1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu kukutana na rais Putin

9 Machi 2017

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anatarajiwa kukutana na rais wa Urusi Vladimir Putin mjini Moscow siku ya Alhamis, ambapo wanatarajiwa kuzungumzia ongezeko la ushawishi wa Washia Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/2YsoD
Washington Israle Min isterpräsident Netanjahu bei Pk mit Trump
Benjamin NetanyahuPicha: picture-alliance/newscom/P. Benic

Kabla kuelekea Moscow, Netanyahu katika taarifa alisema, mazungumzo yake na Putin ni muhimu mno kwa usalama wa Israel na kwamba atapinga vikali uwepo wa Iran nchini Syria.

Kikosi cha Iran na wanamgambo wa kishia, Hezbollah, ambao wote ni maadui wa Israel, wote wanamuunga mkono rais wa Syria Bashar Al Assad katika mapigano yanayoendelea nchini humo.

Urusi inamuunga mkono pakubwa Assad na kuingilia kwake vita vya Syria, kulisaidia kulibadili wimbi la vita hivyo ambavyo sasa vinaonekana vitashindwa na serikali.

Mbali na taarifa hiyo aliyoitoa Netanyahu, waziri mkuu huyo aliliambia bunge la Israel pia kwamba ananuia kukubaliana na Urusi kuhusiana na mzozo wa Syria katika mazungumzo hayo.  

Hali nchini Syria ni ya umuhimu mkubwa kwa Israel

"Kuna jaribio la Iran kukita kambi kabisa nchini Syria wakiwa na majeshi ya ardhini na majini,"alisema Netanyahu, jambo linaloonekana kuwa kitisho kwa Israel. "Kuna jaribio pia la kuweka kikwazo dhidi yetu katika eneo la Golan, nitaonyesha pingamizi kubwa kwa uwezekano huu," aliongeza Netanyahu.

Israel Panzern-Übung in den Golanhöhen
Vifaru vya Israel katika mazoezi eneo la GolanPicha: picture-alliance/dpa/A. Safadi

Katika wiki za hivi majuzi Israel imeonesha jinsi inavyozingatia kwa umakini kitisho hichi. Gazeti la the Times nchini Israel liliripoti kwamba Januari 8, Israel ilifanya mashambulizi kadhaa katika eneo la Golan lililokuwa na wanamgambo wa kishia wa Hezbollah.

Kulingana na mshauri wa usalama wa ngazi ya juu Chagai Tzuriel, hali nchini Syria na matokeo yake ni ya umuhimu mkubwa kwa Israel. "Syria ni eneo muhimu mno, mataifa yenye nguvu kama Urusi na Marekani yako huko, na hata mataifa makubwa mashariki ya kati kama Uturuki na Iran. Isitoshe kuna makundi hasimu nchini humo, kama uongozi wa Assad, upinzani, Wakurdi na wanamgambo wanaojiitia Islamic State," alisema Chagai.

Wanaounga mkono wanasema adhana huleta usumbufu kwa wasio Waislamu

Wakati huo huo, bunge nchini Israel Jumatano, lilipitisha katika awamu ya kwanza miswada miwili itakayozuia misikiti kuadhini, ishara ya kuwaita Waislamu kwa sala, huku mswada mmoja ukitaka misikiti izuiwe kabisa kutumia spika kwa adhana.

Mswada huo wa pili ambao unanuia kupiga marufuku utumizi wa spika kuadhini katika miji kuanzia saa tano usiku hadi saa moja asubuhi, utafanyiwa marekebisho, huku kukiwa kumesalia vikao vitatu vya kuijadili miswada hiyo kabla haijakuwa sheria.

Miswada hiyo iliidhinishwa baada ya wabunge wa muungano tawala na wenzao wa Kiarabu kubishana vikali, hali iliyopelekea baadhi ya wabunge kuzipasua karatasi za mswada huo na kutimuliwa bungeni.

Israel Zusammenstöße in Jerusalem Polizisten auf dem Dach der Al Aksa Moschee
Msikiti wa Al-Aqsa mjini Jerusalem ni mmoja wa itakayoathirikaPicha: Reuters/B. Ratner

Huku miswada hiyo kimaandishi ikiwa inalenga maeneo yote ya kuabudu, Waislamu wanasema nia yake ni kutilia kikomo adhana misikitini, jambo ambalo limekuwa likifanywa tangu jadi.

Wanaounga mkono hatua hiyo ya bunge wanasema, inanuia kuzuia usumbufu kwa maelfu ya Waisraeli ambao sio Waislamu.

Rasimu ya kwanza iliyokuwa inalenga kudhibiti sauti siku nzima, ilikataliwa na bunge kwasababu ingemaanisha, kutopigwa kwa king'ora katika maeneo ya Wayahudi kila Ijumaa baada ya machweo ya jua, kuashiria kuanza kwa Sabato.

Mwandishi: Jacob Safari/DW/AFP/AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman