1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yaua raia wengine wanane Afghanistan

Josephat Nyiro Charo16 Februari 2010

Wanajeshi wa Marekani wakabiliwa na upinzani mkali Marjah

https://p.dw.com/p/M2c9
Wanajeshi wa Marekani huko MarjahPicha: AP

Kwa mara ya pili katika siku chache zilizopita, vikosi vya kigeni nchini Afghanistan vimewaua kwa bahati mbaya raia watano kwenye shambulio la angani. Mauaji hayo yametokea wakati wanajeshi wa Marekani wanaoongoza operesheni ya jumuiya ya NATO nchini Afghanistan wakikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wapiganaji wa Taliban mjini Marjah.

Kikosi cha kimataifa cha kulinda usalama nchini Afghanistan, ISAF, kimethibitisha kuuwawa raia watano wa Afganistan katika mkoa wa Kandahar kusini mwa nchi hiyo, kwenye harakati ya kijeshi ambayo haihusiani na operesheni kubwa dhidi ya wanamgambo wa Taliban katika mkoa jirani wa Helmand, iliyopewa jina, Operation Moshtarak.

Taarifa ya jeshi la ISAF imefahamisha kuwa vikosi vya ISAF na wanajeshi wa Afghanistan waliwaona watu waliokuwa wakijaribu kutega mabomu wakati walipokuwa wakifanya doria ya pamoja na kuitisha shambulio la angani dhidi ya watu hao wakiwashuku kuwa ni wapiganaji. Watu wengine wawili walijeruhiwa katika shambulio hilo.

"Tumesikitishwa na tukio hili na tunatoa rambirambi zetu kwa familia za waliouwawa na kujeruhiwa," amesema naibu mnadhimu wa kikosi cha ISAF anayehusika na operesheni za pamoja, meja jenerali Michael Regner. Regner ameahidi kufanya uchunguzi kubaini vipi raia hao watano walivyouwawa na kwamba wanajeshi wa NATO watafanya kila linalowezekana kuepusha vifo vya raia wasio na hatia.

Jeshi la Marekani pia limetangaza kwamba raia wengine watatu wa Afghanistan walipigwa risasi na kuuwawa katika matukio matatu tofauti wakati wa operesheni ya Moshtarak siku ya Jumapili na Jumatatu kwa kudhaniwa walikuwa wapiganaji.

Tangazo la mauaji ya bahati mbaya ya raia wa Afghanistan limetolewa siku moja baada ya raia wengine 12 kuuwawa kimakosa na maroketi mawili yaliyovurumishwa na wanajeshi wa NATO dhidi ya wapiganaji wa Taliban lakini yakaanguka kwenye nyumba walimokuwemo watu hao mjini Marjah mkoani Helmand Jumapili iliyopita.

Kamanda wa jeshi la Marekani nchini Afghanistan, jenerali Stanley McCrystal, amesema, "Wakati rais Karzai alipoidhinisha kufanyika operesheni hii, alitupa mwongozo maalum wa kuendelea kuwalinda Waafghanistan. Kwa hiyo operesheni hii imefanywa tukizingatia hilo."

Wanajeshi wa Marekani wanaoongoza mojawapo ya harakati kubwa ya jumuiya ya kujihami ya NATO dhidi ya wanagambo wa kiislamu wa kundi la Taliban wanakabiliwa na upinzani mkali katika baadhi ya maeneo kutokana na kushambuliwa kwa risasi na makombora na mitego iliyowekwa na wapiganaji dhidi yao. Wanajeshi hao wamelazimika kuitisha ndege za kivita na helikopta za kuvurumishia makombora.

Kumekuwa na taarifa za kutatanisha kuhusu ufanisi wa operesheni hiyo ya NATO, lakini inadhihirika wazi dhahiri shahiri kwamba harakati ya kutaka kuyateka maeneo yanayodhibitiwa na kundi la Taliban kabla kuanza kupunguza wanajeshi wa kigeni nchini Afghansitan mwaka 2011 kama ilivyopangwa, huenda ikaendelea kwa wiki kadhaa. NATO imetangaza wanajeshi wake wawili wameuwawa kwenye shambulio la bomu huko Helmand katika harakati isiyohusiana na operesheni dhidi ya Taliban.

Harakati ya Moshtarak ni mtihani mkubwa wa kwanza kwa mpango wa rais wa Marekani Barack Obama kupeleka wanajeshi 30,000 zaidi Afghanistan, ambako wapiganaji wa Taliban wamejiimarisha tangu walipong´olewa madarakani kufuatia uvamizi ulioongozwa na Marekani mnamo mwaka 2001.

Katika taarifa yake kuadhimisha miaka 20 tangu kuondoka vikosi vya muungano wa zamani wa Sovieti kutoka Afghanistan, kundi la Taliban limeonya kwamba wanajeshi wa NATO watakiona kilichomtoa kanga manyoya kama Warusi wakati walipopambana na wapiganaji wa Mujahedeen walioungwa mkono na nchi za magharibi.

Na katika hatua muhimu kwenye vita dhidi ya Taliban, kamanda wa kundi hilo, Mullah Abdul Ghani Brader, amekamatwa katika mji wa bandari wa Karachi kusini mwa Pakistan kwenye harakati iliyofanywa na maafisa wa ujasusi wa Marekani na Pakistan. Marekani imethibitisha kwamba kiongozi huyo, anayeshikilia nafasi ya pili katika uongozi wa Taliban baada ya muasisi wake Mullah Muhammad Omar, alikamatwa siku chache zilizopita. Kundi la Taliban kwa upande wake limekanusha taarifa hiyo likisema kamanda huyo bado yuko Afghanistan akiratibu harakati za kijeshi na kisiasa za kundi hilo.