1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Niger yamchagua Rais wa mpito.

23 Februari 2010

Utawala wa Kijeshi nchini Niger ambao ulifanya mapinduzi ya kijeshi nchini humo wiki iliyopita, sasa umemchagua Kiongozi wao Meja Salou Djibo,kuwa Rais wa mpito

https://p.dw.com/p/M8ov
Wananchi wa Niger washerehekea mapinduzi ya kijeshi.Picha: AP

Utawala huo pia ulizindua mpango wa kupatikana kwa katiba mpya itakayopigiwa kura ya maoni. Meja Salou Djibo, anaongoza baraza la kijeshi lililomwangusha Rais Mamadou Tandja, liitwalo Supreme Council for Restoration of Democracy, (CRSD) .

Taarifa hiyo iliyotolewa jana katika redio ilisema CRSD ndio afisi yenye mamlaka yote makuu nchini Niger na itasimamia sera zote nchini humo, na Kiongozi wake ndie sasa takuwa Rais wa mpito wa Niger.

Niger Demosntration für den Militärputsch Flash-Galerie
Raia nchini Niger washerehekea kuangushwa kwa Mamadou Tandja.Picha: AP

Na rais huyo atakuwa na mamlaka yote anayepaswa kuwa nayo Kiongozi wa nchi na vile vile Kiongozi wa Serikali. Taarifa hiyo iliendelea kusema mpangilio huo wa mamlaka utadumu tu katika kipindi hicho cha mpito, lakini taarifa hiyo ilikuwa kimya kuhusiana muda ambao serikali hiyo ya mpito itakuwepo mamlakani.

Meja Salou Djibo, katika nafasi yake kama Kiongozi wa utawala huo wa kijeshi- ndie sasa anakuwa rais wa mpito wa Niger. Utawala huo wa kijeshi pia uliahidi kuunda bodi itakayosimamia sheria mpya za uchaguzi pamoja na mswada wa katiba mpya, ambao utawasilishwa kwa wananchi kuupigia kura ya maoni.

Tangazo hili kutoka mji mkuu wa Niamey linakuja wakati Marekani imeongeza sauti yake ya Niger kurejea katika utawala wa kiraia haraka iwezekanavyo. Lakini utawala huo wa kijeshi haujakosa watetezi- Mamia ya raia nchini Niger kutoka katika mji wa Rais aliyepinduliwa walimiminika majiani kusherehekea kuondolewa madarakani kwa Rais Mamadou Tandja.

Mwishoni mwa wiki Viongozi hao wa kijeshi walikutana kwa majadiliano na wajumbe mbali mbali kutoka Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika pamoja na wajumbe kutoka Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Magharibi mwa Afrika ECOWAS kuzungumzia hali nchini Niger. Kiongozi wa ECOWAS Mohammed Ibn Chambas alisema viongozi hao wa kijeshi waliwaondolewa wasiwasi kwa kuwahakikishia wataachana na madaraka punde tu wanasiasa watakapokubaliana na suala la katiba mpya.

Niger / Tandja / Putsch
Rais Mamadou Tandja alipinduliwa Alhamisi.Picha: AP

Hata hivyo hadi sasa viongozi hao wa kijeshi hawajasema bayana ni lini wataachana na madaraka. Alhamisi wiki iliyopita, wanajeshi waliuvamia mkutano wa baraza la mawaziri katika Ikulu ya Rais na kumkamata Rais Tandja pamoja na mawaziri wake. Muda mfupi baadaye wakaivunjilia mbali serikali na kusimamisha katiba ya nchi hiyo, ambayo Rais Tandja alikuwa ameibadili ili imruhusu kuongeza muda wake madarakani zaidi ya mihula miwili ya miaka mitano kama ilivyotakikana.

Chini ya mpangilio huu mpya- Kamati ya Katiba pamoja na Mahakama zitaundwa ili kuchukua mahala pa Mahakama ya Kaziba na Mahakama kuu zilizovunjiliwa mbali baada ya mapinduzi hayo ya kijeshi. Rais wa mpito atakuwa na madaraka ya kuwateua mawaziri, na pia kuwafuta kazi, ikiwemo Waziri Mkuu.

Niger, ambayo ipo katika eneo la Magharibi mwa Afrika lenye uzoefu wa mizozo, iimekuwa na utulivu wa kiasi cha mwongo mmoja. Lakini iliingia katika mzozo mwaka uliopita pale Rais Tandja alipoaumua kuongeza muda wake madarakani kinyume ana katiba ilivyomruhusu.

Mwandishi: Munira Muhammad/ AFPE

Mhariri: Aboubakary Liongo.