1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama arudi Washington baada ya likizo

MjahidA18 Agosti 2013

Rais Barrack Obama wa Marekani anarejea mjini Washington leo hii(18.08.2013) baada ya likizo fupi. Hata hivyo kurudi kwake kutoka likizoni kunatarajiwa kuwa ndio mwanzo wa kupambana na siasa za chama cha Republicans.

https://p.dw.com/p/19Re9
Rais wa Marekani Barrack Obama
Rais wa Marekani Barrack ObamaPicha: Reuters

Wiki iliopita Rais Obama alilazimika kujitokeza mbali ya kuwa katika likizo yake ya siku nane na kutoa tamko juu ya oparesheni dhidi ya waandamanaji inayofanywa na jeshi la Misri.

Lakini kutokana na ghasia nchini humo na pia kufanyika kwa mkutano wa viongozi wa nchi 20 zenye viwanda na zinazoinukia kiviwanda unaofanyika nchini Urusi mapema mwezi ujao, huenda mambo hayo mawili yakawekwa kando kidogo ukilinganisha na ajenda za nchini Marekani kwenyewe ambako chama cha Republican kimetishia kusitisha shughuli za serikali mwezi wa Oktoba kutokana na bajeti ya nchi hiyo pamoja na ukomo wa serikali kuweza kukopa.

Chama cha Republican kina viti vingi katika baraza la wawakilishi na kina ushawishi mkubwa pia katika bunge la Marekani jambo ambalo linaweza kuwawezesha kutopitisha ama kuzuia bajeti itakayowasilishwa kabla ya kuanza kwa mwaka mpya wa bajeti unaoanza Oktoba mosi.

Rais wa Marekani Barrack Obama akizungumzia Misri
Rais wa Marekani Barrack Obama akizungumzia MisriPicha: Reuters

Tangu chama cha Republican kilipopata tena udhibiti wa baraza la wawakilishi mwaka 2011 kimekuwa kikitishia kuizuwia serikali kufanya shughuli zake na kuingia katika mvutano na Rais Obama kabla ya kuondoa wazo lao hilo katika dakika za mwisho.

Hata hivyo mwaka huu vigogo wa chama hicho wamesema hawatorudi nyuma katika mipango yao kwani wanania ya kuvuruga mpango mkubwa wa mabadiliko katika sekta ya afya uliopendekezwa na rais Obama.

Raia wa Marekani wasiokuwa na bima ya afya wanaweza kuanza kujisajili katika masoko katika kila jimbo ambalo serikali itatoa ruzuku kuanzia Oktoba Mosi.

Hata hivyo baadhi ya wanachama wa Republican wenye takriban jumla ya kura arobaini zinazoweza kubadili sheria ya mpango huo wa afya wa rais Obama wameapa kuzuia bajeti yoyote ambayo itagharamia malipo ya bima ya afya.

Maoni zaidi juu ya nia ya chama cha Republican

Kwa upande wakeThomas Mann, msomi katika taasisi ya Brookings amesema iwapo chama hicho kitafanya hivyo basi kitakuwa kimetenda kosa kubwa sana linaloweza kuwa na athari kubwa katika nchi ya Marekani.

Siku ya Alhamisi na Ijumaa Rais Obama anatarajiwa kuwa katika ziara ya siku mbili akitumia basi kuzunguka katika maeneo ya nchi akitangaza mpango wake juu ya uchumi wa nchi .

Baadhi ya wafuasi wa chama cha Republican katika uchaguzi wa mwaka jana
Baadhi ya wafuasi wa chama cha Republican katika uchaguzi wa mwaka janaPicha: Reuters

Awali Agosti Obama aliwaambia waandishi habari kuwa nia ya kutaka kuizuwia serikali kutekeleza majukumu yake na kuzuia takriban watu milioni 30 kupata huduma za afya ni jambo baya.

"Kitu unachopaswa kufikiria ni namna ya kuwezesha kuinua maisha ya watu wa kima cha chini kuendelea mbele pamoja na watoto wao." Alisema Obama.

Rais huyo anataka kufuta utaratibu ambapo walipa kodi matajiri hupewa muda wa kutolipa kodi, na pia kufanya mabadiliko mfumo wa kodi ya makampuni makubwa huku akiwekeza katika masuala ya miundo mbinu na elimu jambo linalopingwa vikali na chama cha Republican.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Sekione Kitojo