1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni lini Marekani itaishambulia Syria?

29 Agosti 2013

Rais Barack Obama wa Marekani amesema Jumatano (28.08.2013) bado hajasaini mpango wa kuishambulia Syria lakini kuna uwezekano wa kuchukuliwa hatua hiyo baada ya Marekani kuashiria haitohitaji ruhusa ya Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/19YPF
Rais Barack Obama wa Marekani.
Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: Reuters

Shutuma za kisiasa nchini Uingereza zimeweka mashaka iwapo Uingereza itaweza kujiunga na hatua ya kijeshi ya Marekani kuiadhibu serikali ya Rais Bashar al Assad wa Syria kutokana na shambulio lake la silaha za sumu iwapo hatua hiyo ya kijeshi itachukuliwa kabla ya wiki ijayo.

Timu ya wakaguzi wa Umoja wa Mataifa inaendelea na kibaruwa kigumu mjini Damascus kuchukuwa vipimo kwa wahanga wa shambulio hilo linalodaiwa kuwa la gesi ya sumu ambalo limeuwa mamia ya watu wiki iliopita na kutishia kuyaingiza mataifa ya magharibi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria ambavyo hatima yake haijulikani.

Obama ambaye alikuwa ameonya kwamba matumizi ya silaha za sumu nchini Syria yatakuwa yamevuka mstari mwekundu uliowekwa na Marekani amesema serikali ya Marekani imefikia hitimisho la uhakika kwamba utawala wa Assad ndio wa kulaumiwa kwa shambulio hilo la silaha za sumu wiki iliopita.

Afisa mwandamizi wa Ikulu ya Marekani ameliambia shirika la habari la AFP kwamba serikali itawataarifu wabunge waandamizi leo hii kuhusu taarifa za kijasusi juu ya shambulio hilo la silaha za sumu.

Bado sikuamuwa

Alipoulizwa lina anapanga kuamuru shambulio la Marekani dhidi ya Syria ambalo linatarajiwa kuanza na mashambulizi ya makombora Obama amekiambia kipindi cha televisheni cha Marekani cha PBS katika mahojiano kwamba bado hakufanya uamuzi.

Rais Barack Obama wa Marekani.
Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: Reuters

Lakini ameonya kwamba Marekani inapanga kuiadhibu Syria ili kuhakikisha kwamba nchi hiyo haitorudia tena jambo hilo.

Amekiri kwamba mashambilizi hayo ya kiasi fulani yanayopangwa na Marekani hayatositisha mauaji ya raia nchini Syria na pia anaona kwamba kujihusisha katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo ambayvo tayari vimeuwa watu 100,000 hakutosaidia hali hiyo.

Kiongozi huyo wa Marekani anayetaka kuacha haiba ya kumaliza vita vya kigeni na kutoingia katika vita vipya amesema ni muhimu kutuma ujumbe wa wazi sio tu kwa Syria bali duniani kote. Amesema inabidi wahakikishe kwamba wakati nchi zinapovunja kanuni za kimataifa juu ya silaha kama vile za sumu ambazo zinaweza kuwa kitisho kwao nchi hizo zinawajibishwa.

Diplomasia ndio suluhisho

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameyataka mataifa makubwa kuepusha mzozo huo wa Syria na kusema kwamba wakaguzi wa Umoja wa Mataifa inapaswa kupewa muda zaidi na kutowa ombi jipya kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kundokana na tafauti zao kuhusu Syria.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.Picha: Reuters

Amesema "Mazungumzo na usuluhishi wa kisiasa huu ni msimamo muhimu sana .Na ndio sababu kwa nini Umoja wa Mataifa umekuwa ukifanya maandalizi ya Mkutano wa Pili wa Kisiasa wa Geneva na ni matarajio yangu ya dhati mkutano huo utaitishwa kwa haraka."

Wakati huo huo Rais Vladimir Putin wa Urusi na mwenzake wa Iran Hassan Rouhani wanakubali kwamba matumizi ya silaha za sumu ni jambo lisilokubalika lakini wanapinga kuingiliwa kati kijeshi katika nchi hiyo mshirika wao.Taarifa ya Ikulu ya Urusi imesisitiza haja ya kutafuta njia za kuutatuwa mzozo huo kwa njia ya kidiplomasia tu.Marais wa nchi hizo mbili wameujadili mzozo huo wa Syria kufuatia ombi la Iran.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP
Mhariri: Josephat Charo