1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nyama ya mbwa na paka ni biashara kubwa Indonesia

Iddi Ssessanga
21 Mei 2018

Nyota wa kimataifa wa uigizaji, muziki na michezo wamemuhimiza rais wa Indonesia kupiga marufuku kile wanachosema ni biashara ya kikatili ya nyama ya mbwa na paka kwa ajili ya ulaji wa binadamu.

https://p.dw.com/p/2y4X7
Demo gegen Dog-Meat-Festival
Picha: Picture alliance/NurPhoto/R. Tivony

Wito huo unakuja baada ya wanaharakati wa kupinga ukatili dhidi ya wanyama nchini Indonesia na shirika la Humane Society International kutaja masoko kwenye kisiwa cha Sulawesi ambako mbwa walikuwa wakipigwa kwa rungu na kuchomwa wakiwa hai ili kuondoa nywele zao  mbele ya watazamaji, wakiwemo watoto.

Barua yao kwa Rais Joko "Jokowi" Widodo iliyochapishwa siku ya Jumatatu imesema ikiwa Indoneisa itajiunga na mataifa mengine ya Asia ambayo yamepiga marufuku biashara hiyo ya kikatili, hatua hiyo "itasherehelewa kimataifa" na kuondoa doa kwenye sifa ya taifa hilo.

Muungano huo wa wapiga kampeni unaojiita "Indonesia Isiyo na Nyama ya Mbwa" pia umeonya juu ya hatari za kiafya zinazoweka kutokana na uwezekano wa kusambaa kwa ugonja wa kichaa cha mbwa.

"Wanyama hawa, wengi wao wakiwa waliibwa, wanateswa kwa kutumia mbinu za kienyeji za utekaji, usafirishaji na uchinjaji, na mateso makubwa na hofu wanavyopitia vinavunja moyo na kutisha," ilisema baru hiyo.

Indonesien Hundefleisch wird als Nahrung verwendet
Mbwa wakiwa wamefungwa kabla ya kuchinjwa katika bucha ya nyama ya mbwa katika eneo la Yogyakarta nchini Indonesia.Picha: Getty Images/U. Ifansasti

Muigizaji Cameron Diaz, muongozaji wa kipindi cha Televisheni Ellen DeGeneres, muibuaji vipaji Simon Cowell, Mchekeshaji Ricky Gervais, muimbaji wa pop wa Indonesia Anggun na mwanamuziki Moby ni miongoni mwa zaidi ya nyota 90 walioorodheshwa kwenye barua hiyo.

Nyama ya mbwa inaliwa na asilimia ndogo tu ya Waindonesia, lakini katika taifa la wakaazi milioni 250 bado inawakilisha biashara kubwa. Malefu ya mbwa na paka huchinjwa kila wiki katika kaskazini mwa Sulawesi, wengi wao wakiwa wameingizwa kutoka mikoa mingine nchini Indonesia, kwa mujibu wa makundi ya kupinga ukatili dhidi ya wanyama.

Baada ya wimbi la ukosoaji mwezi Januari, soko maarufu la Tomohon lililoko kaskazini mwa Sulawesi, lilisitisha uchinjaji wa wazi wa mbwa, lakini mkanda wa vidio uliochukuliwa na wanaharakati ulionyesha mizoga ya mbwa ilikuwa bado inaletwa kutoka maeneo mengine.

"Tunamsihi rais Widodo kushirikiana nasi kutafuta suluhisho lilalolinda siyo tu mbwawa Indonesia, lakini pia afya waru wake," alisema Rais wa shirika la Humane International Kitty Block katika taarifa.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape

Mhariri: Mohammed Khelef