1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za magharibi sasa pia zinasisitiza mazungumzo juu ya Libya

Abdu Said Mtullya7 Aprili 2011

Madola ya NATO yasema kila linalopasa litafanywa ili kuwalinda raia nchini Libya

https://p.dw.com/p/10pHa
Waasi wa Libya katika mapigano dhidi ya GaddafiPicha: AP

Libya imeilaumu Uingereza kwa kukishambulia kisima chake cha mafuta wakati ambapo Marekani imeupinga mwito wa Gaddafi kwa Rais Obama juu ya kuacha kuishambulia nchi yake.

Viongozi wa nchi za magharibi sasa pia wanaweka mkazo katika juhudi za kuleta suluhisho kwa njia ya mazungumzo nchini Libya wakati mapigano baina ya wapinzani na majeshi ya serikali yanazidi kuingia katika hali ya kukwama.Hakuna upande unaosonga mbele haraka kwa sasa.

Aliekuwa mbunge wa chama cha Republican Curt Weldon aliwasili Tripoli kwa mwaliko wa Kanali Gaddafi. Lakini amesema lipo jambo moja tu ambalo Gaddafi anapaswa kulifanya nalo ni kung'atuka.

Kwa mujibu wa habari wasi wasi umezidi kuwa mkubwa juu ya hali ya raia waliozingirwa katika mji wa Misrata.Jumuiya ya kijeshi ya Nato, inayoongoza operesheni za kijeshi ili kulitekeleza azimio la Umoja wa Mataifa juu ya kuwalinda raia imesema kuwa sasa ni hatari kuyashambulia kwa ndege,majeshi ya Gaddafi kwa sababu yanawatumia raia kama ngao.

Hata hivyo NATO imesema kuwa itafanya kila linalowezekana ili kuwalinda raia katika mji wa Misrata ambako Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema kuwa hali ni mbaya sana.

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Libya Khaled Kaim amesema kwenye mkutano na waandishi habari mjini Tripoli,kwamba ndege za Uingereza zimekishambulia kisima cha mafuta- cha Al - Sarir-kilichopo kusini mashariki mwa Libya ambacho ni kikubwa kuliko vingine vyote nchini humo. Katika shambulio la ndege hizo za Uingereza walinzi watatu wa Libya waliuawa.Naibu waziri huyo Khaled Kaim amesema bomba linalokiunganisha kisima hicho na Tobruk limeharibiwa.

Lakini hakuna taarifa kutoka wizara ya ulinzi ya Uingereza wala kutoka Nato inayoziongoza operesheni za kijeshi dhidi ya Gaddafi.Hata hivyo waasi wamesema kwamba ni majeshi ya Gaddafi yaliyofanya shambulio hilo.

Wakati huo huo, huku wapinzani wakijaribu kuziteka tena sehemu zilizotekwa hapo awali na majeshi ya Gaddafi, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton ameukataa mwito wa Gaddafi aliouwasilisha kwa Rais Obama juu ya kusimamishwa mashambulio yanayofanywa na madola ya Nato dhidi ya Libya.Waziri Clinton badala yake ameeleza kuwa Gaddafi ndiye anaepaswa kusimamisha mashambulio ya majeshi yake.Clinton amesema Gaddafi anapaswa kuyaondoa majeshi yake na aondoke Libya.

Habari zaidi zinasema kuwa aliekuwa waziri wa nishati wa Libya Omar Fathi Bin Shatwan ameruka kambi ya Gaddafi na kukimbilia Malta. Msemaji wa serikali ya Malta amezithibitisha habari hizo leo.

Mwandishi/Jürgen Stryak/Mtullya Abdu/

ZAR/AFP/CNN/

Mhariri/ Yusuf Saumu Ramadhani