1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama aiadhibu Urusi kuhusiana na udukuzi

Iddi Ssessanga
30 Desemba 2016

Rais wa Marekani Barack Obama ameamuru kufukuzwa maafisa 35 wa Urusi na kuyawekea vikwazo mashirika ya ujasusi kuhusiana na udukuzi wa mitandao ya taasisi za kisiasa katika uchaguzi mkuu. Urusi imetishia kulipa kisasi.

https://p.dw.com/p/2V37Z
China Treffen Putin Obama
Picha: picture-alliance/Sputnik/A. Druzhinin

Hatua hizo zilizochukuliwa katika siku za mwisho wa utawala wa Obama, zinaashiria kiwango kipya cha chini kabisaa katika uhusiano wa Marekani na Urusi baada ya vita baridi, na zimeweka uwezekano wa mvutano kati ya rais ajaye Donald Trump na Warepublican wenzake wanaodhibiti bunge la Congress, juu ya namna ya kuishughulikia Urusi.

Obama ambaye ni kutoka chama cha Democratic, aliahidi kuchukuwa hatua baada ya maafisa wa uchunguzi kuilaumu Urusi kwa udukuzi uliolenga kushawishi matokeo ya uchaguzi wa rais. Maafisa walimnyoonshea kidole moja kwa moja rais Vladmir Putin kwa kuongoza binafsi udukuzi huo, ukiwalenga hasa wanasiasa wa chama cha Democratic, ambao walimtia kishindo Obama kuchukuwa hatua.

"Hatua hizo zinafutia onyo za siri na za wazi tulizozitoa mara kwa mara kwa serikali ya Urusi, na ndiyo majibu stahiki dhidi ya juhudi za kuhatarisha maslahi ya Marekani kwa kukiuka utaratibu uliowekwa kimataifa," Obama alisema katika taarifa kutoka mapumzikoni mjini Hawaii, na kuongeza kuwa Wamarekani wote wanapaswa kustushwa na vitendo vya Urusi.

USA Donald Trump in Palm Beach
Rais Mteule Donald Trump kuwasikiliza wakuu wa idara za ujasusi kuhusiana na ripoti ya udukuzi wa Urusi.Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Harnik

Wanadiplomasia wapewa saa 72 kuondoka

Obama alisema Warusi hawataruhusiwa kuyatumia tena majengo mawili yanayomilikiwa na serikali ya Urusi yalioko Maryland na New York na serikali imetoa muda wa msaa 72 kwa maafisa wa Urusi waliotuhumiwa kuondoka marekani pamoja na familia zao. Mashirika ya Ujasusi ya Marekani yamehitimisha kwamba  lengo la Urusi lilikuwa kumsaidia Donald Trump kushinda uchaguzi - tathmini ambayo Trump ameipinga kama kichekesho.

Na haijabainika wazi iwapo Trump, ambaye amemsifu Putin mara kwa mara, na kuwateuwa watu wanaoonekana kama marafiki wa serikali ya Moscow katika nyadhifa za juu serikalini, atataka kufuta hatua hizo pale atakapochukuwa madaraka Januari 20. Trump hata hivyo alisema siku ya Alhamisi kuwa angekutana na maafisa wa idara za ujasusi kupata maelezo zaidi.

Wabunge wa vyama vya Democratic na Republican wameelezea wasiwasi juu ya vitendo vya Urusi, na hivyo kuweka uwezekano wa upinzani iwapo Trump atajaribu kuondoa hatua hizo. Spika wa baraza la wawakilishi Mrepublican Paul Ryan, alisema Urusi imekuwa ikitaka kudhoofisha maslahi ya Marekani na kusema vikwazo hivyo vimechelewa. Maseneta wa chama cha Republican John McCain na Lindsay Grahama, walisema wanakusudia kuongoza juhudi bungeni kuiwekea Urusi vikwazo vikali zaidi.

"Nina wasiwasi juu ya nini kitatokea nchini Ufaransa, Ujerumani kuhusiana na ushiriki wa Urusi. Lakini tunahitaji kuweka msimamo, na hilo litahitaji maumivu kidogo. Vikwazo tunavyovitaka vitakuwa vya kidukizi zaidi kuliko vya sasa. Vitaiumiza Urusi zaidi," alisema Graham katika mkutano na waandishi wa habari.

Washington Russische Botschaft
Muonekano jumla wa ubalozi wa Urusi mjini Washington, Marekani Desemba 30,2016.Picha: picture-alliance/AA/Y. Ozturk

Kremlin yaahidi kujibu katika kiwango sawa

Ikulu ya Kremlin ambayo imelaani vikwazo hivyo na kuvitaja kuwa kinyume cha sheria na kuahidi kujibu ipasavyo, imehoji iwapo Trump ataidhinisha vikwazo hivyo vipya.  Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov ameutuhumu utawala wa Obama kw akujaribu kuharibu kabisaa uhusiano wa Marekani na Urusi, na kuahidi Moscow itajibu vile inavyostahiki.

Maafisa wa Marekani wamesema wana taarifa kwamba Urusi imeifunga shule ya Anglo-Amerika katika mji mkuu Moscow, ambayo inahudhuriwa zaidi na watoto wa wanadiplomasia, lakini hawakuweza kuthibitisha ripoti hizo.

Trump amehoji iwapo kweli Urusi ilibadili mwelekeo wa matokeo, akizikosoa tuhuma za Obama kama juhudi za Rais wa chama cha Democratic kuharamisha ushindi wa Mrepublican. Wakati tayari Trump amepokea taarifa za kiintelijensia kuhusu uchaguzi na ushahidi wa kutosha umewekwa hadharani, ahadi yake ya kukutana na wakuu wa mashirika ya ujasusi inaweza kutoa fursa ya kulegeza msimamo wake.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe, rtre.

Mhariri: Josephat Charo