1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ngono ni njia ya kujikimu kimaisha Afrika ya Kati

Amina Abubakar2 Machi 2016

Human Rights Watch wanasema licha ya wasichana wengine kubakwa na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, kuna mifano ya wale wanaojihusisha wenyewe na biashara ya ngono ili kujikimu kimaisha.

https://p.dw.com/p/1I5Iu
Picha: picture-alliance/AA/H. Serifio

Baadhi ya wasichana wanaoishi katika kambi ya watu waliopoteza makaazi yao katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wameliambia shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch (HRW) kwamba wanajeshi wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo (MINUSCA) wanawadhulumu kimapenzi.

Lakini kando na hilo, inasemekana baadhi ya wasichana wanakubali kujihusisha katika biashara ya ngono ili kujikimu kimaisha, licha ya MINUSCA kusema kuwa inafanya kila juhudi kukomesha visa hivyo vinavyodaiwa kufanywa na wanajeshi wake.

Wakati akitafuta chakula au pesa kidogo katika kambi ya MINUSCA, msichana mmoja mwenye umri wa miaka 18 alibakwa na wanaume watatu.

"Walinichukua kichakani, walikuwa na silaha wakasema wataniuwa iwapo nitakataa," alisema msichana huyo alipozungumza na shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch.

Mkusanyiko wa wanajeshi, vita na umasikini katika Jamhuri ya Afrika ya Kati umesababisha visa vya kuogofya vya udhalilishaji wa kingono. Tangu kuanza kwa operesheni ya wanajeshi wa kulinda amani nchini humo mnamo Septemba mwaka wa 2014, visa 42 vya udhalilishaji wa kingono vimeripotiwa huku wachunguzi kutoka Ufaransa wakichunguza madai ya ubakaji dhidi ya wanajeshi waliopelekwa katika koloni lake la zamani.

Aidha mwaka uliopita thuluthi tatu ya kesi zilizoripotiwa miongoni mwa vikosi takriban 16 vya kulinda amani vya Umoja wa mataifa duniani viliwahusisha wanajeshi wa MINUSCA. Mjumbe wa Umoja huo mjini Bangui, Onanga-Anyanga, amesema visa hivyo ni vya kusikitisha na visivyokubalika.

Tukio la hivi karibuni lilitokea mwezi wa Februari lililowahusisha watoto wanne katika kambi ya watu waliopoteza makaazi waliodaiwa kudhulumiwa na wanajeshi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Licha ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, kumfuta kazi mkuu wa kikosi cha wanajeshi 10,000 cha MINUSCA mwezi Agosti, kufuatia kuongezeka kwa visa vya udhalilishwaji wa kingono, bado madai hayo yanazidi kuongezeka. Wanajeshi wanaohusishwa na visa hivyo viovu wanasemekana kutokea mataifa kama Congo, Morocco, Niger, Bangladesh na Senegal.

Zentralafrikanische Republik Bangui Proteste und Gewalt
Picha: picture-alliance/AA/H.C. Serefio

Katika kila tukio lililotokea katika Jamhuri ya Afrika ya kati linasemekana kutokea katika kambi ya watu waliopoteza makaazi yao iliyoko karibu na kambi ya MINUSCA iliyowekwa hapo kwa ajili ya kuwalinda watu hao.

Umasikini wawafanya wasichana wajiingize kwenye ukahaba

Hata hivyo, wanajeshi wa Umoja wa Mataifa sio wa kulaumiwa kwa kiwango kikubwa kwa sababu baada ya miaka mitatu ya mapigano kati ya Waislamu na Wakristo yaliyoyumbisha uchumi wa taifa hilo na nchi kuwa katika vurugu, visa vya udhalilishaji wa kingono vimekuwa vikienea.

Kambi moja ya wakimbizi ya M'poko iliyoko karibu na mji wa Bangui imegeuka kuwa makaazi duni iliyojaa wakimbizi na umasikini, huku wasichana wadogo wakikubali kuwa na mahusiano ya kingono na wanaume wakiwemo wanajeshi wa kulinda amani ili weweze kupata chakula kama mkate au fedha ambayo ni chini ya euro moja.

"Wanawake wana miili yao tu ya kuuza ili kulisha familia zao iwapo itakuwa waume zao waliuwawa au kupotea," alisema Irene Ngogui, anayefanya kazi na shirika moja lisilokuwa la kiserikali. Irene anasema saa nyengine ni wazazi wenyewe wanaowatuma watoto wao kujiuza.

Kwa hiyo kashfa zinazowahusisha wanajeshi wa MINUSCA hazikuwashitua watu wanaoishi katika kambi hiyo ya M'poko lakini tangu kashfa hizo zilipoanza, jeshi la MINUSCA limesema limechukua mikakati ya kuyawekea mipaka majeshi hayo. Doria ya polisi wa ndani pia imeongezwa hasa wakati wa usiku ili kuhakikisha wanajeshi hao wa Umoja wa Mataifa hawapatikani mahali wasipohitajika.

Mwandish: Amina Abubakar/AFP
Mhariri: Josephat Charo