1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria yadai imefikia makubaliano na Boko Haram

18 Oktoba 2014

Maafisa na wanaharakati wanaofanya kampeni wamesubiri kwa shauku kubwa leo Jumamosi kupata taarifa zaidi juu ya hatima ya zaidi ya wasichana wa shule 200 waliotekwa nyara.

https://p.dw.com/p/1DY0k
Boko Haram will Mädchen freilassen
Wanaharakati wa Turejesheeni wasichana wetu nchini NigeriaPicha: AFP/Getty Images/P. Utomi Ekpei

Serikali ya Nigeria imedai kuwa imefikia makubaliano na kundi la Boko Haram kuweza kuwaachia wasichana waliotekwa nyara tangu Aprili mwaka huu.

Mkuu wa jeshi la Nigeria Air Marshal Alex Badeh amewaambia maafisa waandamizi wa jeshi kutoka Nigeria na Cameroon wanaokutana mjini Abuja siku ya Ijumaa kwamba " makubaliano ya kusitisha mapigano" yamekamilika kati ya serikali na wapiganaji hao.

Nigeria Flüchtlinge in Maiduguri
Wakimbizi katika mji wa MaiduguriPicha: picture alliance/AP Photo

"Nimewaelekeza viongozi wa majeshi kuhakikisha utekelezaji mara moja wa hatua hizi," ameongeza.

Tangazo hilo la Badeh limekuja baada ya msaidizi mwandamizi wa rais Goodluck Jonathan , Hassan Tukur, kuliambia shirika la habari la AFP kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano yamefikiwa kufuatia mazungumzo, pamoja na kuachiliwa kwa wasichana 219 wanaoshikiliwa mateka tangu mwezi Aprili.

Madai ya serikali yatia wasiwasi

Lakini vigezo vya serikali vilivyopita na madai ya jeshi juu ya kumalizika kwa mapigano yaliyosababisha maafa makubwa katika mzozo wa muda wa miaka mitano na hatima ya wasichana ambao hawajulikani waliko imewaacha wadadisi wengi wakichukua tahadhari.

Angriff von Boko Haram im nordöstlichen Stadt Konduga nahe Maiduguri / Nigeria
Wanajeshi wa Nigeria wanaopambana na Boko HaramPicha: dpa

Jonathan anatarajiwa kutangaza nia yake ya kutaka kuchaguliwa tena katika wiki za hivi karibuni , na taarifa njema kama hizo juu ya mateka hao na ghasia zinaweza kumpatia msukumo mkubwa kisiasa.

Shehu Sani, mtaalamu kuhusu Boko Haram ambaye amefanya majadiliano na kundi hilo kwa niaba ya serikali amesema "hamjasikia" Danladi Ahmadu , ambaye Tukur amedai anawakilisha wapiganaji hao katika mazungumzo.

Ralph Bello-Fadile mshauri wa mshauri wa usalama wa taifa nchini Nigeria (NSA), amesema NSA imekabiliwa na walaghai wakidai kumuwakilisha kiongozi wa kundi la Boko Haram Abubakar Shekau.

"Serikali inataka majadiliano lakini hadi sasa hakuna mtu ambaye amefika anayezungumza kwa niaba ya Shekau," ameuambia mkutano wa Catham House mjini Abuja siku ya Jumatatu.

Msemaji wa usalama wa serikali ya Nigeria binafsi , Mike Omeri , pia amesema kuwa hakuna makubalino yaliyofikiwa hadi sasa kuhusiana na kuachiliwa kwa wasichana hao.

Nigeria Protest Boko Haram Entführung 26.5.2014
Maandamano ya kudai wasichana warejeshwe nyumbaniPicha: picture-alliance/AP Photo

Marekani haiwezi kuthibitisha

Marekani imesema haiwezi kuthibitisha iwapo makubaliano hayo yamefanyika.

Nigeria Boko Haram Abubakar Shekau Archiv
Kiongozi wa kundi la Boko Haram Abubakar shekauPicha: picture alliance/AP Photo

"Kwa hakika , tungekaribisha kumalizika kwa matumizi ya nguvu, kurejea kwa usalama na , nafikiri ni dhahiri , tungekaribisha kuachiliwa huru kwa wasichana ambao wamepotea kwa muda mrefu sana. Lakini hatuwezi kuthibitisha kwa njia huru kuhusu hilo katika wakati huu.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande siku ya Ijumaa amekaribisha tangazo hilo la kupatikana makubaliano kuhusiana na wasichana hao kuwa ni "habari nzuri". Amesema katika mkutano na waandishi habari mjini Paris kuwa "tuna taarifa ambazo zinaturuhusu kufikiri kwamba , kuachiliwa kwa wasichana hao kunaweza kutokea katika saa chache zijazo ama siku". Hakutoa maelezo zaidi.

Boko Haram Video 12.5.2014
Wasichana waliotekwa na Boko HaramPicha: picture alliance/abaca

Wakati huo huo Cameroon imesema siku ya Ijumaa kuwa jeshi lake limewauwa wapiganaji 107 wa Boko Haram, wakati afisa wa polisi ameliambia shirika la habari la AFP kuwa kiasi ya raia 30 wameuwawa na kundi hilo la wanamgambo kabla ya kushambuliwa kwa kushitukiza.

Mapigano hayo yalitokea siku ya Jumatano na Alhamis baada ya wanamgambo kutoka kundi la Boko Haram kupita katika miji ya mpakani ya Amchide na limani, wizara ya ulinzi ya Cameroon imesema katika taarifa iliyosomwa katika radio ya taifa.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Amina Abubakar