1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu kuwa na mazungumzo na Mubarak kesho Jumanne.

Sekione Kitojo28 Desemba 2009

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kuwa atakutana kwa mazungumzo kesho Jumanne na rais Hosni Mubarak wa Misr katika juhudi za kutafuta amani ya mashariki ya kati.

https://p.dw.com/p/LEmb
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akipeana mkono na kiongozi wa chama cha Kadima Tzipi Livni, kushoto.Picha: AP

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema jana Jumapili kuwa atakuwa na mazungumzo nchini Misr kesho Jumanne na rais Hosni Mubarak katika kutafuta njia za kusukuma mbele juhudi za kuleta amani katika mashariki ya kati. Wakati huo huo maafisa wawili kutoka kundi la Hamas wameingia nchini Misr kutoka Gaza jana Jumapili kujadili jibu la Israel kuhusiana na pendekezo la kubadilishana wafungwa.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amewaambia waandishi habari mwanzoni mwa mkutano wa kila wiki wa baraza la mawaziri kuwa anaamini Israel ina nia ya kusukuma mbele hatua za kuleta amani katika njia kadha. Netanyahu amesema ameomba mkutano na rais Hosni Mubarak baada ya mkuu wa kitengo cha ujasusi nchini Misr Omar Suleiman kufanya mazungumzo nchini Israel wiki iliyopita.

Misr na Ujerumani zinafanya upatanishi kuhusu kubadilishana wafungwa kati ya Israel na kundi la Hamas , ambapo kundi hilo linalodhibiti eneo la Gaza , litamwachilia huru mwanajeshi Gilad Shalit na Israel itawaachia wafungwa 1,000 wa Kipalestina kati ya wafungwa 11,000 walioko katika jela za Israel.

Msemaji wa Hamas amesema kuwa viongozi wawili wa kundi hilo ambao wanaishi Gaza , Mahmoud al-Zahar na Khalil al-Hayya wanakwenda Syria kupitia Misr kesho Jumanne. Wanapanga kujadili na viongozi wao walioko Damascus kuhusu jibu la Israel kuhusu mpango huo wa kubadilishana wafungwa. Kwa kauli mbiu "ushindi na uvumilivu" chama kinachoongoza eneo la Gaza kimetayarisha shughuli mbali mbali jana Jumapili ikiwa ni pamoja na mikutano na sherehe katika kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu pale Israel ilipofanya mashambulizi yake dhidi ya Gaza kwa muda wa wiki tatu.

Hamas feiert Jahrestag und kündigt Überraschung an Ismail Hania
Waziri mkuu Ismail Haniyeh kutoka katika ukanda wa Gaza akipepea bendera za chama hicho pamoja na za Palestina wakiadhimisha mwaka mmoja tangu Israel kushambulia eneo hilo Desemba 27 , mwaka jana.Picha: AP

Meya wa mji wa Sderot David Buskila amesisitiza jana Jumapili kuwa hali katika ukanda wa Gaza imebaki kuwa mbaya. Anaamini kuwa kukaribiana kisiasa ni suala la haraka na lazima katika mzozo huu.

Serikali yetu inapaswa kukaa na yeyote ambaye anajali kuhusu hali ya Gaza. Mamlaka ya Palestina ama yeyote ambaye ana madaraka ya kuleta mabadiliko katika Gaza na kutafuta suluhisho la kisiasa. Sisi ni majirani, tulikuwa majira hapo kabla. Majirani wema.

Kwa wakati huu hakuna makubaliano na sifahamu iwapo kutakuwa na makubaliano, waziri mmoja aliyeshiriki katika mkutano wa baraza la mawaziri jana Jumapili amesema akimnukuu Netanyahu.

Netanyahu mara ya mwisho kutembelea Misr ilikuwa Mei mwaka huu, alikutana na Mubarak katika mji wa kitalii wa Sharm el-Sheikh, ambako kiongozi huyo wa Israel aliahidi kuendeleza mazungumzo na Wapalestina.

Kiongozi huyo wa Israel mpenda mabavu alikuwa na mkutano wa saa mbili na kiongozi wa upinzani Tzipi Livni jana Jumapili kuhusiana na chama chake cha mrengo wa kati cha Kadima kujiunga na serikali ya umoja wa kitaifa. Hakuna mwanasiasa yeyote kati yao aliyetoa taarifa baada ya mazungumzo hayo lakini chama cha Kadima kimesema kuwa viongozi wake watakutana leo Jumatatu kujadili pendekezo la Netanyahu.

Lakini ripoti nchini Israel zinasema kuwa waziri huyo mkuu anapendekeza kutoa wizara mbili tu zisizo za wizara maalum katika baraza la mawaziri lililoongezwa. Pia anasisitiza kuwa hakutakuwa na mabadiliko katika mpango wa serikali yake ya mrengo wa kulia na kwamba atabaki kuwa na madaraka katika sera zinazohusu juhudi za Marekani za kufufua hatua za kuleta amani katika mashariki ya kati. Livni ameeleza wasi wasi mkubwa baada ya mkutano wake wa kwanza na Netanyahu siku ya Alhamis, akisema kuwa pendekezo lake ni mtego.

Lakini kutokana na wajumbe wengi wa chama cha Kadima kutishia kukikimbia chama hicho kwenda serikalini, waziri huyo wa zamani wa mambo ya kigeni ameliweka suala hilo katika ajenda ya mazungumzo na viongozi wa chama chake.

Mwandishi : sekione Kitojo / RTRE / AFPE

Mhariri : Mwadzaya thelma