1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama atangaza mkakati mpya Afghanistan

Nina Markgraf27 Machi 2009

Rais Barack Obama ametangaza rasmi mpango wake wa kuwatuma wanajeshi 4,000 zaidi nchini Afghanistan. Obama aliungama kwamba hali Afghanistan ni mbaya.

https://p.dw.com/p/HLIt
Rais wa Marekani, Barack Obama.Picha: picture-alliance / dpa


Akitangaza mpango huo rais Obama alisema ni zaidi ya miaka saba sasa tangu wataliaban waon´golewe madarakani, lakini bado waasi wanayadhibiti maeneo kadhaa ya Afghanistan na Pakistan.

Akaongeza kwamba mashambulio dhidi ya wanajeshi ya marekani, washirika wa jumuiya ya kujihami ya NATOP na wale wa serikali ya Afghanistan yameongezeka hatua kwa hatua, na kwamba kinachoumiza zaidi ni kuwa mwaka 2008 ulikua mwaka wa vifo vingi zaidi vaya wanajeshi wa Marekani katika vita hivyo.

Obama akaonya kwamba magaidi wa Al Qaeda wanaandaa mashambulio mapya dhidi ya Marekani kwa kutokea Afghanistan na kuitaka nchi hiyo kuwa mshirika imara katika mapambano dhidi ya wanaharakati na kuwatoa kutoka kwenye mapango wanamo jihifadhi. Akasema jukumu lake ni kuwalinda raia wa Marekani na nchi yake haiana lengo la kuitawala Afghanistan.


Obama pia alitoa wito wa ushirikiano wa jamii ya kimataifa akisema hali tete nchini Afghanistan sio mzigo tu kwa Marekani bali pia ni tishio la usalama kwa ulimwengu mzima.


'' Kama rais, jukumu langu ni kuwalinda raia wa Marekani. Hatupo nchini Afghanistan kuitawala, tupo Afghanistan kuabiliana na adui anayetishia kuangamiza raia wa Marekani, washirika wetu na marafiki zetu, na hasa raia wa Afghanistan na Pakistan ndio wameumia sana na tishio la magaidi. Hivyo nataka raia wa Marekani waelewe kuwa hatutachoka hadi tuwaangamize magaidi Afghanistan na Pakistan.'' Alisema Obama.


Kiongozi huyo wa Marekani alisema washirika wa NATO, Iran, Urusi,China India zote zina jukumu katika suala la usalama nchini Afghanistan na Pakistan.


Aidha alikua pia na ujumbe kwa serikali ya Afghanistan akisema kamwe hatovumilia kuendelea kwa rushwa serikalini na kuwataka washirika wa Marekani kuwapa uungaji mkono mkubwa zaidi raia wa Afghanistan.


Pakistan imeukaribisha mpango huo mpya wa Marekani kuelekea Afghanistan na kuahidi kushirikiana na taifa hilo ikisema utawala wa rais Obama una muelekeo muafaka kuhusiana na hali ya mambo katika eneo hilo.


Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Pakistamn Shah Mehmood Qureshi alisema nchi yake iko tayari kutoa mchango madhubuti kwa sababu inahisi amani na usalama wake unafungamana na Afghanistan.

Wakati huo huo Urusi imesema iko tayari kutoa ushirikiano mkubawa zaidi katika mgogoro wa Afghanistan. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov aliuambia mkutano wa kimataifa kuhusu Afghanistan unaofanyika mjini Moscow kwamba nchi yake iko tayari kushirikiana zaidi na NATO, ambayo majeshi yake yanakabiliwa na kitisho kinachoongezeka kutoka kwa wapiganaji wa Al-Qaeda na washirika wao.


Urusi, Marekani, Iran ,China na nchi jirani na Afghanistan za eneo la Asia ya kati zinashiriki katika mkutano huo. Pia Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon na waakilishi wa nchi zilizoendelea kiviwanda za kundi la G7. Marekani imemtuma waziri wake mdogo wa mambo ya nchi za nje, lakini hakuna ratiba yoyote iliotangazwa juu ya uwezekano wa kukutana na maafisa wa Iran.


Mwandishi Munira Muhammad/ AFP


Mhariri: Mohammed Abdulrahman