1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nicolas Sarkozy amefikia lengo lake la kuwa rais wa Ufaransa.

8 Mei 2007

Nicolas Sarkozy ni rais mpya wa Ufaransa na mrithi wa Jacques Chirac ambaye tangu mwaka 1995 amekuwa akiishi katika kasri la Elysee. Wafuasi wake walipokea habari hiyo kwa vifijo na shangwe.

https://p.dw.com/p/CHEf
Mshindi wa uchaguzi wa urais katika Ufaransa, Nicolas Sarkozy.
Mshindi wa uchaguzi wa urais katika Ufaransa, Nicolas Sarkozy.Picha: AP

Waziri huyo wa zamani wa mambo ya ndani, mwenye umri wa miaka 52, na kiongozi wa Chama tawala cha Ki-Conservative cha UMP mwishoni mwa wiki iliopita alishinda katika duru ya pili ya uchaguzi kwa asilimia 53 ya kura dhidi ya mtetezi wa Chama cha kisoshalisti, Bibi Segolene Royal, aliyejipatia asilimia 47 ya kura. Wafaransa wengi sana walijitokeza kupiga kura, asilimia 86 ya wale walio na haki, hivyo kudhihirisha vipi Wafaransa walivouona uchaguzi huo kuwa muhimu kwa mustakbali wa nchi yao.

Mwenyewe Nicolas Sarkozy, katika tangazo lake baada ya kushinda, alisema hivi:

+Rais wa Jamhuri lazima awapende Wafaransa wote, bila ya kujali maoni yao. Nataka kusema kwamba nitakuwa rais wa Wafaransa wote. Nataka kusema kwamba leo ushindi sio wa Ufaransa dhidi ya mtu mwengine, lakini ni ushindi wa demokrasia na zile thamani zinazotuunganisha pamoja.. Nataka kurejesha mamlaka, uchapaji kazi na heshima. Natoa mwito kwa washirika wetu wa Ulaya, na ninasema kwamba katika maisha yangu yote nimekuwa mkereketwa wa Umoja wa Ulaya na leo Ufaransa imerejea tena katika Ulaya. Nataka kutoa mwito kwa marafiki zetu wa Marekani na kuwaambia kwamba wanaweza kuutegemea urafiki wetu. Ufaransa maisha itakuwa upande wao, wakati wowote wanapotuhitaji. Lakini nataka wakati huo huo kusema kwamba urafiki maana yake ni kukubali kwamba rafiki anaweza kufikiria vingine.+

Mbunge wa hapa Ujerumani wa chama tawala cha CDU, Andreas Schockenhoff, akizungumzia lama siasa ya Ufaransa kuelekea Marekani itabadilika ukilinganisha na ile ya Rais Chirac ya kujivuta kutoka Marekani, hasa kutokana na mzozo wa Iraq:

+Nicolas Sarkozy anautafsiri utambulisho wa Ulaya sio kuwa ni dhidi ya Marekani. Hatakuwa kama Chirac kujaribu kujaribu kuunda mhimili dhidi ya Marekani katika siasa za nje, lakini anauona mustakbali wa Ulaya katika ushirikiano baina ya pande mbili za Bahari ya Atlantik. Na katika hali hiyo ni kwa manufaa ya siasa yetu ya Ulaya.+

Nicolas Sarkozy, ambaye wazee wake ni wahamiaji wa kutokea Hungary, aliishukuru Ufaransa kwa kila kitu iliochompa, na kusema sasa ulikuwa ni wakati kwake kulipa kila kitu ambacho nchi hiyo imemfanyia kwa kuitumikia vilivyo. Bila ya shaka, hili lilikuwa sio tu porojo, lakini uzito wa wadhifa huo mpya na kazi inayomkabili umesababisha ayaseme hayo.

Suala walilokuwa wanajiuliza Wafaransa wengi kabla ya uchaguzi, na hasa vijana, ni nani atakayeweza kuibadilisha Ufaransa, tena kwa kutumia njia gani?

Wananchi wengi walikubaliana kwamba nchi yao ilihitaji mwanzo mpya, baada ya kupita miaka ya uchumi kuzorota na nchi yao kuporomoka kutoka kuwa nchi muhimu duniani. Nicolas Sarkozy alikuwa anajiamini, asiovumilia masihara katika kutekeleza yale anayoamini kuwa ni sawa, na pia mjanja anayejuwa kuyakimbilia wapi madaraka yaliko. Kwa upande mwengine, Bibi Royal anataka marekebisho, lakini yafanyike kwa mkono wa huruma, mtu asiyetaka Ufaransa iwe katika malumbano yasiokwisha. Baada ya kutangazwa kwamba ameshindwa kuwa mwanamke wa kwanza kuiongoza Ufaransa, Segoline Royal aliahidi kwamba mapambano yataendelea, vuguvugu lake la kisiasa halitasimama, na lengo lake ni kuibadilisha jamii na kuupa uhai mpya mrengo wa shoto katika siasa za Ufaransa. Kwanza kabisa jambo hilo linakihusu chama hake cha kisoshalisti ambacho kwa vyovyote kitahitaji kijitazame upya. Kitahitaji, kwa vyovyote, kiangalie namna ya kuzivutia kura za watu walio katika mrengo wa katikati, kama vile alivofanya waziri mkuu wa Uengereza, Tony Blair na chama chake cha Labour zaidi ya miaka kumi iliopita, au Filipe Gonzales na chama chake cha kisoshalisti katika Spain, au hata kujigeuza kuwa kama chama cha Social Democratic, SPD, cha hapa Ujerumani. Kushindwa mara ya tatu kwa Wasoshalisti katika Ufaransa ni jambo linalowalazimu watafakari.

Ilimchukuwa Nicolas Sarkozy hadi mwaka 2002 kutambulika kama kizito katika siasa. Alijulikana kama mtu asiyejali kuzungumzia masuala yanayoleta ubishi na yasiopendwa na watu. Alitunga sheria kali za kuwaadhibu wanaofanya makosa ya usafiri mabarabarani ambayo yanasababisha vifo vya watu wengi. Michafuko ya vijana ya mwaka 2005 katika vitongoji vya miji mikuu ya Ufaransa ulikuwa mtihani mkubwa kwa Nicolas Sarkozy hata ikambidi atangaze hali ya hatari.

Rais mpya atakuwa na mrundo wa mapendekezo ya marekebisho mbele ya meza yake. Ukosefu wa kazi ni mkubwa na uchumi ni dhaifu ukilinganisha na vipimo vya kimataifa. Pengo la wanaojiweza na wasiojiweza katika jamii ya Kifaransa ni kubwa mno na linahitaji kwa upesi kupunguzwa, ama sivyo kuna hatari ya kutokea mizozo ya kijamii mikubwa kuliko ile iliotokea mwaka juzi katika vitongoji vya miji mikubwa. Lakini kuweza kuyatekeleza marekebisho alioahidi, Nicolas Sarkozy anahitaji wingi ulio wazi katika bunge, ambalo uchaguzi wake utafanyika mwezi ujao. Naye atashinda tu uchaguzi huo pindi ataweza kuzivutia kura za walio katika mrengo wa katikati.

Ufaransa na Ujerumani ni nchi mbili ambazo zamani zilikuwa hasimu na baadae kupatana, na jambo hilo limekuwa ndio msingi wa fikra ya kuweko Umoja wa Ulaya na mara nyingi hadharani sura ya siasa ya Ulaya ilionekana sio kupitia rais wa tume ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels, lakini sura pacha za kansela wa Ujerumani na rais wa Ufaransa, kama ni Valery Giscard d’Estiang na Helmut Schmidt au Helmut Kohl na rafiki yake, Francois Mitterand. Kama vile watangulizi wao, Rais Jacques Chirac na Kansela Angela

Merkel wameufanya uhusiano baina ya Ujerumani na Ufaransa kuwa ni urafiki wao wa kibinafsi. Katika ziara yake ya mwisho alioifanya Rais Chirac hapa Ujerumani, kansela Merkel alisema:

+Nataka kutoa ahsante ya kibinafsi kwamba nimeweza kugawana pamoja na wewe uzoefu ambao umenisaidia katika kazi yangu kama kansela wa Ujerumani. Nataka kukumbusha kwamba wewe ulikuw amkuu wa kwanza wa dola au serekali ambaye alihutubia katika jengo jipya la bunge mjini Berlin. Wakati huo ulisema iishi Ufaransa, iishi Ujerumani. Nataka kuengeza uishi urafiki baina ya Ujerumani na Ufaransa.+

Pia katika hotuba yake ya ushindi, Nicolas Sarkozy alielezea malengo yake kwa bara la Afrika:

Insert O-Ton…Nicolas Sarkozy

+Nawatolea mwito Waafrika wote, mwito wa udugu kwa kuliambia Bara la Afrika tunataka kuwasaidia, kuisaidia Afrika katika kupambana na maradhi, kuipiga vita njaa, kuung’oa umaskini, kuishi kwa amani, nataka kuwaambia tutaamua kwa pamoja namna ya kudhibiti wimbi la uhamiaji na sera za maendeleo imara.+

Bila ya kujali ushindi wa Nicolas Sarkozy, uchaguzi huu umedhihirisha ushindi wa demokrasia katika Ufaransa. Nadra Wafaransa waliwahi kushiriki kwa hamasa na vishindo katika mijadala ya kisiasa kama ilivyojiri mara hii. Ule mshtuko walioupata mwaka 2002 umetoweka pale chama cha kizalendo cha mrengo wa shoto cha Jean-Marie Le Pen kilipata ushindi na kuingia katika duru ya pili ya uchaguzi kutokana na kushiriki kwa uchache watu katika uchaguzi . Kwa hivyo Nicolas Sarkozy, kama ilivyo Ufaransa, yuko mbele ya mtihani mkubwa.

Miraji Othman