1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu huenda akakubali ufumbuzi wa madola mawili

Oumilkher Hamidou9 Juni 2009

Waziri mkuu wa Israel anatazamiwa kutangaza muongozo wa siasa ya nje ya serikali yake

https://p.dw.com/p/I65r
Waziri mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: AP

Shinikizo la rais Barack Obama wa Marekani kwa serikali ya Israel limeanza kuleta tija.Kiongozi wa serikali ya Israel,Benjamin Netanyahu anataka kujibu hotuba muhimu iliyotolewa na rais wa Marekani,alkhamisi iliyopita katika chuo kikuu cha Cairo.Jukwaa alilolichagua Netanyahu ni chuo kikuu cha Bar Ilan huko Ramat Gan,karibu na Tel Aviv.Huko ndiko Netanyahu anakopanga,jumapili ijayo kumjibu Obama.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ametangaza azma ya kutoa hotuba muhimu kuhusu siasa ya nje.Hotuba hiyo inatazamiwa kufafanua misingi inayotazamiwa kufuatwa na Netanyahu na serikali yake ili kuweza kufikia amani na usalama.Katika mkutano wa baraza lake la mawaziri uliofanyika jumapili iliyopita,Netanyahu alizungumzia mkondo anaopanga kuufuata na kusema:

"Tunataka kufikia amani pamoja na wapalastina na pia pamoja na mataifa ya ulimwengu wa kiarabu na wakati huo huo kuwafikiana ipasavyo na Marekani na marafiki zetu kote ulimwenguni.Nnapigania amani imara itakayoihakikishia usalama Israel na wakaazi wake."

Magazeti ya Israel yanahisi Netanyahu anafikiria kubadilisha msimamo wake katika ugonvi pamoja na wapalastina.Nahum Barnea ameandika katika gazeti linalosomwa na wengi la Yedioth Achronot" inaweza kua hotuba ya mageuzi."Barnea anategemea,Netanyahu atakubali lengo la kufikiwa "makubaliano ya kanuni za mwisho" pamoja na wapalastina.Inamaanisha waziri mkuu huenda akaunga mkono fikra ya ufumbuzi wa madola mawili-jambo ambalo hadi wakati huu alikua akilikwepa.

Dhana za gazeti hilo si za bure.Duru za rais wa Israel zinasema,Shimon Perez anashirikiana na Netanyahu kwa lengo la kufufua mazungumzo ya amani pamoja na wapalastina.Lengo hapo ni kusawazisha uhusiano pamoja na mataifa ya kiarabu.Inasemekana waziri wa ulinzi Ehud Barack ndie aliyeshinikiza mkondo huo.Aliporejea kutoka ziarani mjini Washington ,June sita iliyopita,Ehud Barack alisema:


Israel Verteidigungsminister Ehud Barak Regierungskrise
Waziri wa ulinzi wa Israel Ehud BarakPicha: AP


"Kweli,kuna hitilafu za maoni pamoja na Marekani katika baadhi ya masuala,lakini kuna mengine ambayo msimamo wetu ni mmoja.Kwa jumla msingi wa uhusiano ni imara na wa dhati na hatustahiki kuuvuruga.Tunabidi tuzingatie ukweli wa mambo.Israel itafanya la maana kukubali fikra ya kupatikana ufumbuzi wa kimkoa na kutambua pia makubaliano yaliyofikiwa awali."

Anapozungumzia juu ya "Makubaliano ya awali",pengine anamaanisha mpango mpya wa amani unaojulikana kama "Road Map" ulioandaliwa mwaka 2002.Mpango huo ulipendekezwa na rais wa zamani wa Marekani George W. Bush .Mpango huo unasimamiwa mpaka leo na pande nne zinazoshughulikia suala la mashariki ya kati,yaani Marekani,Umoja wa mataifa,Umoja wa Ulaya na Urusi.Hata mwanasiasa wa siasa kali za mrengo wa kulia,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Israel Liebermann ameutambua hadharani mpango huo mpya wa amani.

Suala hilo hilo ndio kiini cha ziara ya mjumbe maalum wa Marekani katika Mashariki ya kati George Mitchell anaetazamiwa kuwasili hii leo mjini Jerusalem .Anataka kuzungumza na waziri mkuu Netanyahu,rais Peres,waziri wa mambo ya nchi za nje Liebermann na waziri wa ulinzi Barack.


Mwandishi:Sebastian Engelbrecht /ZR/Oummilkheir Hamidou

Mhariri:M.Abdul-Rahman