1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nusu fainali ya Champions League:Hatimaye Schalke yatolewa rasmi na MANU

5 Mei 2011

Manchester United imefanikiwa kuingia fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya baada ya kuichabanga Schalke 04 ya Ujerumani mabao 4-1 na hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 6-1.

https://p.dw.com/p/119DP
Kikosi cha Schalke mazoezi kabla ya pambanoPicha: AP

Hiyo ni mara ya tatu kwa United kuingia fainali ndani ya kipindi cha misimu minne, na sasa itakumbana na Barcelona katika fainali itakayofanyika kwenye uwanja wa Wembley mjini London tarehe 28 mwezi huu.

Barcelona walifuzu baada ya kuwatoa mahasimu wao huko huko Uhispania Real Madrid.

Manchester United iliteremsha karibu kikosi cha pili, kwa kuwapumzisha wachezaji wake tisa kwa ajili ya pambano lao la Jumapili katika ligi kuu ya Uingereza dhidi ya Chelsea.

Hata hivyo kikosi hicho kilichoingia uwanjani Old Trafford kiliweza kutoa kipigo hicho ambacho ni kikubwa kuwahi kutokea katika nusufainali ya michuano hiyo ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Kocha wa Schalke Ralf Rangnick alisema kuwa timu yake ilistahili kipigo hicho na kuongeza kuwa ni lazima aipongeze United kwani ilionesha soka zuri katika mechi zote mbili na kwamba walipofungwa tu basi ilikuwa ngumu sana kwao.

Rangnick amesema kikosi cha pili cha United ilichokumbana nacho, kiwango chake cha soka ni cha juu sana, huku akiwanyooshea zaidi kidole Barbatov na Anderson kuwa ni aina ya wachezaji ambao kila timu katika ligi ya Ujerumani Bundesliga ingependa kuwa nao.

Naye mlinda mlango wa timu hiyo ambaye katika mechi ya kwanza alidhihirisha ujogoo wake katika milingoti mitatu, Manuel Neuer alisema.

´´Kila timu ingependa kufikia tena katika nusufainali.Tumepoteza nafasi katika mecho zote mbili.Ilikuwa ni lazima kila mchezaji aoneshe kiwango cha juu cha kandanda katika mechi zote mbili.Na kwa sababu kiwango cha uchezaji hakikuwa cha kutosha ni vigumu kuweza kufuzu mbele ya Manchester United´´

Golikipa wa United Edwin van der Sar alisema kuwa sasa ni wakati wa kujifunza zaidi makosa waliyoyafanya katika mechi zilizopita walipokumbana na Barcelona kabla ya mpambano wao huo wa fainali.

Mwaka 2009 Barcelona iliwatoa Manchester United katika fainali ya michuano hiyo mjini Roma kwa mabao 2-0.

Naye Kocha wa Manchester United Alex Ferguson akizungumzia mpambano wa fainali tarehe 28 kati yao na Barcelona alisema anategemea itakuwa fainali ya kusisimua kabisa.Timu hizo mbili zitakuwa zikiwania kutwaa ubingwa wa Ulaya kwa mara nne.

Amesema michuanao ya ligi ya mabingwa barani Ulaya ni michuano mikubwa kabisa duniani kwani timu zote bora hushiriki, na kufika fainali hayo peke yake ni mafanikio, lakini kushinda ubingwa ni mafanikio makubwa zaidi.

Mwandishi. Aboubakary Liongo/ Reuters/AFP

Mhariri: Abdul-Rahman