1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Njaa Kenya hata kwa wa tabaka la kati

Zainab Aziz
16 Oktoba 2017

Upungufu wa chakula nchini Kenya sasa unazigusa hata familia za tabaka la kati, ambapo bei za vyakula zimepanda kwa zaidi ya 100% na wengi hawalalamiki juu ya ukame tu, bali pia sera za serikali.

https://p.dw.com/p/2lZix
Hunger Dürre Kinder Afrika
Picha: picture-alliance/dpa/S. Morrison

Katika siku mojawapo, wingu jeusi linazidi kutanda juu ya shamba la Kisilu Musaya. Lakini mkulima huyo anajua maana ya wingu hilo. Kwa mara nyingine, halitaleta  mvua inayotarajiwa.

Misimu mitatu ya mvua imepita bila ya mvua kunyesha kusini mwa Kenya, ambako ni nyumbani kwa Kisilu Musaya na mkewe, Christine. Mikunde michache tu bado imechipua lakini mahindi yote ya Musaya, chanzo chake kikuu cha mapato, yamekauka. 

"Hapo awali nilikuwa akiba ya kutosha kwa ajili ya kuilisha familia yangu kwa angalau kwa miezi miwili hadi mitatu. Lakini sasa ninachokivuna hakitoshi hata kwa wiki moja," anasikitika mkulima huyu.

Kwa miaka saba, Musaya amekuwa anashiriki katika mradi wa filamu: anaorodhesha taarifa juu ya mabadiliko ya hali ya hewa katika mkoa wake. Ameziona athari nyingi ya mabadiliko ya tabia nchi: ukame na mafuriko. Lakini hali mbaya kama ya sasa, haijawahi kuonekana.

Badala ya kuwa na uwezo wa kuuza mavuno yake, Musaya anapaswa kuyauza mahindi yake sokoni yaani chakula cha msingi cha Wakenya wengi. Lakini kiwango anachoweza kukimudu kinazidi kuwa kidogo na anaamini kuwa serikali imeshindwa kumkwamua.

"Mimi kama mkulima nahisi kuwa nimesahauliwa. Najitahidi kila siku ili kuweza kuilisha familia yangu, lakini serikali haitusaidii hata kidogo," anasema.

Mgogoro wa unga wa mahindi

Simbabwe Dürre Mais Landwirtschaft
Kilimo cha mahindi kimeathirika kwa ukosefu wa mvua na maradhi.Picha: Getty Images/AFP/A. Joe

Hata katika mji mkuu Nairobi, unaofahamika kama "mgogoro wa unga wa mahindi" umekuwa na unasababisha mvutano mkubwa wa kisiasa kwa miezi kadhaa sasa.

Bei ya unga wa mahindi imepanda kwa zaidi ya  asilimia 100 mnamo siku za karibuni. Sababu ni kwamba maghala yaliyokuwa yamejaa mahindi ya akiba yalikauka muda mfupi tu baada ya ukame kuanza.

Je, mahindi hayo yalioza au yaliibiwa? Wahusika bado hawajatoa maelezo hadi leo. Lakini hatimaye serikali ilichukua hatua ya kuagiza mahindi na kuanzisha mpango wa ruzuku ili kuiteremsha bei ya unga wa mahindi.

Mchambuzi wa masuala ya fedha, Ali Sachu wa Shirika la Usimamizi wa Mali, anasema mfumo wote ni wa ufisadi mtupu.

"Watu wenye leseni kwa sasa wanachuma faida kubwa sana na watu wengine nchini kote wanabeba mzigo wa kulipa. Na watu wengine wanaamini kwamba kiasi fulani cha faida kinakwenda kwa wanasiasa," anasema mchambuzi huyo.

Matumaini yaliyopotea yanarejea

Mkulima Kisilu Musaya ameacha siku nyingi sasa kuweka matumaini ya msaada kutoka serikalini. Badala yake  yeye pamoja na wakulima wenzake wadogo wadogo wanakusudia kujenga mfumo wa umwagiliaji kwenye mashamba yao.

Lakini mtambo huo bado haujaanza kufanya kazi kama ilivyotarajiwa.

Hata hivyo, nyanya zimeanza kustawi. Kutokana na hali hiyo wakulima hao wanaweza kuwa na matumaini ya kuvuna mahindi yao katika msimu ujao.

Mwandishi: Sella Oneko/Jan  Philipp
Tafsiri: Zainab Aziz
Mhariri: Mohammed Khelef