1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu na Livni kila mmoja adai kushinda uchaguzi mkuu wa Israel

Aboubakary Jumaa Liongo/AFP11 Februari 2009

Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Tzipi Livni na Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo Benjamin Netanyahu kila mmoja amedai ushindi katika uchaguzi mkuu uliyofanyika jana.

https://p.dw.com/p/GrOf
Kiongozi wa Chama cha Likud Benjamin NetanyahuPicha: AP


Chama cha Kadima kinachoogozwa na Bi Livni kimepata viti 28 kati ya 120 vya bunge la nchi hiyo Knesset, wakati Likud cha Benjamin Netanyahu kimepata viti 27.


Akizungumza mbele ya wafuasi wake kwenye makao makuu ya chama cha Kadima Waziri huyo wa Nje wa Israel Bi Livni amesema kuwa wananchi wa Israel wameamua kukichagua chama chake na kumuomba Benjamin Netanyau ajiunge naye katika kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ikiongozwa naye.


Tzipi Livni anajiwinda kuwa mwanamke wa pili kushika wadhifa wa uwaziri mkuu katika historia ya miaka 60 ya taifa la Israel, baada ya Marehemu Golda Meir kutoka chama cha Leba aliyekua Waziri mkuu 1969 hadi 1974.


Hata hivyo kwa Benjamin Netanyahu, pamoja na chama chake cha Likud cha mrengo wa kulia kuwa nyuma ya Kadima kwa kiti kimoja, anapewa nafasi kubwa ya kuwa Waziri Mkuu mpya wa Israel.


Chini ya mfumo wa siasa huko Israel chama kinachoongoza kwa wingi wa viti bungeni siyo lazima kuwa na jukumu la kuunda serikali, na wachambuzi wengi wa siasa za Israel kabla ya uchaguzi huo, walibashiri ya kwamba Netanyahu yuko katika nafasi nzuri ya kupata idadi ya wabunge wanaotakiwa ambao ni 61.Hii ni kutokana na uhusiano wa kisera na vyama vingine husunai vile vyenye kuegemea mrengo wa kulia


Waziri huyo mkuu wa zamani aliwaambia wafuasi wake ya kuwa, chama chake kimepata ushindi na kwamba ana hakika ya kuongoza serikali ijayo.


Chama cha Yisrael Beitenu cha mrengo wa mbali kulia kinachoongozwa na Avigdor Lieberman kimepata viti 15 na kushika nafasi ya tatu hali inayokifanya kuwa na turufu muhimu katika uundwaji wa serikali ya mseto.


Chama chenye kuegemea mrengo shoto kwa mbali cha Labour kinachoongozwa na Waziri wa Ulinzi Ehud Barak kimepata viti 13, yakiwa ni matokeo mabaya kabisa katika historia ya chama hicho.


Kutokana na matokeo hayo wachambuzi wa siasa za nchi hiyo wanasema kuwa huenda serikali itakayoundwa itakuwa ni ile inayoegemea mrengo wa kulia, hii ni kutokana na vyama vya Likud na kile cha Beitenu kuwa na ujumla wa viti vingi.


Gideon Saar ni mbunge kutoka kikundi kilichojitenga na chama cha Likud.


CLIP:SAAR

´´Kutokana na tahadhari inabidi sote kusubiri muda mrefu kwa matokeo kamili, lakini kuna baadhi ya vitu vichache ambavyo vikowazi kabisa.Kwanza Likud ni chama kilichopata umaarufu zaidi toka kumalizika kwa uchaguzi uliyopita.Pili mrengo wa kulia ambao siasa zake hazikubaliwi na serikali ya sasa umepata viti vingi´´


Na Bi Livni ambaye chama chake cha Kadima ni cha mrengo wa kati amethibitisha hilo ambapo amesema kuwa Israel haiwezi kuwa upande wa kulia, kama ambavyo amani haiwezi kuwa upande wa kushoto.


Hali hiyo inaifanya Israel kutumbukia katika mvutano mpya wa madaraka na kuifanya kuwa katika hali ya wasi wasi kisiasa katika wiki zijazo.


Kkwa upande wake Serikali ya Mamlaka ya Palestina inayoungwa mkono na nchi za magharibi imekuwa ikichukua tahadhari kutosema dhahiri ni mgombea gani inayempenda, lakini mjumbe wa ngazi ya juu wa serikali hiyo katika mazungumzo ya amani ya mashariki ya kati Saeb Erakat alielezea kufadhaishwa na kufanya vizuri kwa vyama vyenye kufuata mrengo wa kulia.


CLIP:ERAKAT

´´Nadhani matakwa ya amani hayatoweza kufikiwa na serikali yoyote ya mseto itakayoundwa kutokana na matokeo ya uchaguzi huu.Serikali yoyote itakayoundwa haitokubaliana na suluhisho la kuwepo kwa mataifa mawili, hatokubali kutekeleza makubaliano yaliyotiwa saini na itaendelea na ujenzi wa makaazi ya walowezi na pia kuendelea na mashambulizi yao.Nadhani tutawachukulia kuwa siyo washirika´´


Kundi la Hamas linalodhibiti Ukanda wa Gaza ambao bado huko katika madhara ya wiki tatu za uvamizi wa majeshi ya Israel uliyogharimu maisha ya wapalestina zaidi ya 1300 na waisrael 13, limesema kuwa viongozi wote wa Israel wako sawa.


Msemaji wa kundi hilo la Hamas Fawzi Barhuni amesema kuwa waisrael wameamua kuwachagua wagombea aliyowaita makatili ambao ni hodari katika kutoa kauli za kihafidhina.


Kiongozi wa Likud Benjamin Netanyahu ambaye mwaka 1996 alikuwa Waziri Mkuu kijana kuwahi kuongoza Israel akiwa na umri wa miaka 46, katika kampeni zake alisema kuwa atakapoingia madarakani atahakikisha anauangusha utawala wa Hamas huko Gaza.


Matokeo rasmi ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutolewa baadaye hii leo.