1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni miaka 25 ya muungano Ujerumani

3 Oktoba 2015

Ujerumani Jumamosi (03.10.2015) imeadhimisha miaka 25 tokea kuungana upya kwa furaha kwa viongozi wake kulihimiza taifa kukusanya nguvu ile ile na mshikamano kukabiliana na wimbi kubwa la pili la wakimbizi.

https://p.dw.com/p/1GiAq
Rais Joachim Gauck akihutubia katika maadhimisho ya miaka 25 ya muungano wa Ujerumani.(03.10.2015).
Rais Joachim Gauck akihutubia katika maadhimisho ya miaka 25 ya muungano wa Ujerumani.(03.10.2015).Picha: Reuters/R.Orlowski

Madhimisho haya ya siku iliyoziunganisha tena Ujerumani ya mashariki ya ukoministi na ile ya magharibi ya kibepari kuwa taifa moja yanakuja wakati nchi hiyo yenye nguvu kubwa za kiuchumi barani Ulaya ikiwa njia panda.

Kansela Angela Merkel na Rais Joachim Gauck wa Ujerumani ambao wote wawili wamekulia chini ya utawala wa ukomunisti walihudhuria sherehe hizo katika mji mkuu wa kibiashara wa Frankfurt kwa kauli mbiu iliovuma "Kuondokana na Mipaka."

Katika hotuba kuu Rais Gauck amezingatia mzozo wa wakimbizi na kutowa wito kwa Wajerumani kurudia tena mwamko wao kwamba wanaweza ambao waliutumia wakati nchi hiyo ilipokuwa kwenye miezi migumu kati ya kuanguka kwa Ukuta wa Berlin na kuungana upya kwa Ujerumani ya mashariki na magharibi.

Ujasiri na kujiamini

Gauck ambaye aliwahi kuwa mchungaji mpinzani amesema "Leo tunasheherekea ujasiri na kujiamini tuliokuwa nao wakati huo. Tuitumie sherehe hii kama daraja."

Rais Joachim Gauck na mshirika wake Daniela Schadt katika maadhimisho ya miaka 25 ya muungano wa Ujerumani.(03.10.2015)
Rais Joachim Gauck na mshirika wake Daniela Schadt katika maadhimisho ya miaka 25 ya muungano wa Ujerumani.(03.10.2015)Picha: picture-alliance/dpa/B.Roessler

Amesema hapo mwaka 1990 pia kulikuwa na suala lenye uhalali kwamba : "Je tunaweza kukabiliana na changamoto hii?". Wakati huo pia kulikuwa hakuna mfano wa kihistoria kuufuata.Hata hivyo mamilioni ya watu walijitwika jukumu la taifa la kuungana tena kuwa taifa badala tu ya kuwa sehemu ya taifa.

Merkel ambaye hapo mwezi wa Novemba atatimiza miaka kumi madarakani mwaka huu anakabiliwa na kuwasili kwa watu milioni moja wanaokimbia vita na shida.

Kutokana na nguvu zake za kiuchumi na soko imara la ajira wapiga kura kwa kiasi kikubwa wameuunga mkono sera yake ya konyosha mkono wa msaada.

Kukaribishwa kwa wahamiaji

Watu wa kujitolea wamewakaribisha mamia kwa mamia ya wakimbizi kwa mikono miwili na kuwapa msaada mkubwa wa mahitaji muhimu jambo ambalo Merkel amesema limemfanya "ajivunie nchi yake."

Kansela Angela Merkel (wa pili kulia) Rais Joachim Gauck (wa tatu kulia) mjini Frankfurt. ( 03.10.2015)
Kansela Angela Merkel (wa pili kulia) Rais Joachim Gauck (wa tatu kulia) mjini Frankfurt. ( 03.10.2015)Picha: Reuters/K.Pfaffenbach

Hata hivyo kutokana na kuongezeka kwa idadi hiyo ya wakimbizi umashuhuri wa Merkel umeshuka wakati akishutumiwa na wakosoaji wake ndani na nje ya nchi kwa kukubali kwake kupokea mzigo huo kwa Ulaya.

Merkel amesema Jumamosi kwamba mzozo wa wahamiaji unawakilisha mtihani muhimu kwa Umoja wa Ulaya.Amewaambia waandishi wa habari mjini Frankfurt kwamba baada ya kupita miaka 25 wanakabiliwa na changamoto kubwa kwa suala la wakimbizi.

Amesema "Hivi sasa pia Wajerumani hawawezi kulitatuwa tatizo hilo peke yao bali kwa kushirikiana na Ulaya tu, kugawana mzigo huo kwa haki pamoja na dunia nzima."

Umajumui wa Ulaya

Mapema katika hotuba yake ya kila wiki kwa njia ya mtandao amesema jambo hilo linapasa kujumuisha hatua mbali mbali ikiwa ni pamoja na juhudi za umajumui ya Ulaya kulinda mipaka yao ya nje,msaada wa maendeleo na utatuzi wa mizozo katika nchi wanakotokea wakimbizi na kugawana kwa mpangilio kwa watu wapya wanaowasili ndani ya Umoja wa Ulaya.

Kansela Angela Merkel akisalimiana na wananchi maadhimisho ya siku ya muungano wa Ujerumani . (03.10.2015)
Kansela Angela Merkel akisalimiana na wananchi maadhimisho ya siku ya muungano wa Ujerumani . (03.10.2015)Picha: picture-alliance/dpa/B. Roessler

Baadhi ya nchi zimekuwa zikipinga juhudi za Ujerumani kushika hatamu za uongozi wa Ulaya kufikia hata Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban kumshutumu Merkel kwa "ubeberu wa maadili."

Gauck ameelezea uwelewa wake kwa hofu za nchi za Ulaya mashariki ambazo pia hazina uzoefu wa kujumuika na wageni tafauti na tajiriba waliokuwa nayo mataifa ya magharibi tokea kizazi hadi kizazi.Kwa mujibu wa Gauck wameona kwamba mabadiliko ya misimamo kwa wakimbizi na wahamiaji yanaweza kuja kwa kupitia mchakato mgumu wa muda mrefu.

Tarehe 3 Oktoba mwaka 1990 katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja baada ya kuanguka kwa Ukuta wa Berlin katika mapinduzi yasiomwaga damu mkataba ulioziunganisha tena nchi mbili za Ujerumani ulianza kazi kwa shangwe kubwa.

Tokea wakati huo siku hii imekuwa siku ya mapumziko kuadhimisha siku ya taifa ya Ujerumani.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Bruce Amani