1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK : Umoja wa Mataifa waiwekea vikwazo Iran

24 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCgb

Mjini New York Marekani Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekubaliana kwa kauli moja kupitisha azimio la kuiwekea vikwazo Iran kutokana na mpango wake wa nuklea.

Imechukuwa miezi miwili ya mazungumzo magumu kwenye baraza hilo kuunda maudhui ya azimio hilo ambapo hapo awali Urusi na China zilikuwa zikipinga uwekaji wa vikwazo dhidi ya Iran.

Azimio hilo nambari 1737 linapiga marufuku uuzaji na upelekaji wa vitu vya nuklia na teknolojia yake kwa Iran katika jitihada za kuzuwiya urutubishaji wa uranium ambao unaweza kutumika kutengeneza mabomu.Kadhalika watu fulani watakaotajwa kwa majina watawekewa vikwazo vya usafiri.

Iran ambayo mapema mwaka huu imegoma kuachana na kazi ya kurutubisha uranium ili ipatiwe vifuta jasho vya kiuchumi imelilani azimio hilo kuwa sio la halali na kusema kwamba halitoathiri shughuli zake za nuklea kwa dhamira ya amani.