1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK : Uchokozi wa Israel huko Gaza watakiwa kulaaniwa

10 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCuM

Israel imeshutumiwa hapo jana wakati wa mjadala wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya shambulio lake la kijeshi lililosababisha maafa katika Ukanda wa Gaza na kutolewa kwa wito kadhaa wa kuwekwa kwa wanajeshi wa Umoja wa Mataifa kusimamia usitishaji wa mapigano kati ya pande hizo mbili.

Nchi za Kiarabu zimeongoza wito wa kutaka kulaaniwa vikali kwa shambulio hilo la Israel la Jumaatano lililouwa Wapalestina 18 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto kwenye mji wa Beit Hanun katika Ukanda wa Gaza.

Mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa Ryad Mansour amesema shambulio hilo ni ugaidi uliodhaminiwa na taifa ni uhalifu wa kivita ambapo kwayo wahusika lazima wawajibishwe chini ya sheria ya kimataifa.

Qatar imewasilisha rasimu ya azimio kwa niaba ya nchi za Kiarabu lenye kulaani kile ilichokiita kuwa mauaji ya Israel huko Beit Hanun na kutowa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano kati ya Israel na Wapalestina na Umoja wa Mataifa kutuma kikosi cha uangalizi na kuchunguza mauaji hayo.

Mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa ameelezea matumaini yake kwamba rasimu ya azimio hilo yumkini likapigiwa kura leo hii.