1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu amtaka Abbas kutojitoa katika mazungumzo.

Halima Nyanza27 Septemba 2010

Waziri Mkuu wa Israel leo amemtaka Rais wa Mamlaka ya Palestina kutojitoa katika mazungumzo ya amani wakati walowezi wa kiyahudu wakianza tena ujenzi baada ya kumalizika kwa muda wa miezi 10, wa kusimamisha ujenzi.

https://p.dw.com/p/PNVY
Waziri mkuu wa Isreal Benjamin Netanyahu akiwa na Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas.Picha: AP

Dakika chache tu baada ya kumalizika kwa muda wa makubaliano yaliyowekwa ya kusimamisha ujenzi wa nyumba mpya katika eneo la ukingo wa magharibi, muda ambao ulimalizika rasmi usiku wa kuamkia leo, Waziri Mkuu wa Israel ametoa ombi kwa Rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas kuendelea kushiriki katika mazungumzon ya amani, ambayo yalianza rasmi mapema mwezi huu, katika jaribio la kupatikana kwa amani kati ya Waisrael na Wapalestina.

Bwana Abbas, ambaye kwa sasa yuko ziarani nchini Ufaransa, amejibu kwa haraka ombi hilo la Netanyahu, kwa kumtaka kiongozi huyo wa Waisrael kuongeza muda wa makubaliano wa kusimamisha ujenzi huo kwa ajili ya kuyaokoa mazungumzo hayo ya amani, kama alivyofahamisha msemaji wake, Nabil Abu Rudeina.

Amesema Netanyahu lazima achukue hatua kusitisha ujenzi huo kwa ajili ya kuendelea na mchakato wa mazungumzo hayo ya amani.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Israel, muda mfupi baada ya jua kuchomoza leo alfajiri, zana za ujenzi kama vile  mabuldoza yalianza kazi katika maeneo machache ya walowezi sehemu mbalimbali za ukingo wa magharibi, ingawa si kwa kiwango kikubwa.

Nahost Israel Palästinenser Siedler Baustopp beendet
Mabuldoza yakifanya kazi katika eneo la ujenzi katika makaazi ya walowezi ya Adam nje ya Jerusalem jana.Picha: AP

Aidha vimearifu kuwa ujenzi ulitarajia kuanza  katika makaazi mengine manane madogo, ikiwemo katika eneo la Kiryat Arba, ambako walowezi wahafidhina takriban 600 wanaishi, eneo ambalo liko kusini mwa mji wa Hebron.

Kumalizika kwa muda huo wa makubaliano ya kusitishwa ujenzi wa makaazi ya walowezi, kuna maanisha kwamba mtu yoyote ambaye alikuwa na ruhusa ya kujenga kabla ya makubaliano hayo, kwa sasa anaweza kufanya hivyo.

Nahost Israel Palästinenser Siedler feiern Ende Baustopp
Wanaharakati wa Israel kutoka katika kundi la ''amani sasa'' wakipepea bendera ya nchi hiyo.Picha: AP

Wakati mazungumzo ya amani yakiwa katika hatihati, juhudi za kimataifa bado zinaendelea kuchukuliwa, ambapo leo Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mahmoud Abbas ambaye bado hajaweka hadharani uamuzi wake juu ya kujitoa katika mazungumzo hayo, kutokana na ujenzi huo wa makaazi ya walowezi, anatarajiwa kukutana na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa mjini Paris kwa mazungumzo.

Bwana Abbas amewasili jana mjini Pars na kukutana na jumuia ya kiyahudi, ambapo baadaye aliwaeleza waandishi wa habari kwamba iwapo Israel haitaongeza muda wa kusitishwa kwa ujenzi wa makaazi ya walowezi, itakuwa ni kupoteza muda.

Wapalestina wanazingatia kuwa ujenzi wa makaazi ya wayahudi kama ni kikwazo kikubwa katika kupatikana kwa amani na kutishia kujitoa katika majadiliano iwapo ujenzi itaanza tena baada ya muda wa kusitishwa ujenzi huo kumalizika jana jioni.

Mwandishi: Halima Nyanza(ap,dap,afp)

Mhariri:M.Abdul-Rahman