1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nawaz Sharif kugombea uchaguzi mkuu Pakistan

P.Martin26 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CTGE

Waziri Mkuu wa zamani Nawaz Sharif amerejea Pakistan,miaka 8 baada ya kupinduliwa na Rais Jemadari Pervez Musharraf.Sawa na Benazir Bhutto, Sharif pia anatazamia kugombea uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanywa tarehe 8 Januari mwakani.

Nawaz Sharif alitua Lahore katika ndege ya Mfalme wa Saudi Arabia Jumapili jioni akisema anataka kusaidia kukomesha utawala wa kidikteta nchini Pakistan.Sharif aliepinduliwa na Jemadari Musharraf miaka minane iliyopita,alijaribu kurejea nyumbani mwezi wa Septemba lakini alirejeshwa Saudia baada ya kutua kwenye uwanja wa ndege.Lakini safari hii ameruhusiwa kubakia Pakistan baada ya Rais Pervez Musharraf aliekwenda Saudia Arabia juma lililopita, kushinikizwa binafsi na Mfalme Abdullah kumruhusu Sharif kurejea nyumbani.Lakini kurejea kwake kumegubikwa na lawama kutoka chama chake cha Muslim League,kwamba maelfu ya wafuasi wa Nawaz Sharif walikamatwa ili kuwazuia kumpokea kwa shangwe.

Lakini polisi na serikali zimekanusha lawama hizo na kusema kuwa ni wachache waliokamatwa na ni kwa sababu ya usalama wa uwanja wa ndege.Hata hivyo,licha ya zaidi ya polisi 5,000 kusambazwa sehemu mbali mbali za mji wa Lahore,maelfu ya wafuasi wa Sharif waliobeba bendera na mabango waliweza kujipenyeza hadi kwenye uwanja wa ndege kumpokea mwanasiasa huyo.

Nawaz Sharif sawa na Benazir Bhutto,anatazamia kugombea uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanywa tarehe 8 Januari.Hata hivyo,haijulikani iwapo vyama vya upinzani vitashiriki kama Rais Musharraf hatoondosha hali ya hatari kati kati ya juma hili.

Hata serikali za nchi za Magharibi zina hofu kuwa utawala wa hali ya hatari wa Rais Musharraf pamoja na hatua za kukandamiza udemokrasia nchini Pakistan,huenda zikawanufaisha wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislamu katika nchi hiyo yenye nguvu za kinyuklia.Musharraf anashinikizwa nyumbani na hata na jumuiya ya kimataifa kuondosha utawala wa hali ya hatari aliyotangaza tarehe 3 Novemba.Musharraf ametumia hali hiyo kuwafukuza majaji wa Mahakama Kuu ambao alihofia kuwa hawatoidhinisha uamuzi wa bunge lililomchagua kuwa rais kwa mara nyingine tena. Baada ya majaji wapya kumuidhinisha kwa awamu nyingine ya miaka mitano,sasa Musharraf anatazamiwa kujiuzulu kama mkuu wa majeshi ili apate kuapishwa kama rais wa kiraia katika kipindi cha siku chache zijazo.

Wachambuzi wa kisiasa nchini Pakistan wanaamini kuwa bado upo uwezekano kwa Musharraf,kama rais kugawana madaraka na waziri mkuu kutoka upande wa upinzani.