1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu akabiliwa na hali ngumu

Lilian Mtono
18 Septemba 2019

Ripoti za matokeo ya awali ya uchaguzi mkuu nchini Israel zinaonyesha waziri mkuu  Benjamin Netanyahu ameendelea kukabana koo na mpinzani wake mkubwa Benny Grantz.

https://p.dw.com/p/3Pm16
Wahlen in Israel- Benjamin Netanyahu
Picha: Getty Images/AFP/M. Kahana

Vyombo mbalimbali vya habari vya Israel vimeripoti kwamba chama cha Netanyahu cha mrengo wa kulia cha Likud na kile cha Bluu na Nyeupe cha mpinzani wake Grantz kila kimoja kimepata viti 32 kati ya viti 120 vya bunge baada ya takriban asilimia 90 ya kura kuhesabiwa.

Ripoti hizo zilinukuu duru kutoka tume ya uchaguzi kwani kiwango hicho cha matokeo kilikuwa hakijachapishwa rasmi na hakikutarajiwa kabla ya leo alasiri.

Matokeo ya awali katika uchaguzi wa Israel kwa kawaida huwa si ya uhakika na huku matokeo rasmi yakitarajiwa kutolewa Jumatano, huenda bado Netanyahu akapata ushindi, ingawa vituo vyote vitatu vimeonyesha matokeo sawa.

Kwa matokeo hayo, pande zote zitatakiwa kuunda serikali itakayojumuisha vyama vingine bungeni hali inayoibua uwezekano wa mazungumzo kuelekea kuundwa kwa serikai ya umoja.

Bildkombo:  Benny Gantz, Avigdor Lieberman und Benjamin Netanyahu
Wagombea watatu wnaoshikana mashati kwenye uchaguzi wa Israel. Kutoka kushoto Beny Gantz, Avigdor Lieberman na Benjamin Netanyahu.Picha: Reuters/R. Zvulun

Iwapo matokeo haya ya awali yatabakia hivyo hadi mwisho, itakuwa ni pigo kubwa kwa Netanyahu, aliyekuwa na matarajio ya kuunda serikali ya muungano wa vyama vya mrengo wa kulia, sawasawa na ule uliopo sasa, huku pia akikabiliwa na uwezekano wa kufunguliwa mashitaka ya ufisadi wiki chache zijazo.

Kwenye mkutano na wafuasi wa chama chake baada ya uchaguzi mjini Tel Aviv jana usiku Netanyahu aliashiria kwamba tayari amejiandaa kwa makubaliano magumu ya kuunda serikali ijayo ya muungano ya Israel, huku akisisitiza umuhimu wa Israel kuwa na serikali imara itakayoutetea kwa nguvu zote Uyahudi.

Amesema, bado anasubiri matokeo rasmi, lakini akisisitiza kwamba Israel iko njia panda kihistoria lakini pia ikiwa na fursa pana pamoja na changamoto kubwa katika siku za usoni, huku akigusia alivyoviita ''vitisho halisi'' kutoka kwa Iran na washirika wake, "Siku chache zijazo mpango wa karne utawasilishwa kwa rafiki yangu wa karibu rais Trump na makubaliano yatakayofuata yatatengeneza mustakabali wa taifa letu kwa ajili ya kizazi kijacho. Kwa wakati huu, Israel inahitaji serikali thabiti, imara na ya Kiyahudi ili kufikia malengo hayo." 

Wahlen in Israel- Anhänger der Blau Weißen Partei
Wafuasi wa chama cha Bluu na Nyeupe cha Beny GantzPicha: Getty Images/AFP/G. Tibbon

Dalili zote zinaonyesha kuwa hakuna anayeweza kupata idadi kubwa ya wabunge kati ya Netanyahu na Gantz bila uungaji mkono wa Avigdor Lieberman aliyekuwa waziri wa ulinzi wa Netanyahu. Lieberman ameibuka kama mshindi wa kweli, kwani kuna uwezekano mkubwa kwamba ndiye atakayeamua juu ya atakayejumuishwa katika serikali ijayo. Chama chake cha Yisrael Beitenu kimepata viti tisa.

Wabunge katika chama cha Gantz pia wameelezea uungaji mkono wao wa serikali ya muungano ambayo huenda ikajumuisha wadhifa wa waziri mkuu ambao utakuwa unazunguka kwa watu tofauti.

Baaada ya matokeo hayo ya awali, Lieberman alitoa mwito wa serikali ya muungano wa chama chake, Likud na Bluu na Nyeupe akisema taifa hilo linakabiliwa na hali ya kile alichotaja kuwa ni "dharura."

Huu ni uchaguzi wa pili katika kipindi cha miezi mitano nchini humo na rais Reuven Rivlin ambaye anatakiwa kuchagua mtu wa kuunda serikali ijayo akisema, ni lazima wajizuie kufanya uchaguzi mwingine.