1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Putin wa Urusi alaani kudunguliwa ndege ya Urusi

Admin.WagnerD25 Novemba 2015

Washirika wa Uturuki katika jumuiya ya kujihami ya NATO wametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka katika kupunguza mvutano unaoelekea kuibuka kati ya Urusi na Uturuki.

https://p.dw.com/p/1HCCl
Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg
Katibu mkuu wa NATO Jens StoltenbergPicha: picture-alliance/dpa/O. Hoslet

Urusi imesema mmoja wa marubani wake wa ndege aliuawa katika tukio hilo huku pia wizara ya ulinzi nchini humo ikisema mwanajeshi mwingine wa Urusi aliuawa wakati helicopter ya uwokozi ya nchi hiyo iliposhambuliwa.

Wakati tukio hilo likianza kuonyesha dalili za kuvurugika mahusiano kati ya mataifa hayo mawili, Uturuki imesema ndege hiyo ya kivita ya Urusi ilikiuka sheria za matumizi ya anga ya Uturuki mara kumi katika kipindi cha dakika tano suala ambalo Urusi imekuwa ikilipinga.

Rais wa Urusi Vladimir Putin amelifananisha tukio hilo la kudunguliwa kwa ndege ya Urusi kama sawa na kuchomwa kisu mgongoni na kusisitiza kuwa ndege hiyo ya Urusi haikuwa na kusudi la kuleta hatari yoyote.

Tukio la kudunguliwa kwa ndege ya Urusi linaashiria kuathiri juhudi za pamoja kutafuta amani katika kujaribu kutatua mgogoro wa Syria ambazo zimekuwa zikichukua kasi katika siku za hivi karibuni kufuatia tukio la mashambulizi ya mjini Parisi Ufaransa yanayodaiwa kufanywa na kundi la dola la kiisilamu ambalo linadhibiti maeneo kadhaa kaskazini mwa Syria.

Obama asema Uturuki inayo haki ya kulinda mipaka yake.

Akizungumzia tukio hilo Rais Barack Obama wa Marekani alisema ya kuwa Uturuki inayohaki ya kuhakikisha kuwa inalinda anga yake na kusema kuwa kipaumbele chake kuhusiana na tukio hilo ni kuhakikisha kuwa anazuia kuibuka kwa mzozo kati ya mataifa hayo mawili.

Rais wa Marekani Barack Obama
Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: picture-alliance/dpa

Ama kwa upande mwingine Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Rais Obama walikubaliana juu ya ya haja ya kujaribu kupunguza mvutano unaoelekea kuibuka kuhusiana na tukio hilo wakati walipozungumza kwa njia ya simu hapo jana.

Katika kauli yake ya awali mara tu baada ya kutokea kwa tukio hilo, Erdogan alisema ya kuwa kila upande unapaswa kuheshimu haki ya Uturuki ya kulinda mipaka yake.

Wakati huohuo katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg alizitaka pande zote .kujaribu kutumia njia za kidipplomasia katika kushughulikia utatuzi wa suala hilo.

Balozi wa Uturuki katika umoja wa mataifa Halit Cevik katika barua yake aliyoandika katika umoja wa mataifa alisema ndege mbili ziliruka katika anga ya Uturuki katika kile alichoelezea kinyume cha utaratibu ambapo moja ilidunguliwa na nyingine ilifanikiwa kuondoka katika anaga hiyo ya Uturuki.

Uturuki na Urusi kwa sasa pia zimekuwa zikivutana kuhusiana na mgogoro wa Syria , wakati Uturuki ikisisitiza kutaka kuondoka madarakani kwa Rais Bashar al Assad wa Syria, anayeungwa mkono na Urusi

Mwandishi: Isaac Gamba/ AFPE

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman

l