1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK: Triesman ataka Sudan iwekewe vikwazo

22 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCPu

Waziri anayehusika na maswala ya Afrika nchini Uingereza, David Triesman, anataka Sudan iwekewe vikwazo na isiuziwe silaha kama rais Omar el Bashir wa nchi hiyo hatatimiza ahadi yake ya kuwaruhusu wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika na wa Umoja wa Mataifa kwenda katika jimbo la Darfur.

Triesman aliwaambia waandishi wa habari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani kwamba umoja huo unatakiwa ufanye haraka kuunda kikosi na umteue mjumbe wake maalumu wa Sudan. Nafasi hiyo imekuwa wazi tangu mdachi, Jan Pronk, alipotimuliwa kutoka Sudan mwaka jana.

David Triesman amesema ikiwa mpango wa kuwatuma wanajeshi 4,000 zaidi kwenda Darfur hautatekelezwa kufikia mwishoni mwa mwezi ujao, jumuiya ya kimataifa inatakiwa ijiandae kukabiliana na athari za kimataifa.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, alimuandikia barua rais wa Sudan Omar el Bashir mwishoni mwa mwezi uliopita kuhusu wasiwasi wa Sudan juu ya kikosi cha kulinda amani lakini mpaka sasa bado anasubiri majibu.