1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege za Assad zaendelea kufanya uharibifu Syria

Admin.WagnerD24 Septemba 2012

Ndege za jeshi la Syria siku ya Jumatatu ziliendelea kuyashambulia maeneo ya waasi licha ya madai kuwa hivi sasa waasi hao wanadhibiti sehemu kubwa zaidi ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/16DFO
Ndege ya serikali ikiangusha bomu mjini Aleppo.
Ndege ya serikali ikiangusha bomu mjini Aleppo.Picha: dapd

Mashambulizi hayo pia yamefanyika wakati mpatanishi wa mgogoro wa Syria, Lakhdar Brahimi anajiandaa kulitaarifu Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa juu ya mazungumzo aliyoyafanya na rais Bashar al-Assad, kabla ya kuanza kwa mkutano mkuu wa baraza la Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne.

Brahimi alizungumzia suala la Syria na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ban Ki-moon siku ya Jumamosi, na wawili hao walikubaliana kuwa mgogoro huo uliyodumu kwa miezi 18 sasa ulikuwa unazidi kuwa tishio kwa amani na usalama wa kanda ya mashariki ya kati.

Mwanamke aliyejeruhiwa katika mashambulizi akitoka katika hospitali ya Dar El Shifa mjini Aleppo.
Mwanamke aliyejeruhiwa katika mashambulizi akitoka katika hospitali ya Dar El Shifa mjini Aleppo.Picha: dapd

Lakini Brahimi ameahidi kuendelea kufanya juhudi hadi pale atakapoona kuwa hawezi tena. "Sintoendelea siku moja zaidi pale ntakapogundua kuwa siwezi kuendelea zaidi. Lakini maadamu kuna matumaini yoyote kwamba tunaweza kusaidia kwa namna yoyote ile tutaendelea," alisema Brahimi.

Watu wazidi kuuawa

Kikao cha Jumatatu kinafanyika siku moja baada ya kuuawa kwa watu wasiyopungua 82 nchini Syria kote, 40 kati yao wakiwa ni raia, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na shirika la uangalizi wa haki za binaadamu la Syria - Observatory - lenye makao yake mjini London. Mkurugenzi wa shirika hilo, Rami Abdul Rahman amesema watoto watatu wa familia moja walikuwa miongoni mwa watu watano waliyouawa wakati ndege za serikali zilipoishambulia wilaya ya Maadi iliyoko katika mji wa zamani wa Aleppo asubuhi ya leo.

Mjini Damascus, mapigano yaliendelea usiku wa kuamkia leo katika eneo la Qaboon, wakati miripuko mikubwa ilitikisa maeneo ya Qudsaya, Douma na Harasata. Siku ya Jumapili ndege za serikali zilishambulia ngome za waasi wakati waasi hao wakisema hivi sasa wanadhibiti sehemu kubwa zaidi ya Syria na kutangaza kuhamisha uongozi wao kutoka nchini Uturuki kwenda maeneo yaliyokombolewa ndani ya Syria. Kanali Ahmad Abdul Wahab wa Jeshi Huru la Syria, alisema hivi sasa mashambulizi ya angani ndiyo yanayowazuia kuuteka mji mkuu wa Damascus. Siku ya Jumamosi FSA ilisema hatua inayofuata sasa ni kuuteka mji wa Damascus.

Mlenga shabaha wa Jeshi Huru la Syria, akitafuta shabaha katika eneo la Bustan Al-Basha, kusini mashariki mwa Aleppo.
Mlenga shabaha wa Jeshi Huru la Syria, akitafuta shabaha katika eneo la Bustan Al-Basha, kusini mashariki mwa Aleppo.Picha: Reuters

Assad azidi kupoteza udhibiti

Shirika hilo la kuangalia haki za binaadamu maarufu kama Observatory, limesema kuwa karibu asilimia 80 ya vijiji na miji katika mpaka wa Syria na Uturuki viko nje ya mamlaka ya serikali ya Assad. Mjini Damascus, vyama vya upinzani 20 vinavyotambuliwa na serikali vilikutana siku ya Jumapili kujadili suluhu ya mgogoro huo katika mkutano uliyohudhuriwa na mabalozi wa Urusi na Iran. Raja al-Nasser kutoka kamati ya taifa ya uratibu wa mabadiliko ya kidemokrasia, alitaka kukomesha mashambulizi ya ukatili ili kupisha mchakato utakaohitimisha utawala wa sasa.

Kwa mujibu wa shirika hilo la Observatory, watu wasiyopungua 29,000 wameuawa tangu kuanza kwa uasi dhidi ya utawala wa rais Assad Machi mwaka 2011. Kutokana na mgawanyiko wa jumuiya ya kimataifa kuhusiana na mgogoro huo, Umoja wa Mataifa hautakuwa na kikao rasmi kuijadili Syria wakati wa mkutano mkuu wiki hii. Lakini rais Brack Obama na viongozi wengine wa nchi za magharibi wanatarajiwa kutoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua katika hotuba zao.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe
Mhariri: Saum Yusufu Ramadhan