1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za Ghuba zakutana kwa dharura

5 Mei 2015

Wafalme wa nchi za Ghuba wanakutana Jumanne (05.05.2015) kwa mkutano utakaohudhuriwa pia na Rais Francois Hollande wa Ufaransa wakati wasiwasi wa jumuiya ya kimataifa ukizidi kuongezeka kuhusiana na vita nchini Yemen.

https://p.dw.com/p/1FKIq
Baraza la Nchi za Ghuba katika mojawapo ya mikutano yake ya kilele mjini Riyadh.
Baraza la Nchi za Ghuba katika mojawapo ya mikutano yake ya kilele mjini Riyadh.Picha: AFP/Getty Images/F. Nureldine

Baraza la Ushirikiano la Ghuba la nchi sita za Kiarabu za Kisunni linakutana Riyadh mji mkuu wa Saudi Arabia wakati eneo lao likikabiliwa pia na tishio la wapiganaji wa jihadi huku kukiwa na wasi wasi wa kufikiwa kwa makubaliano ya mwisho ya nyuklia na Iran.

Nchi hizo zina wasi wasi kwamba taifa la Kishia la Iran yumkini bado likawa na uwezo wa kutengeneza bomu la nyuklia chini ya makubaliano ambayo yatapunguza uwezo wake wa kinyuklia ili iondolewe vikwazo vya kimataifa vyenye kuathiri vibaya uchumi wa nchi hiyo.

Kabla ya Hollande kiongozi mwengine pekee wa kigeni aliyewahi kualikwa katika mkutano wa kilele wa baraza hilo la GCC katika historia yake ya miaka 34 ni Mahmoud Ahmadinajad wakati huo akiwa rais wa Iran mwaka 2007.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry atawasili Riyadh kwa mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo hapo kesho na Alhamisi. Marekani imekuwa ikishinikiza kusitishwa kwa mapigano nchini Yemen kwa misingi ya kibinaadamu ili kuwezesha misaada inayohitajika mno ya chakula, mafuta na mahitaji ya kibinaadamu ifikishwe katika maeneo inakohitajika.

Senegal kutuma vikosi

Katika ishara ya kunatanuka kwa mzozo huo wa Yemen Senegal imetangaza kutuma wanajeshi wake 2,100 nchini Saudi Arabia kujiunga na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kupambana na waasi nchini Yemen.

Wanajeshi wa Senegal wakiwa mazoezini nchini Mali.
Wanajeshi wa Senegal wakiwa mazoezini nchini Mali.Picha: picture-alliance/dpa/Steffen

Waziri wa mambo ya nje Mankeur Ndiaye ametowa tangazo hilo kwa bunge la taifa nchini Senegal ingawa hakuainisha wakati gani vikosi hivyo vitapelekwa.Ndiaye amesema Saudi Arabia ilikuwa imeiomba Senegal kuchangia wanajeshi wake katika muungano huo unaoongozwa na Saudi Arabia mwanzoni mwa mwezi wa Aprili.

Katika mashambulizi ya jana ndege ya mizigo aina ya Ilyushin iliangamizwa wakati ikiwa katika uwanja wa ndege wa Sanaa ambapo mfanyakazi mmoja wa usalama uwanjani hapo akikaririwa akisema kwa kumaka "haya ndio matokeo ya mashambulizi ya kinyama kwa Yemen yeti kipenzi.Na ndege hiyo ya Ilyushin ilikuwa ikitumika kusafrisha bidhaa za chakula kwenye visiwa na majimbo yalioko mbali."

Kushambuliwa kwa uwanja wa ndege

Umoja wa Mataifa hapo jana umeutaka muungano huo unaoendeleza mashambulizi dhidi ya waasi nchini Yemen kuacha kuushambulia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sanaa wakati ikijiandaa kupeleka wafanyakazi wa shughuli za misaada nchini humo kutokea Djibouti na kusambaza misaada nchini kote Yemen.

Watu wakitafuta manusura katika mji wa Saanaa kufuatia mashambulizi ya anga yanayongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen.
Watu wakitafuta manusura katika mji wa Saanaa kufuatia mashambulizi ya anga yanayongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen.Picha: Reuters/K. Abdullah

Chama cha Msalaba Mwekundu pia kimeelezea wasi wasi mkubwa wa kuharibiwa kwa njia za kutungulia ndege katika uwanja huo kutokana na mashambulizi ya anga ya majeshi ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia.

Shirika hilo limesema uwanja wa ndege ni miundo mbinu muhimu na njia kuu ya kufikisha misaada ya kibinaadamu na huduma kwa waathirika wa vita hivyo nchini Yemen.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/Reuters/dpa

Mhariri :Josephat Charo