1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama asema Gaddafi ni sharti aondoke madarakani

20 Mei 2011

Rais wa Marekani Barrack Obama amesema kuwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi ataondoka madarakani apende asipende au aondolewe kwa nguvu.

https://p.dw.com/p/11KGO
Rais Barack ObamaPicha: AP

Hayo yalijri huku Jumuiya ya kujihami ya NATO ikitangaza kuwa imeviharibu pakubwa vifaa vya kivita vya kiongozi huyo wa Libya.

Matamshi ya Rais wa Marekani Barrack Obama yalijiri wakati ndege za jumuiya ya kujihami ya NATO zikizishambulia manowari za kivita za vikosi vya Gaddafi katika bandari za Tripoli, Al Khums na Sirte usiku wa kuamkia leo na kuulemaza uwezo wa kiongozi huyo kuendelea kukwamia madaraka.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon naye alisema kuwa juhudi za kutafuta mwafaka wa usitishaji vita nchini Libya zimegongwa mwamba na mzozo wa kibinadam unazidi kutokota. Waasi wanopigana kumng'atua Gaddafi mamlakani pia walisema kuwa wana wasiwasi kuhusu hali ya kibinadam katika eneo la milima la Nafusa hata baada ya kutwaa udhibiti wa mji wa Magharibi wa Misrata.

Katika hotuba yake ya hapo jana kuhusiana na wimbi la mageuzi katika ulimwengu wa kiarabu, ambalo limewatimua uongozini marais wa Tunisia, Misiri na linawasakama Marais wa Syria na Yemen, Rais Obama alisema kuwa muda unazidi kumpa kisogo Gaddafi.

NO FLASH Gaddafi Gadhafi Libyen Haftbefehl
Kiongozi wa Libya Kanali Muammar GaddafiPicha: AP

Alisema Gaddafi sasa hana udhibiti juu ya nchi yake akiongeza kuwa upinzani nchini humo umeunda baraza halali la serikali ya mpito ambalo lina makao yake katika eneo la Kaskazini mwa nchi hiyo la Benghazi.

Matamshi ya Rais Obama ya kulitambua baraza hilo la waasi yalikaribishwa na naibu mwenyekiti wake Abdul Hafiz Ghoga. Alisema wanataraji kuungwa mkono na marekani na hata jamii ya kimataifa ili kuwasaidia kuendeleza na kutimiza maono yao ya kidemokrasia na kwa maendeleo ya watu wa taifa hilo.

Katibu mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen awali alisema majeshi ya Gaddafi yalikuwa yamelemewa na hali hiyo inaweza kuufikisha kikomo utawala wa Gaddafi. Mashambulizi ya NATO siku ya Alhamis yalilenga bandari ya mji mkuu wa Tripoli na kuharibu meli nane za Gaddafi.

Wakati huo huo kiongozi wa muungano wa Afrika Jean Ping alisema kuwa azimio la Umoja wa Mataifa la kuidhinisha matumizi ya nguvu ili kuwalinda raia nchini Libya limekiukwa. Hali ya Gaddafi imekuwa ya wasiwasi baada ya mwito wa mwendesha mkuu wa mashtaka wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC Luis Moreno Ocampo wa kutaka vibali vya kukamatwa kwa Gaddafi, mwanawe wa kiume seif al islam na shemejiye Abdullah Al Senusi kwa tuhuma za kutekeleza maovu dhidi ya binadam.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri:MirajiOthman