1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege ya AirAsia yatoweka na watu 162

28 Desemba 2014

Ndege ya shirika la ndege ya AirAsia ikiwa na watu 162 imetoweka Jumapili (28.12.2014) ikiwa safarini kutoka Indonesia kuelekea Singapore kwa safari ya masaa mawili.Shughuli za kuitafuta zaahirishwa hadi Jumatatu.

https://p.dw.com/p/1EAqu
Ndege ya shirika la ndege la AirAsia aina ya Airbus A320-200 ikijitayarisha kutua katika uwanja wa ndege wa Sukarno-Hatta huko Tangerang kwenye viunga vya Jakarta mwaka 2013.
Ndege ya shirika la ndege la AirAsia aina ya Airbus A320-200 ikijitayarisha kutua katika uwanja wa ndege wa Sukarno-Hatta huko Tangerang kwenye viunga vya Jakarta mwaka 2013.Picha: Reuters/E. Nuraheni

Hiyo ni ajali ya tatu mwaka huu kuzikumba ndege za Malaysia. Wafanyakazi wa kituo cha kungoza safari za ndege katika uwanja wa ndege walipoteza mawasiliano na ndege hiyo aina ya Airbus A320-200 kama saa moja baada ya ndege hiyo kuruka kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Juanda ulioko kwenye mji wa Surabaya mashariki mwa Java ikiwa ni sasa kumi na moja na dakika ishirini alfajiri saa za Indonesia.Shughuli za kuitafuta katika bahari ya Java zimeahirishwa hadi kesho.

Ndege hiyo ilikuwa ikitarajiwa kuwasili Singapore saa mbili na nusu asubuhi. Muda mfupi kabla ya kutoweka kwake ndege hiyo iliomba ruhusa kutoka kituo cha udhibiti wa safari za ndege cha Jakarta kubadili mkondo wake wa safari na kuruka juu zaidi kutokana na hali mbaya ya hewa katika eneo ambalo linajulikana kwa kutokea dhoruba za kila mara.

Shirika la ndege la Air Asia limesema katika taarifa kwenye mtandao wake wa Facebook kwamba marubani waliomba kubadili mkondo wa safari kutokana na hali mbaya ya hewa kabla ya mawasiliano na ndege hiyo kupotea wakati bado ikiwa chini ya maelekezo ya kituo cha Udhibiti wa Safari za Anga cha Indonesia.

Abiria waliokuwemo ndani

Abiria 156 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo nambari QZ8501 walikuwa ni raia wa Indonesia -- raia watatu wa Korea Kusini na mtu mmoja kutoka kila nchi Singapore, Malaysia na Ufaransa. Kulikuwa na watu wazima 138, watoto 16 na mtoto mchanga mmoja mbali na wahudumu wa ndege watano, rubani mmoja na msaidizi wake ambaye inaaminika kuwa ni Mfaransa.

Bao la matangazo ya safari za ndege katika uwanja wa ndege wa Changi Singapore. (28.12.2014)
Bao la matangazo ya safari za ndege katika uwanja wa ndege wa Changi Singapore. (28.12.2014)Picha: Reuters/E. Su

Kikosi cha anga cha Indonesia kimesema ndege zake mbili zimetumwa kulipekuwa eneo la bahari ya Java kusini magharibi ya Pangkalan Bun katika jimbo la Kalimantan kama nusu njia kwenye njia iliotegemewa ndege hiyo kupita.

Msemaji wa kikosi hicho Hadi Cahyanto amesema hali ya hewa ilikuwa ya mawingu na eneo hilo limezungukwa na bahari na kwamba bado wako njiani kuelekea huko kwa hiyo hawawezi kuzungumzia dhana juu ya kile kilichoisibu ndege hiyo. Ndege ya kijeshi ya uchukuzi ya Singapore chapa C-130 pia imepelekwa kwenye eno hilo baada ya Indonesia kukubali msaada kutoka jirani yake huyo wa Kusini mashariki mwa Asia.

Wasi wasi waongezeka

Ndege hiyo ya injini mbili inasimamiwa na tawi la Indonesia la shirika la ndege la AirAsia lenye makao yake makuu nchini Malaysia ambalo linahodhi soko la safari za ndege la gharama za chini linalokuwa kusaini mashariki ya Asia.

Ndugu wa abiria wa ndege iliotoweka wakiwa katika uwanja wa Surabaya Indonesia.
Ndugu wa abiria wa ndege iliotoweka wakiwa katika uwanja wa Surabaya Indonesia. (28.12.2014)Picha: picture-alliance/dpa/Handoko

Kiongozi mwenyenye wa shirika hilo la AirAsia Tony Fernandes ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa zamani wa sekta hiyo aliyeanza kuliongoza shirika hilo hapo mwaka 2001 amesema yuko njiani kuelekea Surabaya ambapo ndiko walikotoka abiria wengi wa ndege hiyo iliyotoweka.

Ameongeza kusema kwenye mtandao wake wa Twitter kwamba mawazo yake yote yako kwa abiria na wafanyakazi wa ndege hiyo. Kutokana na kuwepo kwa taarifa chache kuhusu kadhia hiyo ndugu wa abiria waliojaa hofu wamekusanyika katika uwanja wa ndege wa Changi nchini Singapore.

Huko Surabaya mamia ya Waindonesia wamejaa kwenye sebule ya safari za ndege uwanjani wakitaraji kupatiwa habari kuhusu ndege hiyo iliotoweka. Nchi ya Indonesia ambayo ni mjumuiko wa visiwa vingi kutokana na kwamba miundo mbinu yake ya safari za ardhini kuwa mibaya imekuwa ikishuhudia kuongezeka kwa haraka sana safari za ndege za bei nafuu katika miaka ya hivi karibuni.

Lakini shughuli hizo za safari za anga zimekuwa zikikabiliwa na viwango vibaya vya usalama katika ene ambalo pia lina uzoefu wa hali mbaya ya hewa. Shrika la AirAsia limesema ndege yake iliotoweka ilikuwa imefanyiwa matengenezo mapya hapo Novemba 16 na kampuni yake hiyo haikuwahi kamwe kupata ajali iliosababisha maafa.

Hali mbaya ya hewa

Afisa kutoka wizara ya uchukuzi ya Indonesia amesema rubani aliomba kuruka juu zaidi kwa mita 6,000 hadi kufikia mita 38,000 ili kuepuka mawingu mazito. Djoko Murjatmodjo ameuambia mkutano wa waandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa Jakarta kwamba ndege hiyo ilikuwa katika hali nzuri lakini hali ya hewa ilikuwa sio nzuri.

Afisa wa shirika la taifa la uokozi la Indonesia huko Medan kaskazini ya Sumatra akionyesha mahala ilipotoweka ndege hiyo ya AirAsia. (28.12.2014)
Afisa wa shirika la taifa la uokozi la Indonesia huko Medan kaskazini ya Sumatra akionyesha mahala ilipotoweka ndege hiyo ya AirAsia. (28.12.2014)Picha: Aditya/AFP/Getty Images

Inaelezwa kwamba kuruka juu kukwepa mawingu makubwa ya mvua ni utaratibu wa kawaida kuchukuliwa na ndege katika eneo kunapokuwepo hali ya aina hiyo. Kwa mujibu wa Dudi Sudibyo mchambuzi wa masuala ya anga aliyeko Indonesia " Hakuna kosa kufanya hivyo. Kile kinachotokea baada ya hapo ndicho kinachopaswa kuekewa alama ya kuuliza." Kutoweka kwa ndege hiyo kumekuja mwishoni mwa mwaka wa balaa kwa shughuli za usafiri wa anga wa Malaysia.

Ndege ya shirika la ndege la Malaysia safari MH370 ikiwa na abiria 239 ilitoweka mwezi wa Machi baada ya kubadili njia yake ya safari bila ya kufafanuliwa sababu za kutoka mkondo wake wa Kuala Lumpur kwenda Beijing.

Ndege nyengine ya shirika hilo la Malaysia ilianguka hapo mwezi wa Julai kwenye eneo la uasi mashariki mwa Ukraine na kuuwa watu wote 298 waliokuwemo ndani ambapo iliaminika kwamba ilidunguliwa na kombora kutoka ardhini.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/dpa

Mhariri: Bruce Amani