1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege za Israel zaendelea kushambulia Ukanda wa Gaza

29 Februari 2008
https://p.dw.com/p/DFf9

GAZA:

Wapalestina 20 wameuawa kwenye Ukanda wa Gaza siku ya Alkhamisi katika mashambulizi ya ndege za kijeshi za Israel.Kwa mujibu wa maafisa wa hospitali, miongoni mwa wale waliouawa ni mtoto mchanga na watoto wanne wa kiume waliokuwa wakicheza mpira uwanjani.Licha ya jumuiya ya kimataifa kutoa mito ya kuwa na uvumilivu,sasa idadi ya watu waliouawa katika kipindi cha siku mbili zilizopita imefikia 33.Miongoni mwa hao 33,mmoja ni raia wa Israel alieuawa siku ya Jumatano katika shambulizi la roketi la wanamgambo wa Hamas.

Israel inasema,vikosi vyake vya anga vinajibu mashambulizi ya roketi zaidi ya 100, kutoka Gaza na kulenga kusini mwa Israel.Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert amesema,mashambulizi hayo ni sehemu ya vita vinavyoendelea dhidi ya wanamgambo wa Hamas.

Wakati huo huo msemaji wa Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas ameituhumu Israel kuwa inajaribu kuvuruga utaratibu mpya wa amani unaoungwa mkono na Marekani,kabla ya ziara ya juma lijalo ya waziri wa nje wa Marekani Condoleezza Rice katika Mashariki ya Kati.