1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Noti za kuupiga jeki uchumi

Oumilkher Hamidou4 Desemba 2008

Serikali kuu ya Ujerumani yapanga kugawa fedha miongoni mwa raia ili kuinua shughuli za kiuchumi

https://p.dw.com/p/G97T
Waziri wa fedha wa serikali kuu ya Ujerumani Peer Steinbrück wa chama cha SPDPicha: AP



Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha zaidi na mipango ya serikali kuu ya kuupiga jeki uchumi wa Ujerumani,maridhiano yaliyofikiwa na vyama ndugu vya CDU/CSU pamoja na chama cha SPD kuhusiana na sheria za idara ya upelelezi ya Bundeskriminalamt-BKA na makubaliano yanayopiga marufuku mabomu ya mtawanyo.


Tuanze lakini na alifu:Linapohusika suala la kukabiliana na mzozo mkubwa wa kibepari,kugawa hundi sio njia pekee ya busara, linaandika gazeti la WEST ALLGEMEINE ZEITUNG la mjini Essen na kuendelea:



Motisha ya kununua vitu itakayosababíshwa na hundi hizo,itainua japo kwa muda shughuli za kibiashara-hapa tusijaribu kudharau kishindo cha kisaikolojia kitakachowateremsha watu madukani.Katika mzozo huu wa sasa kuna jambo moja ambalo ni dhahiri,nalo ni kwamba hofu zimewafanya wajerumani kutunza fedha zao-wanaweka akiba,ili waweze kukabiliana vyema na mitihani inayokuja.Kwa kufanya hivyo lakini wanazidisha makali ya mzozo wa kiuchumi."



Gazeti la LÜBECKER NACHRICHTEN linasifu pendekezo la chama cha Social Democratic-SPD na kuandika:



Kuwapatia raia noti ni njia bora ya kupunguza kodi.Kwasababu zinalenga pale pale palipokusudiwa:Pesa hizo zinatumiwa kununua vitu-hazimalizikii katika akaunti za akiba.Hoja ya pili ya maana ya noti hizo ni kwamba zitawasaidia mamilioni  ya wananchi ambao kutokana na mishahara yao duni,wanalipa kidogo tuu kodi za mapato au hawamudu kabisa kulipa.Kwa hivyo hawafaidiki sana au hata chembe na hatua za kupunguza viwango vya kodi za mapato.Tuchukue mfano mmoja tuu hapa nao ni ule wa waastaafu milioni 18 wa Ujerumani.



 Gazeti la mjini Bonn, GENERAL ANZEIGER lina maoni mengine kabisa.Na linaandika:



Yuro mia tano kwa kila mtu-inamaanisha kitita jumla  cha yuro bilioni 40.Kitatolewa kwa mkumbo mmoja.Zawadi ya X-Mas kutoka serikalini.Hawamudu lakini kufanya hivyo.Na wakijaribu,basi watabidi wawekeze kwengineko:Katika mpango uliofikiriwa muda mrefu-wa mageuzi ya kodi ya mapato.Sio kufumba na kufumbua-hasha-mjadala huu hauambatani na ukweli wa mambo.



Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamezungumzia pia makubaliano yaliyofikiwa jana mjini Oslo-Norway yanayopiga marufuku mabomu ya mtawanyo.Gazeti la MÄRKISCHE ODERZEITUNG la mjini Frankfurt/Oder linasifu makubaliano hayso na kuandika:



"Ikiwa nchi zaidi ya 100 zitapiga marufuku silaha hizo hatari,basi hizo zitakua habari za kutia moyo.Lakini watengenezaji wakubwa na ambao ndio wanaopenda vzaidi kuyatumia mabomu hayo,yaani Marekani,Urusi,China,India,Pakistan na Israel  wanapinga bado kuachana nayo.Kilichodhihirika ni kwamba mabomu hayo ya mtawanyo hayana faida yoyote kubwa kijeshi.Badala yake raia laki moja ama wameuwawa au kujeruhiwa kutokana na kuporomoshwa mabomu hayo yanayotawanyika.Wakati kwa hivyo umewadia kwa silaha hizo kutoweka.Makubaliano yaliyotiwa saini mjini Oslo yatasaidia kwa hivyo kuzidi kuwashinikiza wale wasiotaka kusikia.