1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu ajitahidi kuuokoa muungano unaoongoza

16 Novemba 2018

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amefuta ziara yake ya Austria kufuatia kujiuzulu kwa Waziri wa Ulinzi Avigdor Lieberman. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje amethibitisha hayo leo.

https://p.dw.com/p/38OxL
Israel Lieberman und Netanjahu
Picha: picture-alliance/AP Photo/T. Abayov

Kujiuzulu kwa Lieberman Jumatano wiki hii , kulijiri kufuatia makubaliano ya  kusitishwa kwa mapigano na chama Hamas mjini Gaza, ambako alikuita kuwa  ni ‘‘ Kusalimu amri mbele ya  ugaidi´´. Waziri huyo Aliilaumu serikali ya Netanyahu kwa udhaifu katika shughuli zake na Wapalestina. Makubaliano ya kusitishwa mapigano yaliafikiwa baada ya siku mbili za mapigano mpakani kati ya Israel na Hamas ambayo yalisababishwa na shambulio la Israel l mjini Gaza.

Lieberman mwenye umri wa miaka 60, aliyekuwa  awali Waziri Mkuu wa Masuala ya Nje na kiongozi wa chama cha Yisrael Beiteinu, amekuwa Waziri wa Ulinzi wa Israel tangu mwezi Mei mwaka 2016. Ni mtu anayekabiliwa  na utata katika siasa za Israel kutokana na matamshi yake ya kejeli dhidi ya mataifa ya kiarabu. Serikali ya mrengo wa kulia ya Netanyahu inategemea uungaji mkono wa wabunge watano wa chama cha Yisrael Beiteinu katika Bunge  Knesset. Serikali ina viti  viti 61 kati ya viti 120 vya bunge hilo.

Avigdor Lieberman
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Avigdor LiebermanPicha: Reuters/A. Awad

Hatua ya Lieberman kujiuzulu aidha imekifanya mrengo wa Netanyahu unaoongoza kusalia na kiti kimoja zaidi kwa wingi, suala linaloongeza uwezekano wa kufanyika kwa uhaguzi wa mapema. Leo, Netanyahu amekutana na kiongozi wa chama cha Kiyahudi Naftali Bennet, ambaye ametishia kuiangusha serikali iwapo hatachaguliwa kuwa Waziri wa Ulinzi kumrithi Lieberman.

Katika hotuba aliyotoa jana Alhamisi, Bennett ambaye pia ni Waziri wa Elimu, hakuzungumzia tishio la kujiuzulu lakini akatoa sababu za kwa nini anafaa kuteuliwa waziri wa ulinzi. ´´Kitu kibaya zaidi ni kwa serikali ya Israel kufikiri kuwa hakuna suluhisho kwa tatizo la ugaidi, magaidi, makombora, hakuna la kufanya na si rahisi kushinda. Lakini kuna kitu kinachoweza kufanywa. Kuna suluhuhisho. Israel inapotaka kushinda, tutashinda. Nilikutana na Waziri Mkuu na kumshauri aniteue Waziri wa Ulinzi nikiwa na lengo moja tu, kwamba Israel ishinde tena,´´ alisema Bennett.

Israel Lieberman und Netanjahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu (kulia) akizungumza na Waziri wa Ulinzi Avigdor Lieberman (kushoto)Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Sultan

Waziri wa Fedha wa Israel Moshe Kahlon, ambaye chama chake cha mrengo wa kulia cha Kulanu kina viti kumi katika Bunge la Israel, anadaiwa kumueleza Netanyahu kwamba uchaguzi wa mapema ni muhimu ili kuwa na serikali imara itakayosaidia kuboresha uchumi wa nchi.

Kumekuwepo na  uvumi kwa muda mrefu kwamba Netanyahu huenda akaitisha uchaguzi mkuu kabla ya tarehe iliyopangiwa ya mwezi Novemba mwaka ujao wa 2019.Mamia ya watu waliandamana jana jioni mjini  Tel Aviv kutaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya Hamas ambayo imeshiria kwamba kusitishwa mapigano, na kujiuzulu kwa Lieberman ni ushindi.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/DPAE/APE/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman