1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama awaalika Viongozi wa Kiarabu White House.

22 Aprili 2009

Rais wa Palestina Mahmoud Abbas, atakutana na rais Barack Obama mjini washington mwezi ujao.

https://p.dw.com/p/Hbph
Rais Barack Obama akutana na Mfalme Abdullah wa pili wa Jordan huko White House.Picha: AP


Katika mkutano na mfalme Abdullah wa pili wa Jordan, Obama aliwaalika viongozi wa nchi za kiarabu na Israel kwenda Marekani kujaribu kupiga jeki juhudi ya kutafuta amani Mashariki ya Kati.


Tangu kuingia madarakani Utawala wa Obama, umekuwa mstari wa mbele kupigia debe kuundwa kwa nchi mbili ya Palestina na Israel zitakazoishi pamoja kama njia ya pekee ya kusuluhisha mzozo wa Mashariki ya kati.


Na sasa utawala huu unatia gea ya juu, kuhakikisha kuna nia njema kutoka kwa wahusika wote.


Symbolbild Netanjahu und Abbas Frieden
Mahmoud Abbas, rais wa Palestina na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Akimpokea mfalme Abdullah wa pili wa Jordan, kwa mazungumzo kusikiliza msimamo wa nchi za kiarabu kuhusiana na Mashariki ya kati- Obama akapiga hatua nyingine kuwaalika ikulu ya White House, waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ,rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas na rais Hosni Mubarak wa Misri.


Kumekuwa na wasiwasi kuhusiana na kuuundwa kwa taifa la Palestina, tangu Israel ipate waziri mkuu mpya Benjamin Netanyahu. Netanyahu ingawa ameashiria yupo tayari kwa kufufua mazungumzo ya amani- hajaunga mkono pendekezo la kuundwa kwa taifa la Palestina.


Ni katika muktadha huu wa ati ati ndio Obama amewaalika, viongozi wa kiarabu na Israel mjini Washington kujua upi muelekeo.


Viongozi hawa hata hivyo hawatokuwa pamoja White House, kila mmoja atapata fursa yake pekee yake katika mkutano White House.


Kulingana na afisa mkuu wa Kipalestina, rais wa Palestina Mahmoud Abbas atakutana na Obama tarehe 28 mwezi ujao.


Hillary Clinton
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton.Picha: AP

Wakati huo huo, sera mpya ya Obama, ya mashauri ya kigeni itakabiliwa na mtihani wake wa kwanza leo, pale waziri wa mashauri ya kigeni Hillary Clinton atzakapofika mbele ya bunge la Congress kuelezea kinaga ubaga sera ambazo wamezichukua hadi kufikia sasa katika yale mageuzi ya kutoa sura mpya ya Marekani.


Masuala ambayo Clinton anatarajiwa kugusia ni swala la Mashariki ya kati, sera zao mpya kuhusu Iraq, Iran na Afghanistan na Pakistan.


Mwandishi: Munira Muhammad/ AFP

Mhariri: AbdulRahman