1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama aacha gumzo Berlin

Admin.WagnerD20 Juni 2013

Akikumbushia historia kali ya mji wa Berlin uliyogawika wakati mmoja, rais Barack Obama amezitahadharisha Marekani na Ulaya dhidi ya kuridhika kunakosababishwa na amani, huku akiapa kupunguza silaha za nyuklia.

https://p.dw.com/p/18tGy
Obama na mkewe Michele wakiaga kabla ya kuondoa kurudu Marekani.
Obama na mkewe Michele wakiaga kabla ya kuondoa kurudu Marekani.Picha: Reuters

Rais Obama pia alitangaza kuwa programu yake ya udukuzi wa mawasiliano iliyozua zogo duniani, imenusuru maisha katika pande zote za Atlantiki. Akihutubia umati uliokusanyika katika lango kuu la Brandenburg, Obama alisema ipo haja ya kupunguza kwa sana tu, silaha za nyuklia za Marekani na Urusi, ili kuondoka katika hali ya kivita inayoendelea kuchochea kutoaminiana baina ya serikali za mataifa hayo.

Rais Barack Obama na Meya wa Berlin Claus Wowereit wakimsikiliza Kansela Angela Merkel.
Rais Barack Obama na Meya wa Berlin Claus Wowereit wakimsikiliza Kansela Angela Merkel.Picha: Odd Andersen/AFP/Getty Images

"Tunaweza tusiishi katika hofu ya maangamizi ya nyuklia, lakini maadam silaha za nyuklia bado zinaendelea kuwepo, hatuna usalama wa kweli," alisema Obama wakati akihitimisha ziara ya siku tatu barani Ulaya, ambayo ndiyo ya kwanza tangu aliposhinda muhula wa pili.

Jinamizi la udukuzi wa mawasiliano lamfuata Berlin

Obama anakabiliwa na migogoro ya ndani pamoja na changamoto za sera ya kigeni, ambavyo vinamvurugia malengo yake ya muhula wa pili. Masuala mawili - vita vikali vinavyoendelea nchini Syria, na program ya udukuzi wa mawasiliano - vilimzonga Obama wakati wa ziara yake nchini Ujerumani, na vile vile katika mkutano wa kundi la mataifa nane yalioendelea kiviwanda, G8 mjini Belfast, Ireland ya Kaskazini mapema wiki hii.

Ujerumani, nchi inayolinda sana faragha, ilitaka hasa majibu kutoka kwa Obama kuhusiana na Programu hiyo inayoendeshwa na shirika la usalama wa taifa la Marekani NSA. Kansela Angela Merkel, alitumia mkutano wake na Obama kwa waandishi wa habari, kutaka kuwepo na uangalifu, katika kutathmini wasiwasi kuhusu faragha, inagwa aliepuka kukwaruzana hadharani na rais.

"Kunahitajika kuwepo uwiano, haya ni mapambano ambayo yataendelea," alisema Merkel. Obama alitoa utetezi mrefu wa programu hiyo iliyoidhinishwa na mahakama, akiielezea kama juhudi makhsusi ambayo imesaidia kunusuru maisha. "Tunafahamu kuhusu mashambulizi yasiyopungua 50 ya kigaidi yaliyozuiwa kwa kutumia taarifa hizi, si tu nchini Marekani, bali pia katika maeneo mengine kama hapa Ujerumani."

Rais Obama akiwahutubia wakaazi wa Berlin, Juni 19.2013.
Rais Obama akiwahutubia wakaazi wa Berlin, Juni 19.2013.Picha: Odd Andersen/AFP/Getty Images

Tukio kuu la ziara ya Obama lilikuwa hotuba ya mchana katika lango la Brandenburg, ambako kulikuwa na ukuta wa Berlin uliyougawa mji huo kati ya mashariki na magharibi. Obama, aliesimama nyuma ya kidirisha cha bilauri isiyopita risasi, alizungumza kutoka upande wa mashariki wa lango hilo, eneo ambalo enzi hizo haikuwa rahisi kwa rais wa Marekani kukanyaga.

Alinganishwa na Kennedy

Hotuba ya raia Obama ililinganishwa na ile maarufu ya John F. Kennedy ya "Ich bin ein Berliner" (Mimi ni mkaazi wa Berlin), aliyoitoa miaka 50 iliyopita, na vile vile mapokezi ya kihitoria aliyoyapata Obama mwenyewe alipowasili mjini humo akiwa mgombea wa urais mwaka 2008. Zaidi ya watu 200,000 walifurika katika eneo la karibu na uwanja huo kusikiliza hotuba hiyo, iliyoakisi matarajio makubwa waliokuwa nayo raia wa Ulaya kwa mwanasiasa chipukizi wa Marekani.

Wakati huu akiwa katika mwaka wake wa tano kama rais, Obama bado anaendelea maarufu barani Ulaya. Lakini umati uliokusanyika kumsikiliza siku ya Jumatano ulikuwa mdogo sana ikilinganishwa na mwaka 2008. Hotuba yake iligusia masuala kadhaa yanayotoa changamoto kwa dunia, ambapo alitoa wito kwa mataifa ya magharibi kuwasha upya mzuka uliyoonyesha na Berlin wakati ambapo raia wengi walikuwa wakipambana kuunganisha tena mji huo wakati wa vita baridi.

Rais Obama na mwenyeji wake Kansela Angela Merkel wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin.
Rais Obama na mwenyeji wake Kansela Angela Merkel wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin.Picha: Jewel Samad/AFP/Getty Images

"Vitisho vya sasa siyo kama ilivyokuwa nusu karne iliyopita, lakini mapambano yanaendelea," alisema. "Na nimekuja hapa katika mji huu wa matumaini kwa sababu mitihani ya wakati wetu inatutaka tuwe na roho ya kupambana ambayo mji wa Berlin ulikuwa nayo nusu karne iliyopita."

Mkutano wa nyuklia mwaka 2016

Obama alisema Marekani inaandaa mkutano mwaka 2016, kuhusu juhudi za usalama wa silaha za nyuklia zisizo hifadhiwa vizuri duniani kote, na kuongeza kuwa utawala wake utajitahidi kutafuta uungwaji mkono nchini Marekani, kuridhia Mkataba wa unaopiga marufuku majaribio ya silaha za nyuklia.

Umati wa wageni waalikwa karibu 6000 walivumilia jua kali kushangilia mapendekezo ya Obama kuhusu silaha za nyuklia, na dhamira yake ya kuongeza mara mbili, juhudi za kufunga gereza la Guantanamo lililoko nchini Cuba.

Obama aliondoka mjini Berlin kwa ndege yake ya Air Force One majira ya saa nne usiku, na kuhitimisha ziara iliyodumu kwa masaa 25, katika jiji ambalo wakati mmoja lilikuwa mahali pa hatari kati ya muungano wa kisovieti na mataifa ya magharibi, na ambako vita baridi vilitisha mara nyingi kuripuka katika vita vingine vya dunia. Utawala wa Kikomunisti wa Ujerumani Mashariki ulijenga ukuta wa Berlin, ambao uliugawa mji huo kati ya mashariki na magharibi mwaka 1961.

Wanaharakati wa Amnesty International walifanya maandamano kupinga kuendelea kuwepo kwa gereza la Guantanamo.
Wanaharakati wa Amnesty International walifanya maandamano kupinga kuendelea kuwepo kwa gereza la Guantanamo.Picha: Reuters

Lango la Brandenburg, ambako Obama alitoa hotuba yake, ni jengo la tao lenye njia tano, ambalo wakati mmoja lilisimama karibu na ukuta wa Berlin. Ukuta huo ulifunguliwa Novemba mwaka 1989, na ulivunjwa katika miezi iliyofuata, na Ujerumani iliungana tena mwaka 1990.

Mwaka 1994 rais Bill Clinton alikuwa wa kwanza kutoa hotuba kwa Berlin iliyoungana, na kama Obama, yeye pia alizungumza katika uwanja wa Pariser, katika upande wa mashariki wa lango hilo, akiahidi kuwa ubalozi mpya wa Marekani ungejengwa katika upande wa pili. Ubalozi huo ulinfunguliwa mwaka 2008.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae

Mhariri: Josephat Nyiro Charo