1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK.China yatakiwa itekeleze azimio la baraza la usalama

16 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD2C

Marekani imeitaka China itekeleze azimio la umoja wa mataifa juu ya kuiwekea vikwazo Korea Kaskazini kufuatia hatua ya nchi hiyo ya kufanya jaribio la silaha za nyuklia wiki iliyopita.

Balozi wa Marekani kwenye umoja wa mataifa John Bolton amesema China ina jukumu la kuheshimu azimio 1718 lililopitishwa kwa kauli moja na baraza la usalama la umoja wa mataifa.

Baraza la usalama limeiwekea Korea Kaskazini vikwazo vya biashara ya silaha, bidhaa za anasa na usafiri dhidi ya baadhi ya maafisa wa Korea kaskazini.

Biashara nyingi kutoka Korea Kaskazini zinapitia China inayohofia wimbi la wakimbizi endapo serikali ya Pyongyang itaanguka.

China imesema hatua ya kukaguliwa bidhaa zinazo ingia na kutoka Korea Kaskazini huenda ikazidisha mivutano.

Australia imesema kuwa itazipiga marufuku kuingia katika bandari zake meli za Korea Kaskazini.

Waziri wa mambo ya nje wa Australia Alexander Downer amesema hatua hiyo itaambatana na azimio la baraza la usalama. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleeza Rice anatarajiwa kuzuru eneo la Asia katikati ya wiki hii kutafuta uungwaji mkono zaidi wa azimio la baraza la usalama la umoja wa mataifa dhidi ya Korea Kaskazini.