1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu kukutana na Trump mjini Washington

15 Februari 2017

Waziri Mkuu wa Israel anakutana leo na Rais Trump mjini Washington, katika mazungumzo ambayo wachambuzi wanasema yanafanyika wakati hali ya mambo ikiwa imechukua mkondo tofauti ya ilivyokuwa wakati wa kampeni.

https://p.dw.com/p/2Xa5S
US-Präsidentschaftskandidat Donald Trump mit Benjamin Netanjahu
Rais Trump na Waziri Mkuu Netanyahu baada ya mkutano wao wa awaliPicha: Picture-alliance/dpa/K. Gideon

Wakati mfalme Abdullah wa Jordan alipofunga safari kwenda Marekani hivi karibuni, licha ya kwamba hakuwa na uhakika kuwa atapokelewa na Rais Donald Trump, ilikuwa ishara kwamba alikuwa akibeba ujumbe muhimu. Katika ziara hiyo iliyofanyika siku tatu tu baada ya kuanzishwa kwa marufuku ya safari ya Rais Trump ambayo imeleta utata, hatimaye mfalme Abdullah alifanikiwa kukutana na Trump -kwa muda mfupi, na nje ya Ikulu ya White House.Walikutana katika Stafutahi ya sala ya kitaifa katika hoteli moja mjini Washington, mahali pasipo pa kawaida kufanyika mkutano wa aina hiyo.

Kabla ya mkutano wake na Rais Trump, Mfalme Abdullah alikuwa tayari amefnya mazungumzo na maafisa wengine muhimu wa utawala wa Marekani, wakiwemo Makamu wa Rais Mike Pence, Waziri wa Ulinzi James Mattis, na viongozi wa bunge.

Kwa ziara hiyo ya ghafla, Abdullah alifanikiwa sio tu kuwa kiongozi wa kwanza wa kiarabu kukutana na Rais Trump, bali pia alimpiku Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ambaye leo ndio anakutana na Rais huyo mpya wa Marekani.

Onyo kali kwa utawala wa Trump

USA New York - Abdullah II bin Al Hussein
Mfalme Abdullah wa JordanPicha: Getty Images/D. Angerer

Lengo mahsusi la mfalme wa Jordan halikuwa kuzungumzia marufuku ya kwenda marekani raia wa nchi saba zenye waislamu wengi, ingawa suala hilo pia lilikuwa muhimu. Badala yake, hii ikiwa ni kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la New York Times na vyombo vingine vya habari, Mfalme Abdullah aliwatahadharisha viongozi wa Marekani, kuhusu kuuhamishia ubalozi wa nchi hiyo mjini Jerusalem, jambo ambalo ni ahadi ya kampeni ya Rais Trump, na kuwaonya dhidi ya kuunga mkono upanuzi wa makazi ya walowezi, masuala ambayo anaamini yanaweza kusababisha mtafaruku katika Mashariki ya Kati. Vile vile alitoa hoja kuwa hatua hizo zinaweza kuhujumu matumaini ya kuweko mataifa mawili, kukwamisha vita dhidi ya makundi ya misimamo mikali, na kuyumbisha usalama wa taifa lake, ambalo linawapa hifadhi mamilioni ya wapalestina waliopoteza makazi yao.

Baada ya mazungumzo baina ya Rais Trump na mfalme Abdullah, Ikulu ya White House ilitoa tangazo lenye maneno yaliyochaguliwa kwa uangalifu, likisema upanuzi wa makazi ya walowezi 'unaweza usiwe wa kuleta tija' katika mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati. Zaidi ya hayo, wiki iliyopita Trump alionekana kulegeza msimamo wake kuhusu kuuhamishia ubalozi wa Marekani mjini Jerusalem. Aliliambia gazeti moja la Israel, kwamba kuuhamisha ubalozi sio uamuzi mwepesi, na kuongeza kuwa 'ataangalia hali ya mambo itakavyokuwa'.

Kila mmoja atampima mwingine

Israel Siedlung im Westjordanland
Ujenzi wa makazi ya walowezi wa kiyahudi ni suala lenye utata mkubwaPicha: picture alliance/newscom/D. Hill

Kwa kuyazingatia haya, mtu anaweza kusema kile kilichotarajiwa kuwa mkutano rahisi kwa maswahiba wawili waliomwagiana sifa wakati wa kampeni, kimegeuka kuwa changamoto kubwa.

Mkuu wa Masomo kuhusu Marekani katika Chuo Kikuu cha London Iwan Morgan, anasema viongozi hao watajaribu kuonyesha muafaka hadharani, lakini ikiwa hali hiyo itaishia katika makubaliano muhimu ya kisera, ni suala la kusubiri na kuona.

Mtaalamu wa masuala ya Usalama wa kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Gallen cha nchini Uswisi, James Davis anasema Netanyahu anatafuta kitu cha kuufurahisha mfungamano wa vyama vya mrengo wa kulia anaouongoza, kwa sababu uswawishi wake umekuwa ukiporomoka mnamo miezi ya hivi karibuni.

Davis anasema hatarajii makubaliano muhimu kutoka katika mkutano baina ya Trump na Netanyahu, kwa sababu Trump atabidi kuwa makini zaidi ili asiwaudhi washirika wa Marekani katika ulimwengu wa Kiarabu, na vile vile Netanyahu atajizuia kumwekea shinikizo, akihofia kutibua mambo kama ilivyotokea wakati wa utawala wa Rais Barack Obama.

Kitu kimoja ambacho wachambuzi wanatabiri kitawaunganisha Trump na Netanyahu, ni msimamo mkali dhidi ya Iran, kwa sababu hilo linaweza kuwavutia hata viongozi wa kiarabu, ambao ushawishi wa kikanda wa Iran unawatia tumbojoto.

 

Mwandishi:Michael Knigge

Tafsiri: Daniel Gakuba

Mhariri: Josephat Charo