1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Njama ya kumuua Obama yazimwa.

28 Oktoba 2008

Polisi nchini Marekani imezima njama ya kumuua seneta Obama na kuzusha bahari ya damu.

https://p.dw.com/p/Fihe

Wiki moja kabla ya uchaguzi wa urais nchini Marekani ijumaane ijayo,idara za usalama za Marekani, zimezima jaribio la kutaka kumuua seneta Barack Obama, mtetezi wa wadhifa wa kiti cha urais kwa chama cha democrat.Vijana wawili wametiwa nguvuni huko Tennessee ambao kwanza walipanga kuzusha bahari ya damu kwa kuua wamarekani weusi kadhaa na mwishoe, kumpiga risasi seneta Obama.

Polisi ilisimamisha gari la vijana hao 2 wenye umri kati ya miaka 18 na 20 mjini Alamo,katika jimbo la tennessee wakati wa ukaguzi wao wa kawaida.Katika sehemu ya nyuma ya mizigo ya gari lao,waligundua silaha nyingi zilizofichwa-hii ni kwa muujibu vile kituo cha TV cha CNN kilivyoarifu."Walikuwa na aina mbali mbali ya bunduki walizozificha ndani ya motokaa yao."

Vijana hao 2 vipara au "skinheads" walitoa kielezo kwa polisi-kwamba walipanga kulivamia duka la silaha na kwiba kwa azma ya kujiandaa barabara. CNN ikaripoti,

"Kwa silaha hizi, wakitaka kuivamia shule moja ambayo wanasoma vijana wengi wamarekani weusi na kuwaua na kuzusha bahari ya damu.Kwa muujibu wa mpango wa vijana hao 2,walipanga kuwahilikisha wanafunzi 102 kwa kuwapiga risasi.Binafsi vijana hao wanajiita "wabaguzi wa weupe".

Baadae walipanga wakiondoka hapo kufunga safari haraka kama iwezekanavyo kuhudhuria mkutano wa hadhara wa seneta Obama na kutoka dirisha la motokaa yao kumfyatulia risasi."

CNN imeripoti .

Kumuua mtetezi huyu -mmarekani-mweusi wa kiti cha urais Barack Obama kwa muujibu walivyosema vijana hao 2 wenye siasa kali za mrengo wa kulia kuwe kilele cha kampeni dhidi ya Muamerika-mweusi huyo.

"Vipara hao 2 ambao walijuana kupitia mtandao wa Internet,ni watu waliojitoa mhanga na walikwisha jitolea binafsi kufa katika njama yao ya kumuua seneta Obama. "

Vijana hao 2 watafunguliwa mashtaka kadhaa kwanza kwa kumiliki silaha zisizosajiliwa ,kuandaa njama ya kwiba silaha na pia kupanga njama ya kutaka kumuua mtetezi wa wadhifa wa urais wa Marekani.Watafikishwa kwa mara ya pili hapo alhamisi mbele ya hakimu.

Hofu za kuuliwa kwa mtetzezi wa kwanza kabisa wa mweusi kwa cheo cha urais, ni kubwa mno nchini Marekani.Ukumbusho wa mauaji ya Dr.Martin Luther King na kuuliwa kwa rais John F.Kennedy na nduguye Robert Kennedy,haukushaulika.Barack Obama ambae kwa wafuasi wake mara nyingi huitwa "Kenney mweusi" kila anapohutubia hadharani, analindwa mno kupita mtetezi yeyote wa wadhifa huu kabla yake.