadili mkakati mpya wa NATO. Kufuatia mizozo ya miaka ya 1990 na hatimaye tume za kimataifa ikiwemo nchini Afghanistan, jumuiya ya NATO sasa inakabiliwa na changamoto mpya ambayo si ngeni, nayo ni jinsi ya kukabiliana na Urusi.

Mataifa wanachama wa NATO katika eneo la Balkan kama vile Estonia, Latvia na Lithuania yana wasiwasi pamoja na Poland. Baada ya Urusi kuliteka eneo la Crimea la Ukraine na kusaidia mapambano ya waasi mashariki mwa Ukraine, nchi hizo zinataka zijiandae barabara, iwapo Urusi itaamua kuivamia mojawapo ya wanachama hao wa NATO.

Wasiwasi kuhusu NATO

Egon Ramms, Jenerali wa zamani wa jeshi la Ujerumani Bundeswehr, na kamanda wa zamani wa NATO, alisema, "Inawezakana kabisa bila kazi ngumu kwa Urusi kufanya operesheni za kuziyumbisha Estonia na Latvia, kama inavyofanya sasa nchini Ukraine au kama ilivyofanya Crimea. Natumai na naamini lakini kwamba Urusi itazizuia nchi hizi kupata uanachama wa NATO ili kufaulu kuziyumbisha nchi hizi."

Ukraine Donetsk 28.8.
Shambulizi la mji wa Donetsk Ukraine masharikiPicha: Hermione Gee

Majeshi ya NATO hayawekwi sana nchini Poland na eneo la Balkan, kwa sababu mara kwa mara madai yalisikika kuwa nchi zinazojiunga na NATO zinakuwa katika tabaka la pili katika jumuiya hiyo. Kituo kikubwa cha kijeshi cha NATO kinapatikana katika mji wa Siauliai nchini Lithuania. Madege ya kijeshi ya nchi wanachama wa NATO huanzia safari zao kutoka hapo na kuchukua jukumu la kuilinda anga ya Balkan ambayo haina jeshi la anga inayoilinda. Pia katika mji wa Stettin kaskazini magharibi mwa Poland kuna kikosi cha kimataifa cha wanajeshi 250, ambacho Jenerali Ramms alikiongoza kwa miaka mitatu.

Wanajeshi wa kudumu hawaruhusiwi

Katibu mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen anaiona idadi hiyo kuwa ndogo. Rassmussen ametangaza katika vyombo kadhaa vya habari kwamba anataka kuwe na wanajeshi zaidi mashariki mwa Ulaya, kujenga kambi za kijeshi, kujenga mitambo ya ulinzi dhidi ya makombora na kwa njia hiyo kuhakikisha wanajeshi zaidi wanaweza kupelekwa huko haraka inapohitajika. Hata hivyo kuna makubaliano kati ya NATO na Urusi kwamba NATO haipasi kuweka kikosi cha kudumu mashariki mwa Ulaya. Rasmussen anataka kuendelea kuyaheshimu makubaliano haya, hata kama Urusi imeimarisha sana idadi ya wanajeshi wake katika eneo la mpakani, kama inavyoripotiwa na vyombo kadhaa vya habari.

Kuna njia moja tu ambayo NATO inaweza kuitumia kuhakikisha ina wanajeshi zaidi Ulaya Mashariki na wakati huo huo kuepuka kuvunja mkataba na Urusi. Jenerali Ramms alisema, "Njia moja inayowekezana ni kujenga kambi za mafunzo katika eneo la Balkan na Poland. Kwa njia hii inawezekana kupeleka vikosi vipya kila mara mashariki mwa Ulaya ambavyo vinaweza kuondolewa na kubadilishwa mara kwa mara. Kwa njia hiyo itawezekana kumuonyesha adui kuwa tuna ari ya kuwalinda wanachana wetu wa NATO."

General a.D. Egon Ramms
Jenerali Egon RammsPicha: DW/A. Drechsel

Hatua hiyo ina matokeo ya manufaa kwa kuwa wanajeshi watakaotumwa kwa mzunguko kwa mafunzo Ulaya Mashariki watakuwa kama aina fulani ya jeshi la ulinzi.

Vikosi vya dharura vya NATO

Kamanda huyo wa zamani ameutathimini mkakati mpya wa ulinzi wa jumuiya ya NATO akisema la muhimu ni kuhakikisha kuna uwezekano wa kutuma vikosi kwa haraka. Mpaka sasa jumuiya hiyo inahitaji muda mrefu wa maandalizi kwa ajili ya operesheni kubwa za kijeshi. Mara kwa mara miaka kadhaa huhitajika. Vikosi maalumu vya kukabiliana na matukio ya dharura kama kile cha NATO ambacho kimekuwepo kwa miaka kadhaa sasa, NATO Response Force, NRF, huhitaji wiki kadhaa kuwa tayari kwa mapambano katika harakati ya kijeshi.

Mpango wa Rasmussen ni kwamba anataka kuwe na kikosi maalumu cha wanajeshi ndani ya kikosi cha NRF ambacho kinaweza kutumwa kukabiliana na matukio yoyote ya dharura katika muda wa saa chache. Jenerali Ramms amesema kikosi hicho lazima kiwajumuishe wanajeshi ambao kimsingi wako tayari kwenda vitani kila mara na mikoba yao ya kijeshi wakati wowote. Ramms hauoni mpango wa Rasmussen kama wa kujitakia makuu, bali unaelekea katika mkondo sahihi.

Mwandishi: Josephat Charo/Jansen, Klaus

Mhariri: Mohammed Khelef