1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama atoa mwito wa ushirikiano

Abdu Said Mtullya26 Januari 2011

Rais Obama atumia hotuba yake kwa taifa kuwataka wajumbe wa chama chake cha Democratic na wale wa Republican kushirikiana katika utatuzi wa matatizo ya nchi, badala ya ushindani na misimamo mikali ya kisiasa.

https://p.dw.com/p/104sz
Rais Barack Obama
Rais Barack ObamaPicha: AP

Rais Barack Obama amevitaka vyama vya Democratic na Republican vishirikiane ili kuiwezesha Marekani kupambana na changamoto zinazoikabili. Rais Obama aliyasema hayo katika hotuba yake juu ya hali ya nchi.

Rais Obama amewataka Wamarekani warejeshe uwezo wa ushindani duniani kwa kuekeza katika maendeleo ya elimu, utafiti na miundombinu.

Katika hotuba hiyo, Obama alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na kusema kuwa haitoshi kuketi pamoja tu, bali kinachohitajika ni kufanya kazi pamoja.Alieleza kuwa wapiga kura wameligawanya jukumu la serikali kwa vyama vya Democratic na Republican.

Katika hotuba yake Rais Obama pia alizungumzia juu ya masuala ya uchumi, ukosefu wa ajira nakisi,na changamoto za kimataifa.Ili kuzikabili changamoto hizo Obama amewataka wananchi wake wapanie ili kuirejesha Marekani katika nafasi ya mbele duniani.

Ameeleza kuwa Marekani inahitaji elimu na ubunifu ili kuwa mbele duniani.Amesema pana haja ya kuhakikisha kwamba Marekani inakuwa mahala bora pa biashara kuliko pengine popote duniani.

Rais Obama pia amesema, lazima Marekani ichukue hatua ili kupunguza nakisi.Ameeleza kuwa lazima Marekani iwajibike katika kuikabili nakisi na kufanya marekebisho katika serikali.Hata hivyo Rais Obama aliwaambia wamarekani kuwa nchi yao sasa inatarajia kusonga mbele katika maendeleo baada ya mgogoro mkubwa wa uchumi usiokuwa na mithili katika historia ya nchi.

Huku akishangiliwa Rais Obama aliwataka wabunge wa chama cha Republican washiriki katika juhudi za pamoja za kuyatatua matatizo yanayoikabili Marekani.

Katika hotuba yake Rais Obama pia alizungumzia sera za nje.Kuhusu Afghanistan alisema kuwa mafanikio yamepatikana kutokana na wanajeshi wa Marekani kuwakabili wapinzani kwa uthabiti kiasi cha kuwafanya wabakiwe na maeneo machache wanayoyadhibiti.Hata hivyo amesema bado Marekani itakabiliwa na kazi ngumu katika siku za usoni.Lakini ameeleza kuwa lengo la Marekani ni kuwazuia taliban kuidhibiti Afghanistan.

Juu ya matukio ya nchini Tunisia Obama alitamka kuwa, Marekani inawaunga mkono watu wa nchi hiyo na shabaha za kidemokrasia wanazoziwania.

Rais Obama ametoa hotuba hiyo wakati ambapo umaaruf wake umepanda tena kutokana na kufanikiwa kupitisha sheria kadhaa bungeni.

Mwandishi/Bergmann/ZAR

Tafsiri Mtullya Abdu/

Mhariri/Abdul-Rahman.