1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama afanya ziara ya ghafla Afghanistan

2 Mei 2012

Rais wa Marekani Barack Obama amefanya ziara ya ghafla nchini Afghanistan, na kuahidi kukamilisha kazi na kumaliza vita hivyo. Rais Obama pia amesaini makubaliano ya ushirikiano na mwenzake wa Afghanistan Hamid Karzai

https://p.dw.com/p/14nmf
Rais Barack Obama
Rais Barack ObamaPicha: AP

Ziara ya Rais Barack Obama imekuja siku ambayo ni mwaka mmoja kamili tangu wanajeshi wa Marekani walipomuuwa kiongozi wa mtandao wa al Qaida, Osama bin Laden nchini Pakistan. Imefanyika pia huku Obama akiwa katika kampeni ya kuwania muhula wa pili wa kuiongoza Marekani.

Kwanza alisaini makubaliano na mwenzake wa Afghanistan Hamid Karzai, ambayo yanahusu ushirikiano baina ya Marekani na Afghanistan mnamo kipindi cha miaka kumi baada ya vikosi vya Marekani kuondoka mwaka 2014.

Obama na Karzai wakisaini makubaliano
Obama na Karzai wakisaini makubalianoPicha: AP

Usalama mikononi mwa waafghanistan

Rais Obama amesema kulingana na makubaliano hayo, Marekani itahusika katika harakati za kupambana na ugaidi na kutoa mafunzo kwa jeshi la Afghanistan, lakini akabainisha kuwa Marekani haitakuwa na majukumu ya usalama kwa Afghanistan.

''Katika makubaliano haya, tutawafikiana na waafghanistan juu ya msaada wanaouhitaji kuweza kutimiza majukumu ya kiusalama baada ya mwaka 2014. Tutasaidia kupambana na ugaidi, na tutaendelea kutoa mafunzo. Lakini hatutajenga vituo vya jeshi vya kudumu, wala kufanya doria kwenye miji na milimani. Hiyo itakuwa kazi ya watu wa Afghanistan.'' Alisema Rais Obama.

Vita kuishia vilikoanzia

Ndege yake ilitua kwenye uwanja wa Bagram usiku, na kisha akasafiri kwa helikopta kwenda Kabul kusaini makubaliano na Karzai, kabla ya kurudi kwenye kambi ya jeshi, ambako ametoa hotuba iliyorushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni, hadi kwa wapiga kura nchini Marekani.

Obama aliwaambia wanajeshi kuwa vita vilianzia Afghanistan, na ndiko vitakakoishia. Alisema, ''Kwa kuwekeana imani miongoni mwetu, huku macho yetu yakielekezwa kwenye mustakabali, tutamaliza vita hivi, na kujenga amani ya kudumu''. Obama aliongeza kuwa anafahamu kwamba wamarekani wengi wamechoka na vita.

Katika ziara hiyo ya saa takribani saba, Rais Obama aliwatembelea wanajeshi waliolazwa katika hospitali ya Bagram.

Ziara yake yasindikizwa na miripuko

Kama kudhihirisha jinsi suala la amani lilivyo tete nchini Afghanistan, saa chache baada ya Rais Obama kuondoka, mji mkuu, Kabul ulikabiliwa na mlolongo wa miripuko na risasi kufyetuliwa, ambapo kwa uchache watu sita wameuawa. Mashambulizi yalifanyika karibu na kituo cha ulinzi binafsi, na ambacho hukaliwa na wafanyakazi wa kimataifa.

Saa chache baada ya ziara ya Obama, mji mkuu, Kabul, ulikumbwa na miripuko
Saa chache baada ya ziara ya Obama, mji mkuu, Kabul, ulikumbwa na miripukoPicha: Reuters

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani Sediq Sediqi amesema kuwa mripuko mmoja ulisababishwa na mtu wa kujitolea mhanga. Wanamgambo wa Taliban wamedai kuhusika na mashambulizi hayo.

Mitt Romney, mgombea wa chama cha Republican ambaye anatarajiwa kuwa mpinzani wa Obama katika kinyang'anyiro cha urais baadaye mwaka huu, ambaye alikuwa mjini New York akitembelea eneo la mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001, ambayo yalisababisha vita vya Afghanistan, alimshutumu Obama kutumia mshikamano wa kitaifa uliofuatia kuuawa kwa Osama bin Laden kwa maslahi yake ya kisiasa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/APE

Mhariri:Hamidou Oummilkheir