1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za kigeni zaingilia mgogoro Congo

18 Agosti 2016

Marekani imeonya kutokea kwa ghasia zaidi katika jamhuri ya kidemokrasia ya Congo iwapo rais Joseph Kabila atasalia katika uongozi baada ya kukamilika kwa hatamu yake mnamo mwezi Desemba.

https://p.dw.com/p/1JkGx
Unterzeichnung Friedensabkommen im Kongo
Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila ahudhuria sherehe ya kutia saini mpango wa amani, usalama na ushirikiano wa Congo na mataifa yenye maziwa makuu jijini Addis Ababa.Picha: Reuters

Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo imesema kuwa ghasia zitaendelea kushuhudiwa nchini humo iwapo mataifa ya kigeni yataendelea kuingilia kati masuala ya ndani ya nchi hiyo. Kwa muda wa miezi kadhaa sasa Marekani imekuwa ikifuatilia kwa karibu hali katika Jamhuri hiyo ya Kidemokrasia ya Congo ambapo taharuki inazidi kutanda kabla ya makataa ya tarehe 20 Desemba ya kukamilika kwa kipindi cha pili cha kuhudumu kwa rais wa nchi hiyo Joseph Kabila.

Mnamo mwezi Mei, mahakama ya kikatiba iliamua kuwa Kabila aliyechukuwa uongozi baada ya babake kuuawa mnamo mwaka 2001 kabla ya kuchaguliwa mwaka 2006 na 2011, anaweza kukaimu wadhifa huo iwapo uchaguzi hautaandaliwa kufikia tarehe 19 mwezi Septemba kulingana na katiba inayohitaji kura kuandaliwa siku 90 kabla ya kukamilika kwa kipindi cha kuhudumu kwa rais.

Kongo Beni Menschenmenge nach Massaker
Watu wanalalamika huku mwanamke mmoja akipelekwa hospitalini huko Beni kufuatia mzozo katika eneo hilo.Picha: Getty Images/K.Maliro

Hali nchini Congo

Lakini kulingana na Anthony Gambino aliyekuwa mkuu wa taasisi ya Marekani ya maendeleo ya kimataifa, hali nchini Congo tayari imesambaratika. Aliongeza kuwa kufikia leo imesalia muda wa mwezi mmoja kwa nchi hiyo kuwa na mzozo kamili wa kikatiba .

Rais wa Marekani Barrack Obama pia ameshinikiza kuweko kwa ubadilishanaji mamlaka kwa njia ya kidemokrasia barani Afrika . Mnamo mwaka 2015 katika makao makuu ya Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa alisema,´´Maendeleo ya kidemokrasia nchini Afrika pia yamo hatarini iwapo viongozi watakaa kungatuka mamlakani baada ya kukamilika kwa hatamu zao za uongozi ´´.

Ghasia za hivi punde

Haya yote yanajiri baada ya watu watatu ikiwa ni pamoja na afisa mmoja wa polisi kuuawa hapo jana kwenya makabiliano katika mji mmoja Mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo baada ya ghasia zilizotokana na madai ya kushindwa kwa serikali hiyo kushughulikia maswala ya usalama .

Mamia ya watu pia waliandamana katika barabara za Beni baada ya kukamilika kwa siku tatu za maombolezo zilizoitishwa na makundi ya kijamii kuhusiana na mauaji ya mamia ya watu siku ya Jumamosi usiku. Mauaji hayo yalitokea siku tatu tu baada ya rais Kabila kuzuru eneo hilo na kuahidi kufanya kila awezalo kuhakikisha kudumishwa kwa amani na usalama katika eneo hilo.

Mwandishi: Tatu Karema/afp.

Mhariri: Iddi Ssessanga