1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za Magharibi zahitaji wahamiaji

H.Jeppesen/P.Martin22 Februari 2008

Ripoti ya Shirika la Ushirikiano wa Uchumi na Maendeleo-OECD inaeleza kinagaubaga kwamba uhamiaji si kitisho bali hufungua milango mingi kwa nchi za Magharibi.

https://p.dw.com/p/DBW4

Ripoti iliyotolewa na OECD katikati ya juma hili,inasema suala la kuwajumuisha wahamiaji linapaswa kupewa kipaumbele.Katibu Mkuu wa shirika hilo,Angel Gurria katika ripoti yake ameeleza muundo wa uhamiaji katika nchi zilizoendelea kiviwanda na kuna mengi yanayofaa kuzingatiwa.

Ukweli wa kwanza ni kwamba nchi za Magharibi zilizoendelea kiviwanda zinahitaji wahamiaji kwani katika nchi hizo idadi ya watu walio wazee inaongezeka : na wahamiaji hawatosaidia tu kuhifadhi utulivu wa kiuchumi bali watahitajiwa vile vile kukuza uchumi huo.Kwa hivyo nchi nyingi hujaribu kuwavutia kwa njia mbali mbali wahamiaji wenye elimu ya tabaka ya juu.

Ukweli wa pili ni kwamba katika nchi 30 wanachama wa OECD,wahamiaji siku hizi wana elimu bora zaidi kuliko wenyeji.Takriban katika nchi zote za OECD kila mgeni wa nne anaehamia nchi hizo ana elimu bora zaidi.Kwa wenyeji kila mtu wa tano ndio alie na elimu ya tabaka ya juu.

Ukweli wa tatu ni kwamba baadhi kubwa ya wahamiaji mara nyingi hufanya kazi zilizo chini ya elimu yao.Kwa mfano nchini Ujerumani yawezekana kuwa kila mhamiaji wa pili anaeendesha taxi ana elimu bora kuliko ya huyo anaeendeshwa.Hata hivyo kuna malalamiko ya kibaguzi kuwa wageni huwanyanganya Wajerumani nafasi za ajira.

Chuki za aina hiyo hutumiwa kwa propaganda za vyama vyenye itikadi kali za mrengo wa kulia na makundi mengine kuchochea chuki dhidi ya wageni.Mbali na hayo,ni upumbavu ikiwa elimu na ujuzi wa wahamiaji hautotumiwa.

Ukweli wa nne ni kwamba inawezekana kuwajumuisha wahamiaji katika jamii.Ripoti ya OECD imetoa mifano mbali mbali ya kuanzisha utaratibu huo kama vile nchini Ujerumani ambako watoto hufanyiwa mitihani ya lugha ya Kijerumani mwaka mmoja kabla ya kuanza shule.Kwa njia hiyo wale walio dhaifu katika lugha ya Kijerumani husaidiwa hata kabla ya kuanza shule.

Kutokana na hali hizo nne zilizotajwa katika ripoti ya OECD,ni dhahiri kuwa serikali za nchi wanachama wa shirika hilo hazikutekeleza wajibu wake.Hata ikiwa serikali za Umoja wa Ulaya zitaendelea kujadiliana vipi zifunge mipaka yake,badala ya kujadiliana vipi wahamiaji wanaweza kujumuishwa bora zaidi katika jamii,basi serikali hizo zimetambua ukweli wa kwanza yaani nchi za magharaibi zinahitaji wahamiaji.