1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Norway yaitisha mkutano kuichangia Sudan Kusini

Maja Braun20 Mei 2014

Wafadhili wa kimataifa wanakutana Jumanne hii mjini Oslo, Norway kukusanya dola za Marekani bilioni 1.26 ili kugharimia chakula na afya katika nchi ya Sudan Kusini inayokabiliwa na mgogoro, katika kipindi cha mwaka ujao.

https://p.dw.com/p/1C2yC
Sudanesische Flüchtlinge in Äthopien
Picha: DW/C. Wanjoyi

Maelfu wameuawa na milioni 1.2 wameyakimbia makaazi yao tangu kuibuka kwa mapigano katikati mwa mwezi Desemba, kati ya wanajeshi watiifu kwa rais Salva Kiir na makamu wake wa zamani Riek Machar.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu shughuli za kibinaadamu imesema karibu watu milioni 4.9 walikadiriwa kuhitaji msaada wa kiutu nchini Sudan Kusini. Na idadi hiyo ilitarajiwa kuongezeka kwa sababu raia hawajaweza kupanda mazao kutokana na kuendelea kwa mapigano na ukosefu wa usalama, na kuna hatari ya nchi hiyo kukumbw ana baa la njaa.

Wakimbizi wa Sudan Kusini wakigawana chakula katika kambi ya gambella nchini Ethiopia.
Wakimbizi wa Sudan Kusini wakigawana chakula katika kambi ya gambella nchini Ethiopia.Picha: DW/Coletta Wanjoyi

Hali inazidi kutisha

Mkuu wa shughuli za kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa Valeria Amos na waziri wa mambo ya kigeni wa Norway Borge Brende walisema katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa mkutano wa leo, kuwa karibu watu milioni moja huenda wakakabiliwa na njaa, ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa. Zaidi ya serikali 40 na mashirika 50 yalialikwa katika mkutano huo wa mjini Oslo.

Umoja wa Mataifa ulijiwekea lengo la kukusanya kiasi cha dola bilioni 1.8, lakini hadi sasa wafadhili walikuwa wamechangia dola milioni 536. Kama mwenyeji wa mkutano wa leo na moja wa wafadhili wakubwa wa Sudan Kusini pamoja na Marekani na Uingereza, Norway, ambayo hapo awali ilikuwa imeahidi kutoa dola milioni 17, ilitangaza kuongeza kiasi kingine cha dola milioni 63, na waziri wa mambo ya kigeni Brende alisema hatua hiyo ni ujumbe wa kiasi gani hali ilivyo ya kutisha nchini Sudan Kusini.

Ikulu ya Marekani ilitangaza jana kuwa serikali imeruhusu matumizi ya dola milioni 50 kutoka mfuko wake wa dharura wa wakimbizi kusaidia mahitaji ya haraka ya kiutu. Kiasi hicho kitalisaidia shirika la kushughulikia wakimbizi UNHCR na washirika wake kusaidia wakimbizi zaidi ya 300,000 waliovuka mpaka na kuingia nchi za Ethiopia, Kenya, Sudan na Uganda, na pia wakimbizi wa ndani.

White ilisema milioni hizo 50 ni sehemu ya msaada wa ziada wa dola milioni 300 ambazo Marekani itaahidi kutoa katika mkutano wa leo. Hii inafanya jumla ya msaada wa Marekani kufikia dola milioni 434 tangu mgogoro huo ulipoibuka mwezi Desemba.

Wakimbizi wa ndani waliotoroka mjini Bor wakiwa katika kambi ya Mingkam.
Wakimbizi wa ndani waliotoroka mjini Bor wakiwa katika kambi ya Mingkam.Picha: Reuters/Kate Holt/UNICEF

Kwa upande wake, Uingereza imeahidi kutoka pauni milioni 60, ambazo ni sawa na dola za Marekani milioni 100.97. Ufadhili huu mpya unafikisha msaada wa Uingereza kwa pauni milioni 93 tangu kuibuka kwa mgogoro wa Sudan Sudan.

Mapigano yaendelea

Mgogoro kati ya watu wa kabila la rais Salva Kiir la Dinka, na Nuer lake Riek Machar, umesababisha mgogoro wa kibinaadamu katika taifa hilo changa kabisaa duniani. Mapigano pia yamezuwia uchimbaji wa mafuta, ambayo ndiyo chanzo kikuu cha mapato ya serikali ya nchi hiyo.

Pande zinazohasimiana zilisaini makubaliano ya pili ya kusitisha mapigano nchini Ethiopia karibu wiki mbili zilizopita, lakini makubaliano hayo yalianza kuvunjwa baada ya siku tatu, kwa pande hizo kupigana tena, huku kila upande ukiulaumu mwingine kwa kuvunja makubaliano.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/Schadomsky/rtre,dpae.
Mhariri: Saum Yusuf