1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

New York. Baraza la usalama la umoja wa mataifa laidhinisha azimio juu ya Darfur.

1 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBdF

Baraza la usalama la umoja wa mataifa limepiga kura kwa kauli moja kuidhinisha uwekaji wa jeshi la pamoja kati ya umoja wa Afrika na umoja wa mataifa katika jimbo la Sudan la Darfur.

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon ameieleza hatua hiyo kuwa ya kihistoria na ya mfano.

Jeshi hilo litakalokuwa na wanajeshi 26,000 mchanganyiko, litakuwa na kazi ya kulinda amani katika jimbo la Darfur kutoka kwa jeshi la umoja wa Afrika lililokuwa na wanajeshi 7,000 na ambalo halikuwa na vifaa vya kutosha.

Katibu mkuu Ban aliwaambia wanachama 15 wa baraza la usalama kuwa kuidhinisha jeshi hilo , walikuwa wanatoa ishara ya wazi na nzito ya uwajibikaji ili kuleta hali bora ya maisha kwa watu wa jimbo hilo.

Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown , akiwa ziarani katika umoja wa mataifa , ameainisha mpango huo wa umoja wa mataifa kwa ajili ya Darfur na kuonya kuwa vikwazo zaidi vinaweza kuwekwa iwapo mauaji yataendelea.