1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndoa za Utotoni bado tatizo barani Afrika

12 Juni 2015

Tatizo la ndoa za utotoni linanaonekana kuyakabili mataifa mengi ya Afrika, huku ikielezwa kuwa hali ni mbaya zaidi nchini Cameroon ambako wazazi wanatumia kama mkakati wa kuzalisha kipato.

https://p.dw.com/p/1FgP3
Bildergalerie Grün in Afrika
Picha: AFP/Getty Images

Bienvienue Taguieke mwenye umri wa miaka 12 alitarajiwa kutii wazazi wake na kuolewa na mwanamume anayemzidi umri kwa miaka 40, lakini hatua ya chama cha wanawake katika Mkoa wa Kaskazini mwa Cameroon ambako ndoa za utotoni zimeenea, kuzuia hali hiyo ni ishara kuwa wanawake wameanza kupiga kelele kupinga vitendo hivyo.

"Nilikuwa mwanafunzi katika shule ya serikali Guidimdaz, kijiji kilicho katika eneo la Mokolo Mkoa wa Kaskazini ambako mwanamume alitowa Faranga 5,000 ambayo ni karibu (dola 8.50) kwa mama yangu ili anishawishi niolewe. Nilikataa na kuwaambia baadhi ya watu akiwemo mkuu wangu wa shule, "Bienvienue, ambaye sasa ana umri wa miaka 15, aliliambia shirika la habari la IPS.

Bienvienue anaamini kuwa mama yake alikuwa anataka kushawishika kwa sababu za kiuchumi." Nafikiri mama yangu alikuwa anataka kuniuza kwa sababu ya umaskini. Baba yangu alifariki na kulikuwa hakuna mtu wa kulipa ada ya shule na kututunza, alisema.

Hata hivyo, Mkuu wa shule Asta Djarmi alimuomba mama yake Bienvienue kutomwozesha binti yake kwa mwanamume mzee. "Mkuu wa shule alisimamisha mpango wa ndoa ulioanzishwa na mama yangu, basi watu wa kundi la kampeni la kiraia linalopinga ndoa za utotoni ALDEPA, waliingilia kati na kulipa mahari ya faranga 5,000 kwa mwanamume. Pia wanalipa ada yangu ya shule."

Binti huyo mwenye umri wa miaka 15 anasema ana ndoto ya kuwa mwalimu, na kwamba kufunga ndoa akiwa mtoto ingekuwa mwisho wa ndoto hiyo. Kwa kuwa sasa hakufanya hivyo ana lengo la kuifufua ndoto yake.

Afrika Weizen Mädchen Ernte
Picha: picture alliance / Gavin Hellier/Robert Harding

Tukio hilo sio la kipekee kupingwa katika mkoa huo. Mkoa wa Kaskazini, wasichana wenye umri mdogo wanapinga kile wanachokiona kuwa ni utamaduni wa kuumiza. Katika kijiji jirani Zilling, kwa mfano, Nabila mwenye umri wa miaka 15 amefanikiwa kukimbia kutoka nyumbani alikoolewa.

"Nililazimishwa na wazazi wangu kuingia katika ndoa na mwanamume mzee miaka miwlii iliyopita nilipokuwa na miaka 13 tu. Niliondoka nyumbani kwa mwanamume huyo baada ya siku 14 za maumivu. "msichana alikumbuka.

Lakini siku hizo 14 aliachwa na ujauzito, na sasa analea mtoto mwenyewe. Suala la kushangaza, ni kwamba mwanamume aliyelazimishwa kumuoa sasa kafungua kesi mahakamani dhidi yake, na kudai kuwa Nabila arudi nyumbani kwake alikoolewa.

Simbabwe Cholera Epidemie
Picha: picture-alliance/dpa

Kundi la kampeni la kiraia linalopinga ndoa za utotoni ALDEPA, sasa linatoa msaada wa kisheria kwa akina mama wenye umri mdogo, na afisa mwandamizi wa shirika hilo, Henri Adjini, aliliambia shirika la habari la IPS kuwa hivi sasa wanalipa ada ya shule kwa wasichana 87 waliookolewa kutoka ndoa za utotoni.

Adjini alisema kuwa ndoa za kulazimishwa ni sehemu ya utamaduni wa ndani wa makabila ya Mafa na Kapsiki, akielezea kuwa wazazi kuwaoza binti zao kwa kupata malipo mahari katika mfumo wa fedha, mifugo au mali.

Kuoza mabinti ni mkakati wa kuzalisha kipato nchini Cameroon, ambapo karibu theluthi moja ya nchi hiyo yenye watu milioni 22 ni maskini, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa Hazina ya Umoja wa Mataifa kuhusu Idadi ya Watu (UNFPA), kuna uhusiano kati ya ndoa za utotoni na umaskini katika nchini za Afrika ya Kati, huku asilimia 71 ya watoto wanaoolewa wanatoka katika kaya maskini. Takwimu kutoka Shirika la kuwahudumia watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) kwa mwaka 2014 zinaonyesha kuwa asilimia 31 ya wasichana wenye umri mdogo katika Mkoa wa Kaskazini wamekumbwa na ndoa za utotoni.

Waziri wa familia na Uwezeshaji Wanawake wa Cameroon, Marie Therese Abena Ondoa alikemea hadharani suala la ndoa, akisema kuwauza wasichana kama bidhaa ni kinyume cha maadili.

Ndoa za utotoni sio suala geni nchini Cameroon, hata hivyo. Nchi nyingi katika kanda na duniani zinakabiliwa na tatizo hilo, au hata zaidi.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2013 ya UNFPA, wasichana wawili kati ya watano walio na umri chini ya miaka 18 waliolewa Afrika Magharibi na Afrika ya kati, hali ikiwa ni mbaya zaidi Niger ambako asilimia 75 ya watoto waliolewa kikiwa kiwango cha juu zaidi duniani ikifuatiwa na Chad asilimia 72 na Guinea asilimia 63.

Mhandishi:Salma Mkalibala/IPS

Mhariri:Josephat Charo